Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Yahya Semamba amekitaka Chama cha Watoa Huduma Sekta ya Madini (Tamisa) kuwa na makali ili kiweze kuwadhibiti wanachama wake wanaoleta janjajanja katika utoaji huduma.
Amesema kufanya hivyo kutawasaidia wao kuaminika na kupewa kazi na wamiliki wa migodi, kwani watakuwa wakiwaamini, hali itakayoongeza ushiriki wa wazawa katika sekta ya madini.
Ametoa kauli hiyo wakati akizindua Kamati ya Masoko na Mawasiliano ya Tamisa iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Yahya amesema Serikali inazo taarifa za baadhi ya watoa huduma katika sekta ya madini ambao si waaminifu na wamekuwa wakileta ujanja na kusambaza bidhaa ambao hazina ubora.
“Sekta ya madini inahitaji mtaji mkubwa, mtu anapokuwa ameweka pesa zake halafu wewe unaenda kuleta ujanja ujanja wako kwenye kazi yake, kama Serikali hatutakuvumilia,” amesema.
Ametoa ushauri kuwa waifanye Tamisa kuwa na makali kama ilivyo Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) ambayo imekuwa ikiwashughulikia wanachama wake wanaoharibu kazi.
“Kuweni kama ERB, mhandisi akicheza ERB wanamuwajibisha, jitahidini muwe na mfumo huu, mkifanikiwa hili mtakuwa na watoa huduma wenye nidhamu wasiowaangusha. Ili hili lifanyike ni kuwa na ushirikiano na sisi kama wizara tutawapa kwa asilimia 100,” amesema Yahya.
Amesema ni vyema pia wahakikishe wanakuwa na wanachama hai ambao watapatikana kwa kuhakikisha wote wanafuata taratibu zinazotakiwa kabla ya mtu kusajiliwa.
“Kiwe chama chenye wanachama hai ambao wanajitambua ambao wakiingia katika ofisi ya Serikali kwenda kuongea kuhusu masilahi ya eneo hili unaona kuwa wanajua wanajua wanachojifanya,” amesema.
Mwenyekiti wa Tamisa, Peter Kumalila amesema azma zao kuu ni kusaidia wanachama kukuza biashara kuwajengea uwezo ili washindane katika sekta.
Hiyo inaenda sambamba na kutetea haki za wanachama pale panapotakiwa.
Hata hivyo, Kumalila amesema mara zote watahakikisha wanafanya mchujo wa kina ili wanachama waaminike na waepuke kuharibu kazi wanazopata migodini.
Hiyo ni kutokana na kuwapo kwa malalamiko kutoka kwa wadau juu ya baadhi ya wazawa wanaopewa kazi na kuzembea au kufanya kazi kwa viwango visivyokubalika.
Ametumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kushughulikia changamoto ya wimbi la wageni kupewa kazi ambazo wazawa wanaweza kuzifanya.
“Tunaomba Serikali iingilie kati kuhakikisha haki inatendeka na tunashauri suala la ubia lizingatie sheria na kanuni na ushiriki wa wazawa,” amesema Kumalila.
Mwenyekiti wa kamati ya masoko na mawasiliano iliyozinduliwa, Dk Sebastian Ndege amesema kwa sasa Tanzania ina madini aina mbalimbali na kampuni zimekuwa zikiwekeza, hivyo ni wakati wa Watanzania kuimarisha ushiriki wao katika uchumi wa madini.
Amesema wanafahamu kuwa wanayo haki ya kushiriki katika kutoa huduma lakini pia wanao wajibu wa kuhakikisha wanatoa huduma sahihi kwa wakati sahihi na weledi.
Kwa upande wake, Kamishna wa Madini, Dk Theresia Numbi amesema usimamizi na utekelezaji wa ushirikishwaji wa Watanzania umeibua ongezeko na fursa katika mafunzo, ajira, uhaulishaji wa teknolojia na ununuzi wa bidhaa zinazozalishwa nchini.