Dar es Salaam. Watoto wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala iliyopo Dar es Salaam wamepokea msaada wa vyakula kutoka Shule ya Green Acres iliyopo mkoani hapa.
Shule hiyo imetoa msaada kwa watoto hao ikiwa ni sehemu ya maadhimisho yao ya kutimiza miaka 25 tangu kuanzishwa kwake na kusherehekea mafanikio yao katika kipindi hicho. Pia, shule imetumia njia hiyo kuwafundisha wanafunzi wao uwajibikaji kwa jamii.
Akizungumza na Mwananchi leo Mei 10, 2025, mkurugenzi wa shule hiyo, Jackyline Rushaigo amesema maadhimisho hayo yaliyodhaminiwa na Benki ya CRDB, yameambatana na tukio la kijamii lenye lengo la kuwafundisha wanafunzi wao huruma, upendo na uwajibikaji kwa jamii.
Amesema wameamua kutumia siku hiyo kutoa sadaka kwa wagonjwa kama njia ya kuwajengea watoto msingi wa utu na kuwafanya watambue umuhimu wa kusaidia wahitaji.

“Tumepeleka msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo maziwa, sukari, maji ya kunywa, biskuti, nguo na taulo za kisasa kwa watoto waliolazwa katika wodi ya watoto.
“Hili ni darasa la maisha kwa wanafunzi wetu ili wajifunze kuguswa na mateso ya wenzao,” amesema Rushaigo.
Ameongeza kuwa shule hiyo iko tayari kuendelea kushirikiana na Hospitali ya Mwananyamala katika kusaidia wagonjwa, hasa watoto, kwa kuwa huduma ya afya ni eneo lenye uhitaji mkubwa unaohitaji msaada wa kijamii.
Naye Katibu wa Afya wa Hospitali ya Mwananyamala, Lilian Mwanga ameipongeza shule ya Green Acres kwa hatua hiyo ya kijamii, akisema imeonyesha mfano mzuri kwa jamii katika kusaidia wahitaji.
“Tunaishukuru sana shule hii kwa moyo wa kutoa na kwa juhudi zao za kuwalea watoto katika maadili mema.
“Kupitia msaada huu, watoto waliolazwa hapa wamepata faraja kubwa, pia, tunawashukuru washirika wao Benki ya CRDB kwa kushiriki nasi siku ya leo,” amesema.
Mwanga amesisitiza kuwa hospitali hiyo bado ina uhitaji wa misaada ya aina mbalimbali na kutoa wito kwa wadau wengine waendelee kujitokeza kutoa misaada hospitalini hapo kwa wahitaji.
Ameongeza kuwa tukio hilo limeacha alama ya matumaini na tabasamu kwa watoto wagonjwa huku likiimarisha mshikamano kati ya sekta ya elimu na afya katika kujenga jamii yenye huruma.