Mbeya. Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson ametangaza rasmi nia ya kugombea jimbo jipya la Uyole katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 2025, huku akiwaachia kazi wananchi jijini humo kumchagua mgombea ajaye.
Dk Tulia ametangaza hatua hiyo leo Mei 23, 2025 wakati akizungumza na wananchi mbalimbali wakiwamo makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akiambatana na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro.
Hata hivyo, wakati akitangaza kugombea jimbo hilo, baadhi ya makada na wananchi wameonekana kufurahia wakipiga vigelegele huku wengine wakionesha sura za huzuni na masikitiko.
Dk Tulia ambaye pia ni Spika wa Bunge la Tanzania, amesema pamoja na uamuzi huo kutoa fursa kwa wengine, lakini hatawaacha wananchi wa Mbeya Mjini.

Baadhi ya wananchi wakaimsikiliza Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson wakati akitangaza kugombea Jimbo la Uyole.
Amewaomba wananchi kuwa makini katika kumchagua mgombea wa wananchi akieleza kuwa ipo miradi ya kimkakati inayoendelea, hivyo inahitaji mtu sahihi wa kuendeleza.
“Siyo jambo jepesi kutangaza, ndio maana nimekuja mwenyewe, lakini kwa muda wote mmeniona niko mtu wa namna gani, hii ni kutoa fursa kwa wengine.
“Najua wapo wananyemelea hapa ninapoondoka na wanaokuja ninapoenda kwa kuwa CCM ina mtaji wa watu ila wajipange, niwaombe wananchi wangu, kuweni makini, leteni mtu sahihi kwa kuwa kuna miradi kama Stendi Kuu Sokomatola,” amesema Dk Tulia.