Arusha. Halmashauri ya Jiji la Arusha imefanikiwa kuongeza makusanyo yake hadi kufikia Sh51 bilioni kwa mwaka 2024/2025 kutoka Sh21 bilioni zilizokusanywa msimu wa mwaka 2020/2021 wakati wakiingia madarakani.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa jiji, Mei 22, 2025, Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iranghe amesema siri ya mafanikio hayo ni ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato na kuboresha zilizokuwepo.
Katika mkutano huo wenye lengo la kutoa taarifa ya utekelezaji wa miradi kwa miaka minne waliyokaa madarakani, meya huyo amesema moja ya maboresho ni kutoa mitaji ya biashara kwa vikundi 862 vikiwemo 624 vya wanawake, 58 walemavu na vijana.
“Jumla ya mikopo tuliyotoa kwa vikundi hivyo ni zaidi ya Sh10.3 bilioni kwa ajili ya kuwawezesha kufanya biashara na wengine kukuza mitaji yao ili waweze kulipa kodi kupitia vizimba na leseni,” amesema.
Amesema kwa miaka minne wamefanikiwa kupokea Sh400 bilioni na kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo kuongeza shule za msingi nne kutoka 47 hadi 51 na shule za sekondari sita kutoka 26 hadi 32.
“Pia, tumejenga barabara za lami zenye urefu wa kilomita 20 na kuweka taa za barabarani na kamera, lakini pia ujenzi wa hospitali ya wilaya na zahanati sambamba na kununua vifaa tiba vya kisasa katika kituo cha afya Kaloleni,” amesema.
Mbali na hilo, amesema wanatarajia kuvunja baraza hilo la madiwani rasmi Juni 28, 2025 wakijivunia kuacha utekelezaji wa miradi mikubwa yenye kuongezea zaidi uwezo wa halmashauri hiyo kupaisha makusanyo yake.
“Sisi tunavunja baraza hili mwezi ujao, kuna watakaorudi na wengine watapumzika lakini tunajivunia kutengeneza njia nzuri ya kusisimua ongezeko la mapato ya jiji letu ikiwemo kuongeza vituo vya ukusanyaji, kuongeza mitaji ya wafanyabiashara, pia, kuboresha masoko yetu ya mkakati,” amesema.
Akitaja miradi mkubwa ambayo itafanikisha uongezaji wa mapato kwa jiji hilo, Maximilian amesema kuwa ni ujenzi wa soko la kisasa Kwa Mrombo na Kilombero, maboresho ya maduka ya stendi ndogo na uwanja wa mpira wa mazoezi wa jiji na ukumbi wa mikutano.
“Kwa mfano, maboresho ya maduka ya stendi ndogo pekee kwa sasa inaingiza wafanyabiashara 400 pekee na mapato ya Sh1.2 bilioni kwa mwaka, lakini maboresho yakikamilika yatawezesha wafanyabiashara 2,000 kufanya kazi pale na kuingiza zaidi ya Sh6.0 bilioni kwa mwaka,” amesema.
Wakati meya huyo akitaja mafanikio hayo, kumekuwa na maandamano na migomo ya mara kwa mara ya wananchi huku wakiandamana na wakifunga barabara wakilalamikia ubovu wa barabara za ndani.
Hayo yanatokea ikiwa ni miezi miwili tangu jiji hilo kununua mitambo yenye thamani ya Sh1.7 bilioni ya kutengeneza barabara sambamba na kutoa kiasi cha Sh4 milioni kwa kila kata kwa ajili ya kuboresha barabara za ndani ya mitaa na ubalozi.
Hata hivyo, sehemu kubwa za barabara hizo bado hazijaanza kufanyiwa kazi licha ya kupita miezi miwili, wananchi hao wanadai hawaoni mafanikio yoyote.
“Ni kweli tuliona mitambo na habari za vifusi lakini tunaamua kuandamana na kufunga barabara kushinikiza mabadiliko kwani hatuoni ukarabati wowote zaidi ya sisi kuteseka na kuhangaika na usafiri,” amesema Rehema Mbise, mkazi wa Kata ya Sokoni.
Naye Amina Ramadhani, mkazi wa Muriet amelipongeza Jiji la Arusha kwa kuamua kuboresha soko la Mrombo ambalo limekuwa maarufu kwa uchomaji wa nyama ya mbuzi.
“Hii kweli ina uwezo wa kuongeza mapato na sisi tutanufaika na maboresho hayo, kikubwa isiwe ahadi za matumaini bali utekelezaji ufanyike tuone matunda hayo,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude amewataka viongozi wa kata kufuata ngazi za mawasilisho ikiwemo kuwa na vikao vya mara kwa mara na wananchi wao kujua kero zao na kutafuta ufumbuzi wa mapema.
“Tusisubiri hadi waandamane, tuanze kukimbizana, itisheni mikutano na vikao vya mara kwa mara kujua kero, ili itafutiwe ufumbuzi. Mfano kero ya barabara, waambieni mvua ndio tatizo, imeharibu barabara na tunasubiri ikiisha miradi mikubwa iendelee lakini pia ukarabati ufanyike maeneo korofi zaidi kwa kumwaga vifusi,” amesema.