Dar es Salaam. Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki amewataka viongozi wa Bara la Afrika kuwa wakweli na waaminifu katika kulinda masilahi ya bara lao, ili kufanikisha malengo ya kukuza uchumi na kuboresha maisha ya Waafrika.
Mbeki ameyasema hayo katika hafla ya chakula cha jioni iliyofanyika Mei 23, 2025 jijini Dar es Salaam.
Mbeki amesisitiza kuwa maendeleo ya Bara la Afrika yatapatikana endapo viongozi wataweka mbele masilahi ya nchi zao na kuongoza kwa uadilifu, uwazi na dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko chanya kwa Waafrika wote.

Amesema katika kuadhimisha Siku ya Afrika mwaka huu iliyobebwa na kaulimbiu isemayo “Haki kwa Waafrika na Watu wa Asili ya Kiafrika Kupitia Fidia Kuangazia Historia Yetu na Kuunda Mustakabali Wetu’ aliwakumbusha kuwa haki siyo mwisho, bali ni dai endelevu.
“Ni dai endelevu la ukweli, heshima, na uongozi unaoakisi hali halisi za watu wetu. Tuwekeze katika elimu, ubunifu, ushirikishaji wa vijana katika maamuzi, na kupambana na ufisadi unaoharibu maendeleo,” amesema Mbeki.
Amesema Bara la Afrika lina utajiri na uwezo mkubwa ambao unahitaji viongozi wanaowaza zaidi ya uchaguzi, wasioogopa uwajibikaji, wenye maono na wanaotanguliza maslahi ya wananchi wao na Taifa, kuliko matakwa yao binafsi.

Awali Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema ni wakati kila Mwafrika kutakafari mafanikio, changamoto na matarajio ya kuinua maendeleo ya Afrika kwa amani ya utulivu.
Pia, amesema kuna umuhimu wa kuwaenzi viongozi walioendeleza fikra za Uafrika na wanaoendelea kupigania ukombozi wa kiuchumi na mshikamano wa Bara la Afrika kwani wameacha urithi kwa kizazi cha sasa na kijacho.
“Nichukue nafasi hii kusema kuwa tunawakumbuka na kuwapongeza waanzilishi wa Umoja wa Afrika (OAU) ambao ndoto yao ya kuunganisha na kushirikisha zaidi mataifa ya Afrika imeendelea kuishi hadi leo.
“Tunawakumbuka pia kwa heshima kubwa viongozi waliowafuata, ambao waliendeleza dhima ya Uafrika (Pan-Africanism) na wanaoendelea kupigania ukombozi wa kiuchumi na mshikamano wa bara letu tukufu,” amesema Kombo.
Hafla hiyo iliwakutanisha pamoja mabalozi viongozi wa Serikali, Mabalozi wastaafu, viongozi wa serikali, wanadiplomasia, wasomi, pamoja na wawakilishi wa asasi za kiraia na kijamii kwa ajili ya kusherehekea mshikamano, utofauti na maendeleo ya Afrika.