Arusha. Wakiwa na ndoto za kuufikia urubani wa ndege, uhandisi na utaalamu wa filamu, manusura watatu wa ajali ya gari la Shule ya Lucky Vincent walipitia magumu, ikiwemo kupigania uhai wao saa 20 angani wakielekea kupata matibabu nchini Marekani.
Simulizi hiyo, inayomhusu Doreen Mshana, Sadia Awadh na Wilson Tarimo, imetolewa leo, Jumamisi Mei 24, 2025, na Daktari Bingwa wa Mifupa na Majeraha Mkoa wa Arusha, Elias Mashala, aliyeambatana nao kwa kipindi cha miezi minne ya matibabu yao.
Ajali ya basi la Shule ya Msingi Lucky Vincent ilitokea Mei 6, 2017, katika eneo la Rothia, wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha, wakati wakienda kufanya mitihani ya ujirani mwema. Yalikuwa ni maandalizi ya kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi, ajali hiyo ilisababisha vifo vya wanafunzi 32, walimu wawili na dereva.

Vijana Wilson Tarimo, Sadia Awadh na Doreen Mshana wakati wa mahafari yao nchini Marekani.
Amesema safari ya watoto hao ilikuwa ngumu kwa sababu walikuwa wameumia sana, ingawa walikuwa imara kuweza kusafiri.
“Kazi ya kwanza ilikuwa kuhakikisha wamekuwa stable. Tulisafiri nao zaidi ya saa 20 angani, tulibeba dawa na baadhi ya vipimo kama vya presha, kipimo cha oksijeni, dawa za maumivu, dripu na vitu vingine vya kuwafanya waweze kukaa muda mrefu katika ndege bila changamoto,” amesema Dk Mashala kutoka Hospitali ya Mount Meru.
Amesema ndege ilikuwa nzuri na waliungwa mkono na wafadhili Samaritan’s Purse linaloongozwa na Mchungaji Franklin Graham, ambao walitoa ndege binafsi kuwachukua nchini.
Hata hivyo, amesema changamoto kubwa waliyopata ni kuwa safari ilikuwa ndefu na watoto walikuwa wamekaa sana, hivyo walichoka.
Dk Mashala amesema walivyofika nusu ya safari baada ya kuimaliza Afrika, wakati wanaelekea katika Bahari kubwa ya Atlantiki inayotenganisha Amerika upande wa magharibi na Afrika na Ulaya upande wa mashariki, hali za watoto hao zilibadilika.
“Hali ilikuwa ngumu kidogo kwa sababu ya mawimbi makubwa ya bahari, ndege ilibidi iende juu sana, kwa hiyo wapo wengine kiwango chao cha oksijeni kilishuka mno, lakini tulipata usaidizi kutoka kwa rubani wa ndege na wahudumu. Kwa pamoja tukawasaidia na watoto wakafika salama,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk Mashala, hayo yaliwezekana kwa kuwa walijipanga, kwa kuwa pia walikuwa na mafunzo ya kutosha.

Muonekano wa basi la wanafunzi wa Shule ya Lucky Vincent likiwa limetumbukia kwenye korongo.
Amesema matibabu yalichukua zaidi ya miezi mitatu. “Tuliondoka Mei, tukarudi Agosti. Kipindi hicho chote kilikuwa matibabu mbalimbali. Mara ya kwanza zilikuwa ni operations zote, zilifanyika wiki ya kwanza.”
Hiyo ni tofauti na Doreen ambaye alifanyiwa upasuaji mara mbili kabla ya kupelekwa kitengo cha kuzuia maambukizi kutokana na changamoto nyingi zilizokuwa zikimsumbua.
“Tukiwa huko, kulikuwa na tiba mazoezi, tiba saikolojia, shule, physiotherapy, haya yote yalikuwa ni kumfanya mtoto arudi katika hali yake ya kawaida, na yalikuwa yanatolewa sehemu mbalimbali.”
Kwa miezi minne walipatiwa matibabu katika mji wa Sioux City, Jimbo la Iowa, na baadaye Doreen alihamishiwa katika kituo cha Madonna, Jimbo la Nebraska, kwa ajili ya mazoezi zaidi kutoka kwa wataalamu wa uti wa mgongo walioambatana na wataalamu Watanzania, Dk Mashala na muuguzi.
Dk Mashala amesema anafuraha kuona wanafunzi hao wamefanikiwa kuendelea na masomo na kufikia hatua ya ngazi ya Stashahada ya Juu (Associate Degree) ambayo walikuwa wakiitamani.
“Namshukuru Mungu kuona tulichokifanya wakati wa matibabu kilisaidia kurejesha afya zao na kuendeleza ndoto zao za kuwa watu walioelimika.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Sadhia Abdallah (wa pili kulia) Doreen Mshana wa kwanza (kulia), Wilson Tarimo ( wa pili kushoto) alipokutana nao Oktoba 31, 2024, mjini Iowa, nchini Marekani.
“Mara ya mwisho nilikutana na watoto hao Julai, mwaka 2024, tulikuwa na kambi ya madaktari wa Marekani na sisi huko. Walikuwa imara na wenye akili, walishirikiana nasi wengine kuhakiki taarifa za wagonjwa, wengine kupiga picha kama ilivyo kwa watoto wengine, na afya zao zilikuwa nzuri,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk Mashala, alipobadilishana nao mawazo walimweleza mambo mengi, ikiwemo ndoto zao ambapo Doreen alisema anataka kuwa mtaalamu wa masuala ya utengenezaji filamu, Sadia anataka kuwa rubani na Wilson kuwa injinia.
“Walinieleza hayo, hizi ni hatua za mwanzo za shule. Wakimaliza hatua hizo, naamini wataendelea hatua nyingine mpaka wafikie ndoto zao,” amesema.
Mkuu wa Shule ya Msingi Lucky Vincent, Mwalimu Ephraim Inday, amesema amefurahishwa na hatua waliofikia kitaaluma wanafunzi hao, kuhitimu ngazi ya Stashahada ya Juu (Associate Degree) nchini Marekani.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo, amesema taarifa hizo zinawapa faraja kubwa kama shule, wazazi na watu wote wenye mapenzi mema kutokana na jambo kubwa lililotokea.
“Sikuwa na taarifa hizo, ila nafahamu wafadhili wao wa Marekani waliwapa ufadhili wa masomo hadi ya elimu ya juu. Mimi binafsi na shule kwa ujumla tumepata faraja kubwa, tunaamini watafikia ndoto zao,” amesema Mwalimu Ephraim.

Wanafunzi Sadhia Abdallah (wa kwanza kushoto) Doreen Mshana wa kwanza (kulia) na Wilson Tarimo.
Juzi, Waziri wa zamani, Lazaro Nyalandu alituma ujumbe kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram kuwa: “Wengi wetu tutawakumbuka watoto walionusurika ajali ya basi la Lucky Vincent (Sadia, Doreen na Wilson) mwaka 2017. Sasa, kwa neema ya Mungu, wamehitimu Community College nchini USA na wataendelea na masomo ya juu katika vyuo vikuu.
“Mwaka 2018 walijiunga na elimu ya sekondari katika shule ya Star High School iliyopo wilayani Arumeru, kupitia ufadhili wa taasisi ya Siouxland Tanzania Education Medical Ministries (STEMM), kisha kurejea nchini Marekani kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu.
“Vijana hao Doreen Mshana, Sadia Awadh na Wilson Tarimo wamehitimu katika taasisi ya Western Iowa Technical Community College, Jimbo la Iowa, nchini Marekani na wataendelea na ngazi ya shahada ya kwanza kwa muda wa miaka miwili.” ameandika
Ajali ya basi la Lucky Vincent ni mojawapo ya matukio ya kusikitisha zaidi katika historia ya usafiri wa shule nchini Tanzania.
Ajali ilitokea wakati basi lilipokuwa likishuka kwenye mteremko mkali katika hali ya mvua, ambapo basi liliteleza na kuanguka kwenye korongo la mteremko, likiwa na abiria 38, wakati uwezo wake ulikuwa ni abiria 30.
Taarifa kutoka kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, zilisema kuwa ajali ilitokana na mteremko mkali, mvua kubwa, na mwendo kasi wa basi. Aidha, uchunguzi ulionyesha kuwa basi hilo halikuwa na viti vya usalama (seat belts), jambo lililochangia kuongezeka kwa madhara.
Rais wa wakati huo, Dk John Magufuli, alielezea tukio hili kama ‘janga la kitaifa’ na kutoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao. Serikali ilianzisha uchunguzi wa kina kuhusu ajali hiyo, huku pia ikitoa maelekezo ya kuboresha usalama wa vyombo vya usafiri wa shule.
Mmiliki wa shule, Innocent Mushi na Makamu Mkuu wa Shule, Longino Nkana, walikamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya kukiuka sheria za usalama wa barabarani, ikiwa ni pamoja na kusafirisha wanafunzi bila kibali cha Bodi ya Leseni ya Usafirishaji (TLB) na kutumia basi lililozidi uwezo wake wa kubeba abiria.
Shule ya Lucky Vincent ilifungwa kwa muda ili kutoa nafasi kwa wanafunzi na walimu kushughulikia majonzi. Wanafunzi watatu pekee walinusurika katika ajali hiyo, na walikimbizwa Marekani kwa matibabu maalumu.
Ingawa shule ilifunguliwa tena, majonzi yalikuwa bado yakionekana katika nyuso za wanafunzi na walimu. Serikali ilianzisha mpango wa ushauri nasaha kwa wanafunzi wa shule hiyo ili kuwasaidia kushughulikia maumivu ya kihisia yaliyosababishwa na tukio hilo.
Ajali ya Lucky Vincent inabaki kuwa kielelezo cha umuhimu wa kuzingatia sheria za usalama barabarani, hasa katika usafiri wa wanafunzi, na inatoa fundisho kuhusu umuhimu wa kuwa na miundombinu bora ya barabara na vyombo vya usafiri salama.