Wawakilishi walalama wananchi kutolipwa fidia wakipisha miradi

Unguja. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamesisitiza kuwa licha ya umuhimu wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa, ni lazima wananchi wanaoathiriwa na ujenzi wa miundombinu hiyo walipwe fidia zao kwa wakati.

Wameeleza jinsi athari za miradi hiyo zinavyosababisha maumivu na malalamiko miongoni mwa wenyeji.

Pia, wametaka kuangalia vipaumbele vya barabara zinazotengenezwa kwani yapo maeneo ambayo yanajengwa barabara, lakini ukiyaangalia, yanayoachwa ndiyo yenye uhitaji mkubwa kwa uchumi wa Zanzibar, hususani Pemba.

Hata hivyo, Serikali imesema hakuna mwananchi hata mmoja atakayeshindwa kulipwa fidia baada ya kupisha miradi, ila fidia zingine zinachelewa baada ya wahusika kukataa malipo wakidai ni madogo.

Hayo yamejiri leo Mei 23, 2025, wakati wawakilishi hao wakijadili na kupitisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi.

Wizara hiyo imepitishiwa Sh1.5 trilioni kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele ambavyo vimejikita kwenye miundombinu ya ujenzi, usafirishaji na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Akichangia bajeti hiyo, Mwakilishi wa Wingwi, Kombo Mwinyi Shehe (ACT-Wazalendo) amesema katika maeneo mengi ambayo zimejengwa barabara na uwanja wa ndege Pemba, watu hawajalipwa fidia zao, huku akisema zipo nyumba ambazo zimeanguka na kuingiliwa na maji kwa sababu walishindwa kuziendeleza baada ya kufanyiwa tathmini.

“Tunapojenga barabara na kuhitisha miradi mingine, wale wananchi wanaokumbwa na kadhia hiyo walipwe ili wajiendeleze. Lakini Mheshimiwa Spika, kuna wananchi wamepisha barabara hawajalipwa fidia zao, hili halileti taswira nzuri,” amesema.

Amesema katika uwanja wa ndege Pemba, kwa taarifa alizonazo, kuna kaya 37 hazijalipwa fidia zao.

“Tunaomba waziri lisimamie hili, watu walipwe fidia zao. Tumepitisha miradi, walipwe badala ya kuwaachia maumivu wananchi hawa. Watu ni masikini, ukimvunjia nyumba bila kumlipa, hawana uwezo wa kujenga,” amesema.

Mwakilishi huyo pia amezungumzia kuhusu vipaumbele vya barabara akisema licha ya Serikali kudai inaifungua Pemba, lakini barabara zake muhimu kutoka Mkoani hadi Chake Chake na Chake Chake hadi Wete zimechakaa; zina mashimo ambayo yanaathiri usafirishaji.

“Hizi ndiyo barabara zinazosafirisha mizigo. Hata hayo makontena mnayoleta, bila hizi barabara, yatasafirishwa kupitia wapi? Inashangaza kuona mnaanza kutengeneza barabara za ndani lakini mnaziacha hizi zenye tija katika uchumi wa Pemba, na ndiyo barabara kuu,” amesema.

Mwakilishi mwingine wa Pandani, Profesa Omar Fakih Hamad (ACT-Wazalendo), amesema taarifa alizonazo ni kwamba kuna wananchi takriban 39 ambao hawajalipwa fidia zao baada ya kupisha ujenzi wa uwanja wa ndege Pemba.

“Inawezekana hawajapata uwezo wa kuifikia wizara lakini wanatufikia sisi huku. Kwenye taarifa iliwahi kutolewa hapa barazani kwamba wapo ‘pending’. Sasa tunataka kujua lini watalipwa na kuendeleza maisha yao katika maeneo mengine. Na tukumbuke si vyema kuingiza siasa katika maisha ya watu,” amesema.

Mwakilishi wa Wawi, Bakari Hamad Bakari (CCM), amesema ulipaji wa fidia kwa wananchi umekuwa na changamoto kubwa.

Amesema katika hotuba ya wizara imesema imelipa fidia wananchi 970, lakini haijataja hao waliolipwa ni kati ya wananchi wangapi waliotakiwa kulipwa fidia.

“Kumekuwapo na ripoti nyingi za fidia zinazotofautiana. Ukisikiliza huku wanaeleza mengine, humu barazani tunaelezwa mengine. Lakini kiuhalisia, wananchi wengi hawalipwi fidia zao. Sasa tunaomba waziri tupate ufafanuzi wa jambo hili,” amesema.

Akizungumzia kuhusu uwanja wa ndege wa Pemba, amesema kuna wananchi ambao wapo kwenye buffer zone wote hawajalipwa na wamezuiwa kuendeleza nyumba zao. Ipo kauli kwamba watalipwa mpaka kumaliza mradi huo mwaka 2028.

“Ikizingatiwa kuna athari nyingi zimejitokeza; kuna nyumba takribani 17 zimeanguka na watu hawa hawana sehemu ya kuishi. Ni vyema wizara ikajiridhisha na kufanya tathmini yake ili wananchi wapate haki zao,” amesema.

Akihitimisha hoja hiyo, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Mohamed, amesema hakuna mwananchi ambaye hatalipwa fidia zake na tayari zimetumika Sh12 bilioni kulipa fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa uwanja wa ndege.

Wakati Kombo akisema kuna wananchi 37 hawajalipwa fidia na Profesa Fakih akisema ana taarifa za wananchi 39, Waziri Khalid amesema bado kuna wananchi 47 ambao hawajalipwa akieleza sababu ni kwamba walikataa malipo kwa madai kuwa ni kidogo.

“Tuliunda kamati ya malalamiko na kurudia tathmini upya chini ya Mkuu wa Wilaya. Kwa hiyo nayo imemaliza kazi, watalipwa fidia zao hivi karibuni,” amesema Dk Khalid.

Tatizo hilo pia amesema lipo kwa wananchi waliopisha miradi ya madaraja ya juu (flyovers) za Mwanakwerekwe na Amani Unguja kwamba fedha ni kidogo. Pia, wizara imechukua hatua za kufanya tathmini upya na kazi hiyo inaendelea.

Pia, Waziri Khalid amekiri wamepokea tatizo la nyumba kuanguka kutokana na kuingiliwa na maji, lakini tayari fedha zao zipo na watalipwa kuanzia wiki ijayo.

Hata hivyo, ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi wazingatie sheria za kutojenga kwenye hifadhi za barabara, akisema kwamba hata wengi waliolipwa fidia imetumika busara ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, lakini ingefuatwa sheria kama ilivyo, wengi wao nyumba zao zipo ndani ya hifadhi.

Kwa upande wa kuwa na vipaumbele vya barabara, Dk Khalid amesema barabara alizozitaja Mwakilishi wa Wawi za Mkoani, Chake Chake na Wete: “Ni kweli kulikuwa na ishu ya technical tayari imetatuliwa na Rais, kwa hiyo ujenzi wake unaanza mara moja.”

Related Posts