Dodoma. Wakati wa kuhitimisha mjadala wa leo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema kuna ombi la Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo anataka kusema jambo.
Amesema kwa kutumia kanuni namba 70 ya kanuni za Kudumu za Bunge Tolea la Februari 2023 anampa nafasi ya kusema ambayo inasema kutokusema uongo Bungeni.
Mapema leo Jumatano Aprili 23, 2025, Spika aliagiza Mbunge huyo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Mohamed Mchengerwa wakasikilizwe na Kamati ya Maadili, Kinga na Madaraka ya Bunge baada ya kuwa na mabisho kuhusu tuhuma ambazo zilikuwa zimeibuliwa kutoka Arusha.
“Mheshimiwa Spika, utakumbuka ilitokea sintofahamu leo asubuhi. Baada ya kukaa na kutafakari nimeona niombe radhi,” amesema Gambo.
Gambo amesema katika kipindi cha asubuhi ulitokea aliouita mtifuano ambao hakutaja nini maana yake.
Mbunge huyo amesema hawezi kuendelea zaidi kwani makofi ya wabunge yameonyesha kuwa wamemsamehe hivyo anaomba aishie hapo asije akaharibu.