Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu amechukua fomu kugombea urais kupitia chama hicho katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Kiongozi huyo ndani ya chama hicho anakuwa wa pili kuomba ridhaa ya kuongoza Tanzania, baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, Othman Masoud Othman kuchukua na kurejesha fomu Aprili 13, 2025 akiomba kuteuliwa kuwania urais wa Zanzibar.
Semu anatupa karata yake kwenye uchaguzi mkuu Oktoba, kuchuana na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye tayari chama chake kimempa baraka kuendelea awamu nyingine ya kuomba ridhaa kwa wananchi kurejea madarakani.
Siyo Rais Samia pekee, bali Semu atachuana na Doyo Hassan aliyechukua fomu akiomba chama NLD kimteue kuwania urais wa Tanzania.
Taarifa za kuchukua fomu kwa kiongozi huyo imetolewa na Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, ACT Wazalendo, Shangwe Ayo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Semu amekabidhiwa fomu hiyo na katibu wa Oganaizesheni, Mafunzo na Uchaguzi wa Chama cha ACT Wazalendo, Shaweji Mketo leo Aprili 22, 2025 katika Ofisi za Makao Makuu ya ACT Wazalendo zilizopo Dar es Salaam.
Kulingana na taarifa Semu, baada ya kukabidhiwa fomu amesema, “Nimechukua fomu hii kama ishara ya utayari wangu wa kumkabili Rais Samia Suluhu Hassan na CCM kwa sababu wameshindwa kuendesha nchi na kuwakomboa Watanzania kiuchumi, kisiasa na kijamii.”
Nimechukua fomu kama ishara ya utayari wangu wa kuongoza mapambano ya kulinda thamani ya kura na misingi ya demokrasia nchini,” amesema.
Dorothy amesema atatoa dira na maono yake yaliyomsukuma kuchukua fomu, kupitia hotuba kwa taifa atayoitoa siku ya kurudisha fomu atayoitangaza hivi karibuni.
Akitangaza nia Januari 16, Semu alisema uzoefu alionao kwenye uongozi ni turufu anayoamini itambeba.

“Nipo kwenye uongozi na kwenye siasa kwa miaka 10 naamini nimeiva, pia nipo kwenye chama chenye sera na ilani bora, kinaonyesha tofauti na kujisimamia chenyewe.
“ACT ina miaka 10 tangu kuanzishwa, kinazidi kukua kwa kasi na kutekeleza masuala mbalimbali kama chama makini chenye mikakakati bora na endelevu. Mikakati hii inatuongoza katika hatua ya kwenda kushika dola na itatuletea matokeo bora na kutupa majimbo ya kutosha kuunda Serikali,” alisema.