Kupata shahada Sua siyo lelemama, Mbeki atoa ahadi

Morogoro. Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Raphael Chibunda amesema kuwa kupata shahada katika chuo hicho hakujawahi kuwa jambo rahisi na haitawahi kuwa rahisi, kutokana na viwango vya juu vya kitaaluma vinavyodumishwa na chuo hicho.

Mbali na kauli ya Profesa Chibunda, Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, ametembelea eneo la kihistoria la Mazimbu, ambalo kwa sasa ni sehemu ya Sua.

Eneo hilo lilikuwa makazi na kituo cha mafunzo kwa wapigania uhuru wa Chama cha African National Congress (ANC), ambacho kiliongozwa na Hayati Nelson Mandela katika harakati za ukombozi wa Afrika Kusini.

Akizungumza katika Mahafali ya 46 ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua) yaliyofanyika jana, ambapo jumla ya wahitimu 794 walitunukiwa shahada mbalimbali na Mkuu wa Chuo, Jaji Mstaafu Joseph Warioba, Profesa Raphael Chibunda alibainisha kuwa chuo hicho kwa sasa kinatekeleza jumla ya miradi tisa ya utafiti yenye thamani ya Sh3.8 bilioni.

Aidha, Profesa Chibunda ameeleza kuwa SUA kinaendelea kutekeleza mradi mkubwa wa maboresho ya miundombinu chini ya Mpango wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), wenye thamani ya Sh58.5 bilioni. Wakandarasi tayari wapo kazini na wanaendelea kwa bidii na utekelezaji wa maboresho hayo.

Kwa upande wao, baadhi ya wahitimu wameeleza kuwa safari ya kupata shahada haikuwa rahisi, wakitaja changamoto mbalimbali walizokutana nazo.

Hata hivyo, wamesema changamoto hizo zililenga kuwajenga kuwa wataalamu mahiri na wenye uwezo mkubwa wa kitaaluma kutoka katika taasisi hiyo ya juu ya elimu.

Mmoja wa wahitimu, Robert Komba, amesema kuwa moja ya changamoto kubwa zinazowakabili wanafunzi katika kupata shahada chuoni Sua ni umakini mkubwa wa walimu pamoja na vigezo madhubuti vinavyotumika katika mchakato wa udahili wa wanafunzi.

“Ukichagua kusoma Sua, lazima ujiandae kikamilifu. Hakuna shahada za ‘nyepesi nyepesi’ hapa, hakuna nafasi ya mzaha, wala shahada za huruma. Chuo hiki, mbali na kuwa taasisi ya elimu ya juu, ni kiwanda cha kutengeneza wataalamu wa kweli katika taaluma mbalimbali,” amesema Komba kwa msisitizo.

Kwa upande wake, Fatma Mbaruku Mahmoud, mhitimu kutoka Zanzibar, amesema alichagua kusoma Sua kutokana na mazingira bora ya kujifunzia pamoja na programu za masomo zinazolenga kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujiajiri badala ya kutegemea ajira.

“Nimehitimu shahada ya awali katika masomo ya bustani (horticulture), na mpango wangu ni kujiajiri kwa kufanya kilimo cha mboga mboga. Zanzibar kuna fursa kubwa katika sekta ya bustani, hasa kwa mazao ya mbogamboga, na mimi nimejiandaa kutumia vyema fursa hiyo,” amesema Mahmoud.

Wakati huo huo, uongozi wa chuo hicho ulifanya mazungumzo na Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, katika kampasi ndogo ya Solomon Mahlangu ikiwamo kutembelea eneo  la Mazimbu ambalo kwa sasa ni sehemu ya Sua.

Eneo hilo lilikuwa makazi na kituo cha mafunzo kwa wapigania uhuru wa ANC kilichokuwa kinaongozwa na Hayati Nelson Mandela.

Mbeki ametembelea Mazimbu ikiwa ni katika Maadhimisho ya Siku ya Afrika ambayo huadhimishwa kila mwaka Mei 25.

Katika ziara hiyo, Mbeki ametembelea makaburi ya wapigania uhuru waliokufa na kuzikwa katika eneo hilo, ambapo pia ameweka shada la maua na kupanda mti wa kumbukumbu.

Aidha, ametembelea hospitali ya Sua iliyokuwa ikiwahudumia wanachama wa ANC waliokuwepo katika eneo la Mazimbu, na kuzungumza na uongozi wa chuo hicho ulioongozwa na Mkuu wa Chuo, Mzee Joseph Warioba.

Mbeki ameahidi kuwa taasisi yake, kwa kushirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, itaandaa makala maalum ya picha za mwendo katika eneo hilo, kwa lengo la kuhifadhi na kueneza historia ya eneo hilo kwa wananchi wa Afrika Kusini, ili waweze kujua na kuthamini mchango wa Tanzania kwa nchi yao.

“Mazimbu ni nyumbani kwetu; eneo hili si sehemu tu ya historia ya Afrika Kusini, bali ni alama ya mshikamano wa kweli wa Afrika.

“Tanzania ilikuwa nasi wakati wa giza kuu la ukandamizaji. Leo tuko huru kwa sababu mlitupokea, mkatufundisha, na mkatupa hifadhi,” alisema Mbeki.

Taasisi ya Thabo Mbeki kwa kushirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere wameandaa maadhimisho ya Siku ya Afrika mwaka 2025, ambapo Mhadhara wa 15 wa Taasisi ya Thabo Mbeki utafanyika jijini Dar es Salaam kesho Mei 24 Mei, ili kuadhimisha siku hii muhimu ya Afrika nchini Tanzania.

Related Posts