DPP alivyowang’ang’ania walioachiwa huru kwa mauaji Zanzibar

Zanzibar. Mahakama ya Rufani Zanzibar imebatilisha uamuzi wa kuwaachia huru washtakiwa watatu waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kuua na badala yake, imewaona wana kesi ya kujibu, hivyo kutakiwa kujitetea kortini.

Watuhumiwa hao walikuwa wamefunguliwa shtaka la mauaji ya kukusudia kuwa Januari 17, 2017 saa 3:00 asubuhi, huko eneo la Tumbe Magogoni, Chakechake Pemba, walimshambulia na kumuua Khamis Abdallah Haji.

Uamuzi wa kuwaachia huru Moh’d Said Soud, Suleiman Nassour Suleiman na Jumma Kassim Ally, kwa maelezo kuwa upande wa Jamhuri ulishindwa kujenga kesi yao, ulitolewa Juni 15, 2021 na Jaji Abraham Mwampashi wa Mahakama Kuu.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) hakuridhishwa na uamuzi huo, akaamua kufungua rufaa namba 428 ya 2023, akiegemea sababu tatu, ikiwamo kuwa Jaji alikosea kisheria na kiushahidi alipoamua kuwa washitakiwa hawana kesi ya kujibu.

Sababu ya pili ni kuwa mahakama ilikosea kisheria ilipotoa uamuzi kuwa mauaji ya Khamis Abdallah Haji yalifanywa na wanakijiji wenye hasira kali na sababu ya tatu ni kuwa mahakama ilikosea ilipoona Jamhuri haikujenga kesi yake.

Baada ya kusikiliza rufaa hiyo, jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani— Augustine Mwarija, Issa Maige na Latifa Mansoor, limeona kuwa sababu za rufaa za DPP zina mashiko, hivyo kuwaona washtakiwa hao wana kesi ya kujibu.

Katika hukumu yao hiyo waliyoitoa Mei 22, 2025, na kuwekwa katika mtandao wa mahakama Mei 23, 2025, majaji hao wameamuru jalada la kesi hiyo lirudishwe Mahakama Kuu ili usikilizwaji wa shauri hilo uendelee kwa hatua ya washtakiwa kujitetea.

Ushahidi dhidi yao ulivyokuwa

Katika kuthibitisha shitaka hilo, Jamhuri waliita mashahidi saba ambapo kati yao, mashahidi wawili—Kombo Sharifu Kombo (shahidi wa tatu) na Juma Mohamed Juma (shahidi wa tano), ndio wanatajwa kushuhudia mauaji hayo.

Shahidi wa tatu, ambaye ni mwalimu wa Quran eneo la Madungu Fuweni, alieleza kuwa siku ya tukio alisikia kelele nje ya nyumba yake, na alipotoka aliona kundi la watu wakimshambulia mtu huyo, aliwatambua Moh’d Soud na Juma Ally.

Kwa upande wake, shahidi wa tano, Juma Mohamed Juma, anayeishi eneo la Kichangani, alieleza kuwa anaishi jirani na mshtakiwa wa kwanza, Moh’d Soud, na siku ya tukio alisikia kelele kutoka nyumba ya mshtakiwa huyo.

Alikwenda katika nyumba hiyo na kumkuta Khamis Abdallah Haji (sasa marehemu) akiwa amefungwa kamba mikononi, na alikuwa anavuja damu. Aliona washtakiwa, kwa kushirikiana na watu wengine, wakimshambulia.

Alidai katika ushahidi wake kuwa mshitakiwa huyo alimweleza kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa amemwibia nazi na sasa amemwibia ndizi, na wakati huo mshtakiwa alikuwa anajaribu kumbebesha mzigo huo wa ndizi.

Shahidi huyo aliiambia mahakama kuwa aliwashauri washtakiwa wampeleke mtuhumiwa kituo cha Polisi, lakini badala yake walimwingiza kwenye gari linalomilikiwa na mshtakiwa wa kwanza, Moh’d Said Soud.

Mashahidi wengine wote hawakushuhudia tukio hilo la mauaji, lakini walisimulia nini kilitokea kabla na baada ya tukio, akiwemo shahidi wa pili, Sheha wa Magogoni Juma Kombo Khairalla, aliyeeleza kuwa marehemu aliingia kwake akiwa na kisu na akituhumiwa kuiba ndizi.

Shahidi wa nne, Konstebo wa Polisi Raya anayefanya kazi Kituo cha Chake Chake, alieleza kuwa kabla ya tukio hilo, mshtakiwa wa kwanza alitoa taarifa kuwa ameibiwa tenki la maji na alimshuku marehemu kuwa ndiye mwizi.

Kwa mujibu wa ushahidi wake, mshtakiwa alitoa matamshi mbele ya shahidi huyo kuwa akimkamata Khamis Abdallah Haji angemtia adabu, lakini shahidi huyo alimwonya hatari ya kujichukulia sheria mkononi.

Baada ya Jaji kusikiliza ushahidi wa mashahidi hao na wengine waliokuwa maofisa wa Polisi na daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, aliona kuwa washtakiwa wote hawakuwa na kesi ya kujibu na kuwachia huru. Uamuzi huo ndio ulimfanya DPP kukata rufaa na kushinda.

Katika usikilizwaji wa rufaa hiyo, DPP aliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Seif Mohamed Khamis akisaidiwa na Wakili wa Serikali Shame Farhan Khamis, huku washtakiwa wote watatu wakitetewa na Wakili Rajabu Abdallah Rajabu.

Kuhusu dhamira ovu, Wakili Seif Khamis aliirejea mahakama katika ushahidi wa shahidi wa nne (Ofisa wa Polisi) aliyesema kuwa mshtakiwa wa kwanza alitoa taarifa ya kuibiwa na akasema akimkamata marehemu, atamtia adabu.

Wakili huyo alirejea ushahidi wa mashahidi wa tatu na wa tano waliowashuhudia washtakiwa wakimshambulia marehemu, ambapo shahidi wa tano aliwashauri wampeleke Polisi, lakini walimchukua na kumwingiza kwenye gari.

Alihoji kuwa mauaji hayo yalikuwa ya kikatili, akirejea ushahidi wa shahidi wa saba aliyesema mwili wa marehemu ulikuwa umetapakaa damu na alijeruhiwa mwili mzima na kwamba washtakiwa walikuwa na dhamira ya pamoja.

Wakili wa washitakiwa alipinga rufaa hiyo, akisema Jaji alikuwa sahihi kwamba upande wa Jamhuri ulikuwa umeshindwa kujenga msingi wa kesi na ndio maana washtakiwa walionekana hawana kesi ya kujibu.

Alidai hakuna shahidi hata mmoja aliyewanyooshea kidole washtakiwa kuwa walihusika moja kwa moja na kifo cha marehemu, akisisitiza kuwa ni wananchi wenye hasira kali waliomshambulia.

Alinukuu ushahidi wa shahidi wa tatu akisema washtakiwa walikuwa umbali wa mita 3.5 kutoka kwa marehemu, hivyo walikuwa watazamaji, si washiriki.

Kuhusu ushahidi wa shahidi wa tano, aliyesema aliwaona wakimshambulia marehemu, wakili alisema hakufafanua ni namna gani walikuwa wanamshambulia wala hakusema kama walitumia fimbo, mawe au marungu yaliyokutwa eneo la tukio.

Majaji walisema DPP alilenga kupindua uamuzi wa kuwaachia washtakiwa huru kwa hoja kuwa hawakuwa na kesi ya kujibu na kwamba Jamhuri ilipaswa kuthibitisha bila mashaka kuwa walihusika.

“Hoja ya kutafutiwa majibu ni kama kulikuwa na ushahidi wa upande wa mashitaka, bila kujali kuaminika kwake au uzito wa kutosheleza, ili kuwafanya washtakiwa waweze kuwasilisha utetezi wao dhidi ya tuhuma hizo,” walisema.

Majaji walisema ushahidi wa Jamhuri ulithibitisha juu ya kifo cha Khamis Abdallah Haji kilichotokea Januari 17, 2017, ikiwamo ripoti ya daktari aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu.

Ripoti hiyo ilieleza kuwa mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha mengi na michubuko, ishara kuwa alishambuliwa na watu kwa kutumia vitu butu.

Pia majaji hao walisema ushahidi wa shahidi wa saba (Ofisa wa Polisi) ulithibitisha kuwa eneo la tukio lilikuwa umbali wa mita 300 kutoka Kiganjani ambapo mshtakiwa wa kwanza alisema tukio lilitokea na hivyo kuthibitisha walikuwepo eneo la tukio.

“Hii inathibitisha uwepo wa washtakiwa katika eneo kulipotokea mauaji. Ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri pia unathibitisha kuwa marehemu alikufa mikononi mwa washtakiwa. Hii inaweza kuthibitisha ushiriki wao,”walieleza.

Majaji hao walisema katika hatua ya sasa, mahakama haitakiwi kwenda hadi katika uhalali wa ushahidi dhidi ya washtakiwa au kufanya uchambuzi wa kina wa ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri au kufanya jambo litakaloathiri utetezi.

“Itoshe kusema kuwa ushahidi uliotolewa na mashahidi wa Jamhuri umethibitisha viashiria vya kosa la mauaji ya kukusudia. Katika hii kesi, hakuna ubishi kuhusiana na uwepo wa kifo kutokana na taarifa ya daktari aliyefanya uchunguzi,”walisema.

“Uwepo wa washtakiwa katika eneo la tukio nalo ni jambo lilithibitishwa na mashahidi wa Jamhuri. Tunaona kuwa Jamhuri imewasilisha ushahidi wa kutosha wa kufikia hitimisho kuwa wana kesi ya kujibu na wanapaswa kujitetea”

Related Posts