Dar es Salaam. Wakati Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee, akitoa msimamo wake kuhusu Chadema kususia uchaguzi na kueleza mwelekeo wa alichoamua katika kugombea ubunge, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wamekuwa na mtazamo tofauti.
Mdee ametoa msimamo wake huo jana, Ijumaa Mei 23, 2025, katika mahojiano yake maalumu na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Katika mahojiano hayo, Mdee ameendelea kusisitiza kuwa yeye bado ni mbunge wa Chadema, huku akieleza kuwa Chadema kususia uchaguzi haoni kama kuna tija.
Wakati Mdee akieleza hayo, mara kadhaa uongozi wa Chadema umesisitiza kuendelea na kampeni ya ‘No Reforms, No Election’ kudai mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi, bila kujali vitisho vya kukamatwa, kufungwa mahabusu wala gerezani.
Msimamo huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche, wakati akihutubia mikutano ya hadhara katika kijiji cha Bukokwa, Halmashauri ya Buchosa, kwenye uwanja wa stendi ya zamani mjini Sengerema mkoani Mwanza, alipokuwa akiinadi kampeni hiyo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Akizungumza na BBC, Mdee amesema anachojua hadi sasa yupo Chadema, japo chama hicho hakishiriki uchaguzi.
“Michakato ya uchaguzi ni Oktoba, na michakato inaanza Bunge likivunjwa, lakini chama ambacho nipo mpaka sasa hakishiriki uchaguzi. Kimesema kwa kauli zao kwamba hakishiriki uchaguzi mpaka pale reforms zitakapofanyika.

Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee akionyesha alama zinazotumiwa na vyama vya upinzani cha Chaumma na Chadema alipokuwa ndani ya ukumbi alipohuduria kikao cha 30 cha mkutano wa 19 wa Bunge la Bajeti, jijinni Dodoma Mei 22, 2025. Picha na Edwin Mjwahuzi
“Katika hili niseme inategemea unayemsususia akili yake ikoje. Unajua wakati mwingine flexibility (kubadilika) ina maana yake kubwa sana,”amesema na kuongeza;
“Ukishajua kwamba unapambana na mtu wa aina gani na level gani, lazima na wewe u-strategise (uwe na mikakati) kupambana na huyo mtu kwa level kadha wa kadha, ukiangalia faida na hasara za muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu.”
Akieleza msimamo wake kuhusu kugombea ubunge, Mdee amesema katika hatua ya kwanza, inategemea kuanzia sasa mpaka Bunge likivunjwa na itakuwa kwa utaratibu upi.
“Vilevile kama sitagombea, inategemea Bunge likivunjwa, nitatoa uamuzi gani na kusema kwa nini sitagombea,” ameeleza Mdee ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Kawe.
Hata hivyo, mbunge huyo ametoa tahadhari kuwa, awe yeye atagombea kupitia upinzani au wengine watakaogombea kupitia upinzani, kwa kuwa si mtu wa kuamini katika kususa na kueleza hakusaidii.
Kauli ya wachambuzi wa siasa
Mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mohammed Bakari, amesema katika kauli yake hiyo, Mdee bado ameacha tungo tata, kwa kuwa hajaamua kufunguka moja kwa moja.
“Amefanya hivyo kwa kuwa anajua bungeni anatambulika kama Mbunge wa Chadema, hivyo kuhofia huenda akisema anaenda chama fulani akafukuzwa,” amesema Profesa Bakari.
Hata hivyo, alivyoulizwa mbona wabunge wengine wamekuwa tayari kutangaza kuhama licha ya kuwa bado wapo Bungeni, mchambuzi huyo amesema hilo pia linategemea utashi wa mtu binafsi, na huo ndiyo uamuzi wa Mdee ulipofikia na kutaka watu wasubiri Bunge litakapovunjwa.
“Kila mtu ana mtazamo wake. Huenda walioamua kujilipua licha ya kuwa bado wapo bungeni wamejua hawana watakachokipoteza hata wakitangaza mapema kuhamia chama kingine,” ameeleza Profesa Bakari.
Naye wakili na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Dk Onesmo Kyauke, amesema kwa kauli ya Mdee ni wazi kwamba hayupo pamoja na Chadema, na lolote litarajiwe katika kukihama chama pindi Bunge litakapovunjwa.
“Msimamo wake wa kuwa yeye bado ni Chadema sio kweli kwa kuwa chama tayari kilishamfukuza na walipewa masharti ya nini wafanye kama wanataka kurejea, ambayo hadi leo sidhani kama waliyatekeleza.
“Pili, katika ushauri wake kwamba haoni kama kususia uchaguzi ni sawa, ni wazi kwamba anaonekana haungi mkono kampeni na msimamo wa Chadema, hivyo hizo ni sababu tosha za kumuona hayupo pamoja na chama hicho isipokuwa anasubiri Bunge livunjwe, atangaze anapohamia na atakapogombea,” amesema Dk Kyauke.
Hata hivyo, kuhusu wabunge waliokuwa kundi moja na Mdee na tayari wametangaza kuhamia chama kingine, amesema kilichotakiwa ni kwamba wasiruhusiwe kuhudhuria bungeni tangu siku waliyotangaza, isipokuwa ni sheria tu zimeamua kuvunjwa kwa makusudi.
Amefafanua kuwa sheria zilizopo zinataka kila mbunge aliyepo ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria, lazima awe amepitia chama fulani, na kuhoji kama hao hawapo chama chochote wanasimamiwa na sheria gani.
Katika mahojiano hayo pia Mdee aligusia kuhusu wabunge 19, akiwemo yeye walivyoingia bungeni.
Mdee amesema isivyo bahati katika sakata hilo dunia haikupata ukweli wa upande wa pili ya nini kilichojiri mpaka wabunge wale wakaenda kuapa.
Amebainisha kuwa wabunge wale si wa kuokoteza na pia si watu ambao wanaweza kufanya maamuzi ya hovyo hovyo.
“Halima sikupeleka barua tume, ila barua tume ilipelekwa na mamlaka ya chama,” amesema.
Mdee anawaweka watu njia panda kuhusu chama atakachokwenda kugombea, ikiwa tayari wabunge watatu kati ya wale 19 aliokuwa nao kundi moja wameshaonyesha mwelekeo wao.
Kati ya wabunge hao ambao mpaka sasa wameshakihama chama yupo Nusrat Hanje, ambaye Mei 18, mwaka huu aliwatangazia wananchi wa Mkoa wa Singida na Watanzania kwa ujumla kuwa amehamia CCM.
Nusrat, ambaye ni mbunge wa viti maalumu kundi la vijana kutoka mkoa huo, alisema hayo wakati wa mkutano wa hadhara alioufanya viwanja vya stendi ya zamani, Ikungi mjini, huku akisema kwa miaka mitano aliyodumu bungeni ameiva na sasa anatafuta changamoto nyingine za kisiasa nje ya Chadema.
Ukiacha Nusrat, yupo Jesca Kishoa, ambaye bado hajaweka wazi msimamo atagombea jimbo gani, licha ya kuwa mwaka 2020 aliwahi kugombea Iramba Mashariki, jimbo ambalo kwa sasa linaongozwa na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba.
Kishoa aliweka hilo wazi katikati ya Februari mwaka huu alipofanya ziara mkoani Singida akiwa amevalia mavazi yenye rangi ya kijani, huku nyimbo zilizokuwa zikipigwa zilikuwa za CCM, ikiwemo ile inayoimba “Namletaa Rais, namleta mwenyekiti,” iliyoimbwa na msanii Diamond Platnumz.
Naye Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya, Sophia Mwakagenda, Aprili 29 alitangaza kujiunga na CCM, akisema uamuzi huo unalenga kuendeleza jitihada zake za kuwatumikia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza mbele ya mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Bulyaga iliyopo Tukuyu, mkoani Mbeya, alitumia nafasi hiyo kuwaaga wanachama wa Chadema, akikipongeza kwa kumlea na kumjenga kisiasa tangu aanze safari yake ya uongozi.
Kina Mdee walivyofukuzwa uanachama
Wabunge hao 19, akiwemo Mdee, walivuliwa uanachama wa Chadema Novemba 27, 2020, wakituhumiwa kwa usaliti, kughushi nyaraka za chama, kisha kujipeleka bungeni jijini Dodoma kuapishwa.
Hata hivyo, Mdee na wenzake walikata rufaa Baraza Kuu la Chadema dhidi ya uamuzi huo wa Kamati Kuu. Baraza Kuu lilipokutana Mei 11, 2022 katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, lilitupilia mbali rufaa yao.
Baada ya uamuzi wa Baraza Kuu, walikwenda mahakamani, ambako walikuwa na ombi la kufungua shauri Mahakama Kuu. Kesi ilichukua hatua mbalimbali na ilibatilisha uamuzi wa Baraza Kuu lililobariki kuvuliwa uanachama kwa Mdee na wenzake.
Februari 23, 2025, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu, akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake Tegeta, jijini Dar es Salaam, alisema endapo wabunge hao wanataka kurudi Chadema, mahali pa kuanzia si kwa mwenyekiti.
Lissu alisema wabunge hao watapaswa kuandika barua ya kuomba kurudishiwa uanachama kwa kumpelekea Katibu Mkuu, ambaye naye katika ajenda za Baraza Kuu ataweka na hiyo kama sehemu ya ajenda, Baraza Kuu litajadili.
“Mimi ni Mwenyekiti wa Baraza Kuu, lakini wenye uamuzi kwenye hili ni wajumbe wa Baraza Kuu. Hata nikisema siwataki kabisa, japo sijawahi kusema hivyo bado nitawauliza wajumbe wa Baraza Kuu wanaoafiki waseme ndiyo, na wasioafiki waseme sio, na kutoa majibu,” alisema na kuongeza;
“Utaratibu unasema hivi, mwanachama aliyefukuzwa, akitaka kurudi, atakwenda kuomba msamaha au kuomba kurudi kwenye kikao kilichomvua uanachama.
“Hicho kikao kitamsikiliza, kikikubaliana na maombi yake kitapekeleka mapendekezo kwenye kikao cha juu. Hawa walifukuzwa na Baraza Kuu, kabla walifukuzwa na Kamati Kuu, ndipo Baraza Kuu likaridhia.”