Mwili wa Hayati Msuya wapokewa Kilimanjaro, kuzikwa kesho

Moshi. Mwili wa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya umewasili asubuhi ya leo Jumatatu, Mei 12, 2025 katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) na kupokewa na viongozi wa mbalimbali wa Serikali.

Msuya ambaye alizaliwa mwaka 1931 katika Kijiji cha Chomvu, Usangi, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro alifariki dunia Mei 7, 2025 kwa ugonjwa wa moyo wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam na anatarajiwa kuzikwa kesho Mei 13, 2025.

Mwili huo ambao umebebwa na ndege ya Shirika la Air Tanzania umetua katika uwanja huo wa ndege saa 8:20 asubuhi ambapo baada ya kushushwa kwenye ndege umebebwa na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuingizwa kwenye gari maalumu la jeshi.

Baada ya kupokewa jeneza lenye mwili huo na viongozi hao wa Serikali wakiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, (Bunge na uratibu), William Lukuvi, msafara utaelekea Wilaya ya Mwanga katika viwanja vya CD Msuya, ambapo wananchi watapata fursa ya kuaga.

Baadaye mwili huo utapelekwa katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Kilaweni Usangi kijijini kwake ambapo pia wananchi wa maeneo hayo watapata fursa ya kuaga na kisha utapelekwa nyumbani kwake kwa ajili ya taratibu za maziko.

Related Posts