Unguja. Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi inaendelea na taratibu za uanzishaji wa Chuo cha Uvuvi na Uhifadhi wa bahari ambapo pamoja na mambo mengine kitatoa kozi za kilimo cha bahari na menejimenti ya uchumi wa buluu.
Hayo yamebainishwa leo Jumamosi Mei 24, 2025 barazani wakati Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Shaaban Ali Othman akijibu swali la mwakilishi wa Uzini, Haji Shaaban Waziri alipotaka kujua lini itaanzishwa kozi za uchumi wa buluu ili kuondokana na tatizo la ukosefu wa ujuzi wa matumizi ya rasilimali za sekta hiyo.
“Chuo hiki kinatarajiwa kujengwa Pemba na tayari rasimu ya sheria ya uanzishaji wa chuo hicho imepatikana na iko katika hatua ya kupokea maoni ya wadau mbalimbali,” amesema Waziri Shaaban.
Pamoja na hatua hiyo, amesema Wizara tayari ipo katika hatua za mwisho za upatikanaji wa ardhi pamoja na michoro ya majengo.
Kuhusu ni lini kitakamilika ili kiendane na kasi ya serikali na kwa kuzingatia kuna uhaba wa wataalamu katika fani hiyo, Waziri Shaaban amesema hawezi kusema muda maalumu lakini wanatarajia katika mwaka wa fedha 2025/2026 kitakuwa kimekamilika.
Kuhusu idadi ya wataalamu wanaokosekana katika eneo hilo, Waziri pia amesema hawezi kutaja takwimu kamili lakini ieleweke kwamba kuna uhitaji wa wataalamu hao kwasababu uchumi wa buluu ni mpana.
“Bado kuna uhitaji wa wataalamu, tulifanya tathmini katika maeneo ya uchumi wa buluu, bado kuna uhitaji wa wataalamu kulingana na fani zilizopo na zinazoendelea kuibuka katika sekta hii,” amesema.
Amesema chuo hicho kitakamilika haraka iwapo ikipatikana ardhi kwa ajili ya kujenga majengo yake.
Mwakilishi wa kuteuliwa na Rais, Juma Ali Khatib (Ada Tadea) amehoji, wataalamu wa mafuta na gesi Zanzibar wanapata elimu hiyo wapi na mkakati wa serikali kuwapa mafunzo wataalamu hao.
Waziri Shaaban amesema hakuna chuo kinachotoa kozi zozote za mafuta na gesi Zanzibar, ikizingatiwa jambo hilo ni jipya lakini serikali ipo kwenye tafakuri kuanzisha kozi kwenye vyuo vilivyopo Zanzibar ili kupata wataalamu wanaosoma ndani ya Zanzibar.
Hata hivyo, amesema wataalamu wengi wa eneo hilo husoma nje ya nchi, “Wengi walipo kwenye sekta hii wanasoma nje ya nchi lakini tupo kwenye tafakuri kuingiza kozi kwenye vyuo vyetu vya ndani ili tupate wataalamu wetu hapahapa.”