Zima waka ya umeme yaibua mjadala barazani, Serikali yaeleza sababu

Unguja. Tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara limeibua mjadala mkali miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wakilitaka Serikali kutoa maelezo ya kina kuhusu chanzo cha changamoto hiyo pamoja na mipango ya dharura ya kuikomesha.

Wajumbe hao wameeleza kuwa hali hiyo si tu inasababisha hasara kwa wananchi kutokana na kuharibika kwa vifaa vyao vya umeme, bali pia inakwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika visiwa hivyo.

Wawakilishi hao wameibua hoja hiyo leo, Mei 23, 2025, wakati wa kipindi cha maswali na majibu kwa Wizara ya Maji, Nishati na Madini, wakieleza kukerwa na tatizo la kukatika kwa umeme ambalo, kwa maelezo yao, limeendelea kuwa sugu katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki, Suleiman Haroub Suleiman, amesema licha ya wizara kudai kuwa tatizo hilo limepungua, hali halisi mitaani ni tofauti, kwani bado linawaathiri wananchi wengi kwa kiwango kikubwa na kuharibu shughuli zao za kiuchumi, hususan biashara ndogondogo.

“Wizara inasema hali imeboreshwa, lakini mitaani wananchi wanaendelea kuteseka. Biashara zinaharibika, vifaa vinaungua, na hali inazidi kuwa kero kwa jamii,” alisema Suleiman.

Ameongeza kuwa baadhi ya nguzo za umeme zimezeeka na hazifai kuendelea kutumika, na akaitaka serikali kutoa maelezo kuhusu mpango wa dharura wa kushughulikia miundombinu hiyo chakavu ili kuondoa tatizo hilo kwa haraka.

Naye Mwakilishi wa nafasi za wanawake, Mwanajuma Kassim Makame, alisema uzimaji wa umeme umekuwa jambo la kawaida kwa wananchi wa Zanzibar, hali inayosababisha kuungua kwa vifaa vyao vya umeme na kuwapa hasara kubwa.

“Ni jambo la kusikitisha kuona wananchi wanaendelea kupata hasara kwa kuunguliwa vifaa vya thamani bila taarifa wala fidia yoyote. Serikali ina mpango gani wa kuwafidia wananchi hawa, ikizingatiwa ni watoa huduma ndio wanaosababisha hasara hizo kwa kukata umeme bila mpangilio?” alihoji.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kiwani, Mussa Foum Mussa, aliitaka Serikali kueleza sababu za msingi za kukatika kwa umeme licha ya kuwepo kwa kiwango cha kutosha cha uzalishaji, akieleza kuwa tatizo hilo limekuwa sugu na linahitaji maelezo ya kina kwa wananchi.

Akijibu hoja hizo, Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Zawadi Amour Hassan, alisema changamoto hiyo inasababishwa na uchakavu wa miundombinu pamoja na mzigo mkubwa unaowekwa kwenye baadhi ya laini kuu za usambazaji umeme katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Ni kweli kumekuwa na changamoto, lakini tayari hatua zimechukuliwa. Baadhi ya laini zilizokuwa zinasababisha kukatika kwa umeme maeneo ya Kusini, Fuoni, Fumba na Mazizini zimefanyiwa marekebisho, na hali imeanza kuimarika,” alisema.

Aidha, alieleza kuwa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) linaendelea kujenga laini mpya katika maeneo mbalimbali ili kuongeza uwiano wa usambazaji wa umeme unaokidhi mahitaji ya sasa.

Pia, Naibu Waziri huyo alibainisha kuwa Zeco inatekeleza mradi mkubwa wa kuboresha miundombinu ya umeme unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, ambao utasaidia kumaliza kabisa tatizo hilo kwa kujenga vituo viwili vikuu vya umeme katika maeneo ya Makunduchi na Matemwe.

“Kupitia vituo hivyo, maeneo ya Kusini na Kaskazini yataweza kujitegemea katika upatikanaji wa umeme badala ya kutegemea kituo kimoja cha Mtoni. Hii itapunguza utegemezi na kukomesha tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara,” alisema Zawadi.

Kuhusu hatua za dharura za kukabiliana na changamoto ya kukatika kwa umeme, Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Zawadi Amour Hassan, amesema wizara ina mpango wa kufunga transfoma mpya katika maeneo yote yenye msongamano wa matumizi ili kuimarisha upatikanaji wa umeme.

Aidha, ameeleza kuwa wizara ipo kwenye hatua ya utekelezaji wa mpango wa kutumia nguzo za zege, ambazo ni imara zaidi na hudumu kwa muda mrefu ikilinganishwa na zile za miti.

Hata hivyo, Naibu Waziri huyo amesema hadi sasa wizara haijapokea taarifa rasmi kutoka kwa wananchi waliounguliwa vifaa vyao kutokana na kukatika kwa umeme.

Amefafanua kuwa iwapo malalamiko hayo yatawasilishwa rasmi, wizara itayapitia na kuangalia njia sahihi ya kushughulikia suala hilo.

“Ni muhimu kuelewa kuwa, wakati mwingine vifaa vya umeme vinaweza kuharibika kwa sababu nyingine zisizohusiana moja kwa moja na kukatika kwa umeme. Kwa hiyo, ni lazima kuwe na tathmini ya kitaalamu ili kubaini chanzo halisi kabla ya kuchukua hatua,” alisema.

Related Posts