Dar es Salaam. Wakati migodi mingi nchini ikihamia kwenye uchimbaji wa chini ya ardhi, inaelezwa kuwa hatua hiyo imesababisha uhitaji wa wataalamu, huku uhitaji wa wataalamu hao (mafundi mchundo) wa kuendesha mitambo migodini ukiwa mkubwa.
Awali, uhaba huo ulikuwepo katika eneo la ufundi umeme wa viwandani, ufundi wa mitambo mikubwa ya migodini, umeme wa magari ya migodini, uungaji vyuma vizito na ufundi wa mitambo na ufitishaji.
Akizungumzia changamoto hiyo leo Mei 23, 2025, Katibu Mtendaji wa Chemba ya Madini (TCM), Benjamin Mchwampaka amesema uhaba ulipungua baada ya chemba hiyo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) kuanzisha kozi maalumu iliyoanza mwaka 2009.
Amesema uhaba wa wataalamu hao umerejea tena hivi sasa kutokana na migodi mingi kuhamia kwenye uchimbaji wa chini ya ardhi, hali iliyosababisha mahitaji ya kitaalamu kuongezeka.
Amesema uchimbaji wa chini ya ardhi unahitaji mitambo maalumu, ambayo migodi mingi kwa sasa inatumia wataalamu kutoka nje kuiendesha kutokana na Watanzania wengi kutokuwa na utaalamu huo.
Amesema ili kuziba pengo hilo, TCM kwa kushirikiana na Veta Moshi wameandaa kozi sita kwa ajili ya kuingizwa kwenye mtaala ili kumaliza changamoto hiyo na kutoa fursa za ajira kwa vijana wa Kitanzania.
Amesema kwa sasa wapo katika hatua ya mwisho ya kwenye vyombo vya kuthibitisha ili kozi hizo zipelekwe Nactvet kwa ajili ya kupata ithibati tayari kuanza.
“Tunaamini mchakato huo utaharakishwa ili kuanza kwa kozi hii, ambayo ni ya miaka mitatu, na kijana yeyote wa Kitanzania anayefundishika, mwenye umri wa kuajirika, anayeweza kusoma na kupata ajira ambazo sasa zinafanywa na wageni wengi,” amesema.
Miongoni mwa kozi hizo ni uendeshaji wa mitambo ya Jumbo na Solo, uendeshaji wa Bogger na Cubex, utengenezaji na kuchaji baruti mashimoni na kuinua (Lifting and Rigging).
“Kozi hizi zitaandaa vijana wa Kitanzania kuchukua nafasi zinazoshikiliwa na wataalamu kutoka nje na kusaidia kutekeleza Sera ya Ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini.
“TCM inaunga mkono juhudi za Serikali za kuongeza ushiriki wa Watanzania kwenye mnyororo wa thamani kwa kuwaandaa wahitimu kwa ujuzi unaohitajika sokoni ili kupanua fursa za ajira na kuchangia katika maendeleo jumuishi ya uchumi wa Taifa,” amesema.
Akielezea Mpango wa Mafunzo ya Ufundi kwa Sekta ya Madini (IMTT), ambao unalenga kuwapa vijana wa Kitanzania ujuzi unaohitajika katika migodi, amesema ulianzishwa mwaka 2009, ukilenga kukabiliana na uhaba wa mafundi mchundo waliobobea katika sekta ya madini.
Kabla ya mpango huo, kulikuwa na uhaba wa mafundi mchundo, hali iliyosababisha migodi kuajiri wataalamu kutoka nje ya nchi kama Ghana, Mali na Afrika Kusini.
“TCM ilitenga Dola milioni 2 za Marekani ili kuanzisha mpango huu kwa kushirikiana na Veta Moshi ambako kulikuwa na miundombinu.
“Kupitia IMTT, zaidi ya vijana 1,500 wanaume 1,333 na wanawake 167, wamehitimu hadi kufikia Januari mwaka huu,” amesema.
Amesema wahitimu hao ni katika maeneo matano ya msingi ambayo ni ufundi umeme wa viwandani, ufundi wa mitambo mikubwa ya migodini, umeme wa magari ya migodini, uungaji vyuma vizito na ufundi wa mitambo na ufitishaji.
“Hii ilisaidia kupunguza uhaba na vijana wa Kitanzania takribani asilimia 70 walipata ajira migodini, na waliosalia walipata ajira kwenye sekta nyingine.
“Hata hivyo, baada ya migodi mingi kuhamia kwenye uchimbaji wa chini ya ardhi, uhaba wa wataalamu umerejea kutokana na mitambo inayotumika kwenye uchimbaji huo,” amesema.