………………
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango ametoa rai kwa wazazi hususani wakinamama kuwaongoza watoto wao hasa
vijana kuacha tabia ya kushabikia vurugu wakati wa kampeni na Uchaguzi Mkuu
utakaofanyika mwaka huu.
Makamu wa Rais ametoa rai hiyo mara baada ya kushiriki Ibada ya Sikukuu
ya Pasaka katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa
Ledochowska Kiwanja cha Ndege Dodoma. Amewasihi Watanzania kushiriki Uchaguzi
Mkuu kwa amani na utulivu kwa kuwa vurugu sio sehemu ya jadi ya Watanzania.
Aidha Makamu wa Rais ametoa wito kwa wote watakaopata dhamana ya
kusimamia uchaguzi kuhakikisha wanazingatia sheria na miongozo watakayopewa
pamoja na kutenda haki kwa wote watakaojitokeza kugombea nafasi mbalimbali
katika uchaguzi huo.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amewasihi watumiaji wa vyombo vya moto
kuwa na busara na umakini katika matumizi ya vyombo hivyo ili kuepusha kupoteza
Maisha ya watu barabarani.
Makamu wa Rais amewatakia heri na baraka watanzania wote katika kusherehekea
Sikukuu ya Pasaka na kuwasihi kusherehekea kwa amani na furaha.
Ibada hiyo iliyohudhuriwa pia na Mwenza wa Makamu wa Rais Mama
Mbonimpaye Mpango imeongozwa na Padre Dionis Paskal Safari.