Musoma. Ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu na kushughulikia changamoto za wananchi, ikiwemo migogoro ya ardhi, wakuu wa wilaya za Tarime na Musoma mkoani Mara wamekabidhiwa magari mapya yenye thamani ya zaidi ya Sh504 milioni.
Wakuu wa wilaya hao, Juma Chikoka wa Tarime na Meja Edward Gowele wa Musoma, sasa hawatalazimika tena kuazima magari kutoka idara nyingine ili kuwafikia wananchi, baada ya kukabidhiwa vyombo hivyo vya usafiri.
Wakati wa makabidhiano, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amewataka madereva kuwa waangalifu barabarani ili kuepuka ajali na kulinda usalama wa magari hayo.
Akikabidhi magari hayo leo, Mei 22, 2025, Kanali Mtambi amesema hatua hiyo ni sehemu ya kuboresha mazingira ya kazi kwa wakuu wa wilaya.
Kanali Mtambi amesema kabla ya kukabidhiwa magari hayo, viongozi hao walilazimika kuazima magari kutoka taasisi na idara nyingine za Serikali, hali ambayo huenda ilikuwa kikwazo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
“Niwahimize wakuu wote wa wilaya kuhakikisha mnafika katika maeneo yote ya wilaya zenu, hususan vijijini ili kusikiliza na kutatua kero za wananchi bila visingizio vyovyote.
“Magari haya mliyokabidhiwa yanamaliza rasmi changamoto ya ukosefu wa usafiri iliyokuwa ikiathiri utendaji wa wakuu wa wilaya katika mkoa huu,” amesema Kanali Mtambi.
Kufuatia hilo, amewataka wakuu wa wilaya kuanzisha kliniki za kusikiliza na kutatua migogoro mbalimbali katika jamii, hususan ya ardhi, pamoja na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.
Amesema baada ya wakuu wa wilaya sasa Serikali inajipanga kununua magari kwa ajili ya makatibu tawala wa wilaya.
“Tunaahidi kusimamia na kutekeleza maagizo na maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa ili kuleta tija kwa wananchi,” amesema Chikoka.
Kwa upande wake Meja Gowele amesema magari hayo yatawawezesha kufika katika maeneo yao ya utawala na kutekeleza majukumu yao kwa maslahi ya wananchi.
“Tunaamini kasi ya utendaji kazi itazidi kuongezeka Serikali imeleta fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo sasa ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi hiyo utafanyika kwa uzalendo na uaminifu mkubwa ili miradi ilete tija iliyokusudiwa,” amesema Meja Gowele.