Same. Jimbo Katoliki la Same limeipunguzia hadhi Parokia ya Ugweno, iliyoko wilayani Same mkoani Kilimanjaro na kuifanya kuwa kigango. Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kubainika waamini wa parokia hiyo kutokuwa na ushirikiano na Paroko wao.
Hali hiyo imetajwa kuathiri utendaji wake wa kazi za kitume na za jimbo kwa ujumla.
Uamuzi huo ulitangazwa jana Alhamisi Aprili 17, 2025 na Askofu wa Jimbo hilo, Rogath Kimario alipokuwa akiadhimisha Misa Takatifu ya sikukuu ya Mapadri iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kristo Mchungaji Mwema, mjini Same, siku ambayo alibariki pia mafuta ya Krisma.
Taarifa kuhusu uamuzi huo, ilisambaa haraka katika mitandao ya kijamii ikieleza kuwa moja ya sababu kuu za kushushwa hadhi kwa parokia hiyo ni kushindwa kwa waumini kumhudumia ipasavyo Paroko wao, Padri Ernest Mkwizu, ikidaiwa kuwa wameshindwa kumpatia mahitaji yake ya msingi.
Baada ya kushushwa hadhi, Parokia hiyo ya Ugweno sasa itaunganishwa na vigango vya Mavaa’nja na Kikweni kuunda Parokia mpya ya Kikweni.
Paroko wa parokia hiyo mpya, tayari ametangazwa ni Padri Mkwizu, ambaye pia atatoa huduma katika eneo la Vuchama.
Akizungumza na Mwananchi mmoja wa mapadri waliokuwepo wakati askofu akitoa taarifa hiyo, Padri Salvatory Kisela, alithibitisha taarifa hiyo kusomwa jana kanisani.
“Ni kweli baba Askofu Kimario kaishusha hadhi Parokia ya Ugweno kuwa kigango baada ya waumini kushindwa kumtunza Paroko wao. Taarifa hiyo ilitolewa rasmi wakati wa misa ya kuwekwa wakfu kwa mafuta ya wakatekumeni, wagonjwa na krisma katika Kanisa Kuu la Same,” amethibitisha padri huyo.
Taarifa hiyo imeibua hisia mseto miongoni mwa waumini wa kanisa hilo, huku baadhi wakieleza masikitiko yao.
Crecensia Lukas muumini wa parokia hiyo iliyoshushwa hadhi, ametoa wito wa mshikamano miongoni mwa waumini.
“Kanisa linahitaji umoja na mshikamano ili kazi ya Mungu iendelee. Tunaposhindwa kufanya hivyo tunawavunja moyo viongozi wetu wa kiroho. Hili ni jambo la kujifunza, sisi waumini tunapaswa kujitathmini na kushikamana na viongozi wetu ili tusiliangushe Kanisa,” amesema.