Unguja. Mwakilishi wa Mwanakwerekwe, Ameir Abdalla Ameir ameihoji Serikali kinachokwamisha kukamilisha sera ya Kiswahili wakati ikijua wazi kwamba sera ndio mlezi wa lugha.
Ameir ameibua hoja hiyo leo Mei 24, 2025 alipouliza swali kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo katika mkutano wa 19 wa baraza la wawakilishi Chukwani Zanzibar.
Mbali na kuhoji mchakato huo kuchelewa, pia ametaka kufahamu maabara za matumizi ya Kiswahili zilizipo mpaka sasa kisiwani humo na kwa kiasi gani maabara hizo zinatoa mchango mkubwa katika makuzi ya lugha ya kiswahili.
Akijibu maswali hayo, Kaimu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Shaaban Ali Othman amesema ni kweli sera hiyo ina muda mrefu tangu ianze kuandaliwa lakini kwa sasa ipo kwa wadau muhimu wanatoa maoni yao kisha wakikamilisha, watachaka mawazo hayo na kuifikisha kwenye vyombo vingine kwa hatua zaidi.
“Sera ya lugha ya Kiswahili kwa sasa ipo kwa wadau muhimu wa lugha ya kiswahili kwa ajili ya kuipitia na kutoa maoni yao ya mwisho kabla ya kupelekwa katika ngazi za juu kwa majadiliano na ukamilishaji wake,” amesema Kaimu Waziri Shaaban ambaye ni Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi.
Hata hivyo, amesema hawezi kusema ni lini itakamailika kwa sababu ya michakato yake lakini wana imani itakamilika kwa haraka kulingana na uhitaji wake.
Kuhusu hoja ya mwakilishi wa nafasi za wanawake, Shadya Mohamed Suleiman jinsi gani serikali imejipanga kutumia kiswahili fasaha badala ya kupotosha kama inavyofanyika, Kaimu Waziri Shaaban amesema; “Tumejipanga vyema kuhakikisha Kiswahili kinatumika vyema na kadri kinavyokuwa ndivyo kinavyopelekwa kwa watumiaji.
Kuhusu maabara zilizopo za Kiswahili, amesema Wizara ipo katika mchakato wa kulipatia Baraza la Kiswahili Zanzibar (Bakiza), jengo lenye nafasi ya kuweka chumba cha maabara ya lugha ili kazi za mafunzo na majaribio ya lugha yafanyike kwa ufanisi zaidi.
“Maabara ni eneo la kujifunza kwa vitendo ambalo mwanafunzi hujifunza stadi nne za lugha kwa urahisi, maabara itasaidia kuikuza lugha ya kiswahili kutoa mafunzo ya Kiswahili na utamaduni wake kwa wageni na wenyeji ambao watajifunza msamiati mpya wa kiswahili na kuwafunza wengine ndani na nje ya Zanzibar,” amesema.
Stadi nne zilizotajwa na waziri ni kusikiliza, kusoma, kuandika na kuzungumza lugha.