Unguja. Wakati mchakato wa kuandaa mtaala mpya wa umahiri ukiendelea, wataalamu wa elimu wamesema mtaala huo unatarajiwa kufungua fursa mpya kwa vijana kwa kuwa utawawezesha kujengwa kwa kizazi chenye uwezo wa kubuni, kutekeleza na kuendeleza shughuli za kiuchumi kwa kutumia stadi mbalimbali watakazojifunza shuleni.
Katika hatua ya awali, mtaala huu umeweka msingi muhimu kwa kuanzisha somo la sanaa za ubunifu na michezo kuanzia elimu ya awali (chekechea) hadi ngazi ya elimu ya msingi, kwa lengo la kukuza vipaji, kuendeleza ubunifu na kuimarisha ustadi wa watoto tangu wakiwa katika umri mdogo.
Akijibu swali barazani leo Mei 23, 2025, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Abdugulam Hussein, amesema katika elimu ya sekondari, mtaala umeweka mkazo katika masomo ya mkondo wa amali kama vile ufundi selemala, kutengeneza programu za kompyuta, kuunganisha umeme majumbani, grafiki na utengenezaji mabomba.
Hussein amesema masomo hayo yanamwezesha kijana kupata ujuzi wa moja kwa moja unaomwezesha kuingia kwenye soko la ajira au kuanzisha shughuli binafsi.
Abdugulam alikuwa akijibu swali la Mwakilishi wa Mwanakwerekwe, Ameir Abdalla Ameir, aliyetaka kujua kwa kiasi gani mtaala huo utakuwa mkombozi wa changamoto kwa vijana.
“Mtaala mpya wa umahiri umeandaliwa mahususi kwa lengo la kuhakikisha kuwa wahitimu wa elimu ya maandalizi, msingi na sekondari wanapata ujuzi wa msingi na wa kati unaowasaidia kujiari au kuajiriwa, hivyo kuwa na uwezo wa kujitegemea kimaisha,” amesema.
Amesema katika hatua ya awali, mtaala huo umeweka msingi kwa kuanzisha somo la sanaa za ubunifu na michezo kuanzia elimu ya maandalizi hadi ngazi ya msingi, kwa lengo la kukuza vipaji na ubunifu wa watoto tangu wakiwa wadogo.
“Hili ni jambo la msingi kwa kuwa maendeleo ya stadi na ubunifu huanza kujengwa mapema,” amesema.
Amesema ili kuhakikisha utekelezaji mzuri wa mtaala huu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imewajengea pia uwezo walimu kwa kuwapatia mafunzo ya kitaalamu juu ya namna bora ya kufundisha kwa kutumia mtaala huu mpya.
“Mafunzo haya yamelenga kuongeza ufanisi na kuhakikisha kuwa maudhui ya umahiri yanafikiwa kwa kiwango kilichokusudiwa,” amesema.
Pia, Serikali imekuwa ikiendelea kusambaza vitabu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika skuli mbalimbali Unguja na Pemba ili kuwezesha mazingira bora ya ujifunzaji wa stadi hizo kwa vitendo.