PDPC kuendesha mafunzo maalumu kukabili udukuzi mitandaoni

Dodoma. Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imetangaza mpango maalum wa mafunzo kwa maofisa wa ulinzi wa taarifa binafsi kutoka taasisi za umma na binafsi nchini, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na changamoto za udukuzi wa akaunti na matumizi mabaya ya taarifa za watu.

Mpango huu umekuja siku chache baada ya baadhi ya akaunti za Serikali kuripotiwa kudukuliwa, jambo ambalo limezua hofu juu ya usalama wa taarifa mtandaoni.

Akizungumza Mei 22, 2025, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Stephen Wangwe, alisema mafunzo hayo yatalenga kuwajengea uwezo watendaji wanaosimamia usalama wa taarifa na mitandao, ili kuimarisha viwango vya ulinzi wa taarifa binafsi kulingana na matakwa ya sheria.

“Tunaingia katika zama mpya za kuhakikisha faragha na usalama wa taarifa za watu zinalindwa. Heshima ya mtu ipo kwenye namna taarifa zake zinavyohifadhiwa na kutumika,” alisema Wangwe.

Alibainisha kuwa mafunzo hayo yatatolewa kwa mfumo wa makundi ya washiriki 400 kila moja, na yatajikita katika mafunzo ya kina kuhusu usimamizi wa taarifa binafsi na namna ya kukabiliana na uhalifu wa kimtandao, hasa suala la impersonation ambapo wahalifu hujifanya watu wengine kwa nia ya kudhuru au kuchafua sifa.

“Wale wanaosimamia akaunti za taasisi ni lazima wawe na uelewa wa msingi kuhusu ulinzi wa taarifa. Mafunzo haya yatawapa mbinu za kuepusha kuingiliwa kwa akaunti na madhara yake,” aliongeza.

Meta kuwafikia Facebook, Instagram, na WhatsApp

Pia, Wangwe alisema taasisi ya Meta, inayosimamia mitandao ya Facebook, Instagram, na WhatsApp, imepanga kufanya mafunzo maalum nchini kwa wasanii na watayarishaji wa maudhui. Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wa kutumia majukwaa hayo kwa usalama, tija na manufaa ya kiuchumi.

“Meta wameshafanya mazungumzo na Serikali. Mafunzo haya yatalenga si tu ulinzi wa taarifa, bali pia namna ya kunufaika kimapato kupitia matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii,” alisema Wangwe.

Mmoja wa watumiaji wa mitandao, Joyce Calista, amesema wananchi wengi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi, hivyo elimu hiyo ni ya msingi.

“Ni muhimu kuwa na vipindi maalumu vya elimu kwa umma ili kuwasaidia Watanzania kujua namna ya kulinda taarifa zao na kuepuka matumizi mabaya,” amesema.

Tangu kuanzishwa kwa PDPC, jumla ya taasisi 9,145 zimekamilisha usajili wa kulinda taarifa, huku zaidi ya 2,000 zikiwa katika hatua mbalimbali za usajili.

Related Posts