Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ametangaza kusogezwa mbele kwa operesheni yao ya C4C (Chaumma For Change) ambapo sasa itazinduliwa Juni Mosi, 2025 jijini Mwanza badala ya Mei 30, 2025 iliyotangazwa awali.
Operesheni hiyo ya Chaumma, itakayofanyika kwa kutumia chopa, ina lengo la kuimarisha chama hicho na kutambulisha uongozi mpya kwa wanachama na wananchi wengine katika maeneo yao.
Me 21, 2025, Chaumma kilifanya mkutano mkuu maalumu ambapo kiliwapokea wanachama wapya 3,000 waliokihama Chadema, huku Mwalimu alitangaza operesheni hiyo kwa kuzunguka mikoa mbalimbali kwa siku 16 mfululizo.
Akizungumza baada ya kikao cha kamati kuu kilichofanyika leo Jumamosi, Mei 24, 2025 wakati akisoma maazimio ya kikao hicho, Mwalimu amesema sababu ya kusogeza mbele ni baada ya kufanya mashauriano na baadhi ya vyombo vya habari vinavyotarajia kurusha tukio hilo mubashara.
“Vyombo hivyo vimetueleza siku hiyo kutakuwa na tukio lingine ambalo tayari wamepanga kwenye taratibu zao nalo litarushwa mubashara na halihusishi chama chetu, ni taasisi nyingine,” amesema Mwalimu.
Mwalimu amesema baada ya majadiliano hayo, wameridhia kupeleka mbele ili kuwawezesha Watanzania kupata haki ya kushuhudia uzinduzi huo mubashara kwa wale ambao hawatapata fursa ya kwenda Mwanza.
“Uzinduzi wetu tumepeleka mbele siku moja ili tuweze kufikia muktadha, na ifahamike shughuli yetu tutaizindua Juni Mosi, 2025,” amesema Mwalimu.
Mbali na opresheni hiyo, Mwalimu amesema wanatarajia kuziba mapengo kwenye nafasi za ngazi mbalimbali za uongozi.
“Kumekuwa na mapengo ya uongozi, sasa tumekamilika na tuna watu wenye uwezo wa kushika uongozi kila mkoa na kanda ili kukikifanya chama chenye mwonekano mzuri, kikubwa wanachama wajiandae kuomba,” amesema.
Vilevile, Mwalimu amesema wanakusudia kuunda kamati za kusimamia na kuendesha na kuratibu uchaguzi mkuu katika ngazi zote za kichama.
“Kamati zitakuwa na nguvu kikatiba na kuzipatia uwezo ili kutengenza wagombea kwa kufanya tafiti za kina kujua ni kina nani wanafaa kupeperusha bendera ya Chaumma katika uchaguzi mkuu ili kuhakikisha hakuna ombwe la uongozi na kimkakati,” amesema Mwalimu.
Katibu Mkuu huyo amesema chama hicho katika kipindi cha sasa hadi hapo utakapomalizika uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu, kitakuwa kinaendeshwa kwa mfumo wa uchaguzi.
“Chama chetu kitakuwa chombo cha kiuchaguzi katika ngazi zote kuanzia Taifa hadi chini, kila tunachofanya lazima kilenge na kihusishe moja kwa moja uchaguzi mkuu,” amesema.
Mwalimu ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar alipokuwa Chadema, amesema hawataki kuona chama hicho kinajiendesha kwenye mfumo wa kawaida kama ilivyokuwa huko nyuma kwa kuwa wanaenda kushindana kwenye uchaguzi mkuu na si kushiriki tena.
“Tumefanya hivi ili kuongeza kasi na nguvu ya kufikia mafanikio tuliyojiwekea ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu,” amesema.