Bei lita moja maziwa ya nyuki yagonga Sh12 milioni

Moshi. Wafugaji wa nyuki mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuchangamkia fursa za kiuchumi zitokanazo na mazao ya nyuki ikiwemo maziwa na asali ambapo bei ya lita moja ya maziwa ya nyuki inafikia takribani Sh12 milioni katika soko la kimataifa.

Tanzania inatajwa kuwa nchi ya pili kwa uzalishaji wa asali duniani, ikizalisha takribani tani 38,000 kwa mwaka, ikitanguliwa na Ethiopia ambayo huzalisha tani 50,000 kwa mwaka.

Akizungumza leo Mei 24, 2025 na wafugaji wa nyuki mkoani hapa, Ofisa Mazingira kutoka Shirika la Floresta Tanzania, Judith Makange amesisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya mazao ya nyuki na kutumia mbinu za kisasa katika uzalishaji.

“Maziwa ya nyuki hupatikana kwa njia ya kitaalamu na si rahisi kama ilivyo kwa asali, lakini  bei yake katika soko ni ya juu sana, kwa mfano, lita moja inaweza kuuzwa kwa zaidi ya Sh12 milioni, wateja wakuu ni watu wenye uwezo mkubwa kifedha na wanaotambua faida zake kiafya,” amesema Makange.

Ameongeza kuwa maziwa hayo yamekuwa yakihitajika sana duniani kutokana na faida zake kiafya, ikiwemo kuboresha lishe na kusaidia kuonekana kijana zaidi.

“Kwa mafunzo na mbinu za kitaalamu tulizonazo, tunaweza kuvuna maziwa haya kwa ufanisi zaidi na kuhakikisha yanawafikia walaji kwa ubora unaotakiwa,” amesema Makange.

Makange amesema kuwa upatikanaji wa maziwa ya nyuki bado ni mdogo kutokana na ugumu wa kuyavuna na kwamba inahitaji  kuwa na idadi kubwa ya mizinga ya nyuki kwa ajili ya uzalishaji wake, hivyo ametoa rai kwa wananchi kuchangamkia fursa hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Floresta Tanzania, Richard Mhina amesema tayari wameanzisha vikundi 25 vya ufugaji wa nyuki katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, lengo likiwa ni kuboresha ikolojia na kuwezesha wananchi kujikwamua kiuchumi kupitia mazao yanayopatikana kwa nyuki ikiwemo, maziwa ya nyuki, asali, nta na mengine mengi.

Amesema shirika hilo limetoa mtaji wa mizinga minne kwa kila kikundi pamoja na elimu ya namna bora ya ufugaji wa nyuki na uvunaji wa mazao yake ili kuwezesha wananchi kujiongezea kipato.

Aidha, amesema licha ya kuanza kutoa mtaji wa mizinga katika Wilaya ya Same, tayari wametoa elimu ya ufugaji nyuki katika mkoa mzima wa Kilimanjaro na kuhamasisha wananchi kuchaangamkia fursa hiyo ili kujipatia kipato kutokana na mazao yatokanayo na nyuki.

“Katika ufugaji nyuki, tumeanza na vikundi 25 Wilaya ya Same, ambavyo vina wastani wa watu 25 hadi 32, ambapo tunatoa elimu ya namna bora ya kufuga nyuki na tumekuwa na wataalamu ambao wametusaidia kuhakikisha watu wanapata elimu sahihi kuhusiana na bidhaa ambazo zinatokana na mazao ya nyuki kwani watu wamezoea tu asali lakini katika nyuki kuna zaidi ya asali,” amesema Mhina.

Ameongeza kuwa: “Na ili kuhakikisha hili linakuwa endelevu, tunawapa wananchi elimu ya namna ya kuhakikisha wao wanaendelea kuzalisha mizinga mingine na mazao ya nyuki ili hata tukiondoka kwenye usimamizi na ufuatiliaji, waweze kuendelea na ufugaji huo na kupata mafanikio zaidi kwa kizazi cha sasa na baadaye.”

Related Posts