Washington. Baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kumbana Rais Cyril Ramaphosa kuhusiana na tuhuma za kuwepo vitendo vya unyanyasaji na mauaji ya wakulima weupe (Afrikaners) nchini Afrika Kusini, kiongozi wa Chama cha Economic Freedom Fighters (EFF), Julius Malema amewakosoa viongozi hao.
Jana, Rais Trump katika mazungumzo na Rais Ramaphosa katika Ofisi ya Oval iliyoko Ikulu ya Marekani ambapo miongoni mwa hoja zilizoibuka ni uwepo wa mauaji ya Afrikaners madai ambayo mgeni wake (Ramaphosa) aliyakanusha.
Hata hivyo, video ambazo Trump alizitumia kama vielelezo na ushahidi wa uwepo wa matukio ya chuki, unyanyasaji na mauaji dhidi ya Afrikaners hao ni za Malema ambapo alisikika akisema, ‘Kill the boers’ akimaanisha ‘makaburu wauawe’.
Baada ya mazungumzo hayo ya Trump na Ramaphosa kusambaa mitandaoni, Malema ameibuka na kusema kuwa kundi la wazee (akimaanisha Rais Trump na Ramaphosa) wamekutana Ikulu ya Washington nchini Marekani kupiga umbea kuhusu yeye.
Malema ameenda mbali na kudai kuwa hakuna ushahidi wa uhakika ambao Trump ameutoa kuthibitisha kuwa Wazungu wanabaguliwa ama kunyanyaswa nchini Afrika Kusini.
Malema amesema hawawezi kukubali kuona ardhi ya Afrika Kusini ikiporwa na Wazungu bila malipo wala fidia yoyote kwa faida za kisiasa zinazowanufaisha wachache.
Jana Rais wa Marekani, Donald Trump, alimuuliza Rais Ramaphosa kuwa kama Serikali yake haiungi mkono ubaguzi na mauaji ya Wazungu nchini Afrika Kusini, kwa nini hadi leo hawajamkamata Julius Malema ambaye alitangaza hadharani mbele ya umati wa watu kuwa Wazungu wanapaswa kuuawa na kupokonywa ardhi zao.
Pamoja na kuonyeshwa vielelezo vya video, Rais Ramaphosa aliendelea kusisitiza kwamba Serikali yake haiungi mkono mauaji ya watu na kinachoonekana kikisemwa na Malema kwenye video hizo siyo msimamo wa Afrika Kusini.
Trump amehoji; “Kwa nini hamjamkamata yule mwanamume (Malema), amesema ‘Wazungu wauawe, waueni Wazungu’ kisha anacheza huku anarudia kauli yake, sina uhakika lakini nadhani mtu akisema waueni watu fulani, anapaswa kukamatwa haraka, yule alikuwa anaongea kwenye uwanja wenye mamia ya watu na kuna Wazungu wenye mashamba yao tumeona video wameuawa”
Ramaphosa ambaye katika ziara hiyo ameambatana na mawaziri, wafanyabiashara na wachezaji nguli za gofu nchini Afrika Kusini baada ya kauli hiyo akamweleza Trump kuwa matukio ya mauaji yanaweza kutokea nchi yoyote, huku akisema nchini mwake yapo na mengi yanahusisha watu weusi.
“We need to find out (tunapaswa kulifuatilia),” alijibu Ramaphosa kisha kimya cha dakika zaidi ya tatu kikapita marais hao wakitazamana na kunong’oneza watu waliokuwa pembeni yao.
Mshangao zaidi ulimshika Ramaphosa baada ya Trump kuletewa vielelezo vya makala za mauaji zilizochapishwa kwenye magazeti zikionyesha picha za Wazungu waliouawa kwa kushushiwa vipigo na kuchomwa moto.
“Katika baadhi ya nyakati baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani vimekuwa vinafanya mambo ambayo ni kinyume na sera za nchi. Wanazungumza wanayojisikia kwa sababu ni haki inayolindwa kikatiba lakini haimaanishi kuwa huo ndiyo msimamo wa nchi,” amesema Ramaphosa.
“Hata takwimu za matukio ya mauaji nchini Afrika Kusini siyo yanayohusisha Wazungu bali watu weusi,” amesema.
Ramaphosa ameiomba Marekani kumsaidia kupambana na matukio ya uhalifu yakiwemo yanayodaiwa kuhusisha mauaji ya wakulima wa Kizungu nchini Afrika Kusini.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.