Bosi Yanga Afichua Siri Mzize Kuumia – Global Publishers


Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga

LICHA ya Clement Mzize mshambuliaji wa Yanga kuchaguliwa kuwa mchezaji bora kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Fountain Gate imefichuka kuwa alikuwa ameumia hivyo kulikuwa na hatihati kuukosa mchezo huo.

Katika mchezo huo uliochezwa Aprili 21 2025, Uwanja wa Tanzanite Kwaraa baada ya dakika 90 ubao ulisoma Fountain Gate 0-4 Yanga, Mzize alifunga mabao mawili dakika ya 38 kwa mguu wa kulia akiwa ndani ya 18 baada ya makosa ya kipa John Noble kutema mpira wa faulo iliyopigwa na Aziz Ki.

Mzize alifunga bao jingine dakika ya 69 akitumia pasi ya Jonathan Ikangalombo akiwa ndani ya 18 akifikisha mabao 13 ndani ya ligi. Aziz Ki alipachika bao moja dakika ya 43 kwa mguu wa kushoto akiwa ndani ya 18 baada ya kipa John aliyekuwa ametoka ndani ya 18 kutoa pasi iliyokutana na Ki.

 

Clement Mzize mshambuliaji wa Yanga

Kiungo ambaye alianzia benchi kwenye mchezo huo Clatous Chama alipachika bao moja kwa pigo la faulo dakika ya 89 akitumia mguu wa kulia. Hivyo walikomba pointi tatu mazima ugenini.

Mzize kwenye mchezo huo alihusika kwenye mabao matatu anafikisha mabao 13 ndani ya ligi akiwa kinara kwenye eneo la wakali wenye mabao mengi anafuatiwa na Prince Dube mwenye mabao 12.

Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema kuwa kabla ya mchezo alizungumza na Mzize ambaye alikuwa na maumivu ambapo kulikuwa na hatihati asicheze mchezo huo.

“Wengi hawajui kwamba kulikuwa na hatihati Mzize asicheze mchezo dhidi ya Fountain Gate alikuwa na maumivu, niliongea naye kuhusu umuhimu wa mchezo na kile ambacho tunafikiria kwa sasa katika mbio za ubingwa.

“Hatimaye alinielewa na unaona kwenye mchezo alicheza vizuri na kufunga kisha akachaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo, huwa ninazungumza na wachezaji kwa kuwa ninajua mpira kwa kiasi chake.”

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM. Kuna kazi mpya inaandaliwa inaitwa Moyo Wangu Unavuja Damu usipange kukosa.