Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amewataka vijana nchini kujiepusha na uvunjifu wa amani kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, akisisitiza kuwa wana jukumu la kulinda amani kwa wivu mkubwa.
Makonda ameyasema hayo leo Jumamosi Mei 24, 2025 wakati wa ziara ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa mkoani Arusha akiwa na viongozi wa dini na mila.
Akizungumza na vijana wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa uwanja utakaotumika katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2027) jijini Arusha, amesema ni muhimu kundi hilo la vijana kukataa kutumika.
“Kipindi hiki cha uchaguzi mtasikia watu wengi na mambo mengi, wengine watawakashifu viongozi wetu na watajionyesha wao miamba kabisa. Wataeleza matatizo asubuhi mpaka usiku, niwaombe jambo moja, katika yote watakayowashawishi msikubali kuvunja amani ya mkoa wetu,” amesema.
Awali, akizungumza katika eneo la Lakilaki lililopo Kata ya Mateves ambapo kunajengwa majengo ya Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu, Makonda amesema ni muhimu viongozi hao kuhamasisha amani.
“Ujenzi wa Mahakama hii kwa fedha ya Serikali Sh62.9 bilioni inaonyesha dhamira ya Rais ambaye ni mlinda haki za makundi yote, anayetetea na kupigania haki ya kila mtu, angekuwa kiongozi asiyependa kulinda haki za binadamu, asingekubali kutoa fedha za Serikali kujenga Mahakama hii inayosimamia haki za binadamu.
“Niwaombe viongozi wa mila na dini, msaidie kuendelea kuhamasisha amani na utulivu katika nchi yetu hasa katika kipindi hiki tunapoelekea uchaguzi mkuu,” amesema Makonda.
Kuhusu mkoa huo kuwa wa kidiplomasia, amesema wamejipanga kuhakikisha wanabadilisha uchumi wa wananchi na kuvutia wawekezaji zaidi na kuwa watafanya mazungumzo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Waziri wa Mambo ya Nje ili eneo la kuanzia Burka hadi Lakilaki kutengenezwe mpango mji mpya.
“Tunatamani Arusha tutengeneze mji wa kidiplomasia katika eneo hilo la ekari 5,000, zipimwe na kupanga upya ili tukaribishwe wawekezaji, tunataka kuanzia Watanzania hadi duniani wawekezaji waje kujenga hoteli na miradi mingine ili tubadilishe mji na kutengeneza uchumi na kuvutia uwekezaji,” amesema.
Msimamizi wa mradi huo wa unaotekelezwa na kampuni kutoka China ya CRJE, Mhandisi Gregory Mbuya amesema mradi huo ulianza Agosti 28, 2023 ambapo una majengo sita ikiwemo jengo kuu la Mahakama, kumbi za mikutano na mgahawa.
“Katika awamu hii ya kwanza, eneo hili mradi unaojengwa hapa lina ukubwa wa ekari 16 na ikikamilika tutahamia ujenzi wa eneo la eka 12 ambapo kutajengwa nyumba za majaji na watumishi wengine wa mahakama,” ameongeza.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa mila, mshili mkuu wa kabila la Meru, Mbise, amepongeza Serikali inavyoendelea kutekeleza miradi mbalimbali na kupunguza umaskini.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania, Askofu Dk Israel Maasa alisisitiza vijana nchini kutokujihusisha na uvunjaji wa amani kipindi cha uchaguzi.
“Tunapoelekea miezi ya uchaguzi, nawaasa vijana kutunza amani ya nchi yetu, leo tunakusanyika hivi kwa sababu ya amani tuliyonayo, sisi kama viongozi wa dini tunapenda kuwaasa tulinde amani hii kwa wivu mkubwa.
“Kataeni kutumika vijana, anayekufata kukuambia uharibu amani, kwenda barabarani au kutulia lugha za matusi na kejeli tukatae. Kila mmoja asimame awe mtetezi wa amani ya Mkoa wa Arusha na Taifa kwa ujumla,” amesema Dk Maasa.
Naye Sheikh Khamis Kassim amesema utekelezaji wa miradi mbalimbali unafanikiwa kwa sababu ya amani hivyo ni muhimu kuendelea kutunzwa kwani bila amani na utulivu hakuna kinachoweza kufanyika.
“Haya tunayoona yanafanywa na Serikali amani na utulivu ndiyo huwezesha haya ila kumeanza chokochoko, tukinyamaza italeta shida tunapoona jambo ni baya hatuna namna nyingine zaidi ya kulinda amani yetu.
“Moto huanza na cheche kidogokidogo, mwishowe unalipuka. Tuendelee kumuomba Mungu atujaalie tuwe na amani na utulivu,” amesema.