Kesi ya Boni Yai, yaendelea kupigwa kalenda

Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya kusambaza taarifa za uongo inayomkabili meya wa zamani wa Kinondoni na Ubungo, Boniface Jacob, haujakamilika.

Wakili wa Serikali, Erick Kamala ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Mei 12, 2025 wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Jacob ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, anakabiliwa na mashitaka mawili ya kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wake wa X.

Kesi hiyo ilipangwa leo kwa ajili ya kutajwa na kuangaliwa iwapo upande wa mashitaka umekamilisha upelelezi au laa, lakini wakili Kamala ameieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Wakili Kamala ametoa maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga, anayesikiliza shauri hilo.

Hakimu Kiswaga baada ya kusikiliza maelezo hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 5, 2025 kwa kutajwa na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Boni Yai anakabiliwa na mashitaka mawili ya kuchapisha taarifa za uongo katika mfumo wa kompyuta katika akaunti ya X yenye jina la Boniface Jacob @Ex MayorUbungo kwa nia ya kupotosha umma kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandano namba 14 ya mwaka 2015.

Related Posts