Njombe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linamsaka mtuhumiwa aliyembaka mwanafunzi wa darasa la kwanza mwenye umri wa miaka sita, anayesoma katika shule ya msingi Selestini akiwa ni mkazi wa Mtaa wa Ngalanga, Halmashauri ya Mji wa Njombe.
Inadaiwa kuwa mtoto huyo amebakwa na mtu ambaye hajafahamika wakati akielekea shuleni na hadi sasa Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linaendelea kumtafuta.
Hayo yamebainishwa leo Mei 24, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya jeshi hilo zilizopo mkoani hapa.
Amesema tukio hilo limetokea Mei 22, 2025 saa 1 asubuhi wakati mwanafunzi huyo akiwa njiani kuelekea shuleni na uchunguzi wa kina unaendelea kufanyika ili kubaini mhusika wa tukio hilo.
“Kuna mtoto ambaye ana umri wa miaka sita, ni mwanafunzi wa darasa la kwanza katika shule ya Selestini. Akiwa anakwenda shule, alikutana na mwanaume ambaye bado hajafahamika na kumuingilia kimwili, tunaendelea kulifuatilia tukio hili kwa ukaribu zaidi kuhakikisha mtuhumiwa anapatikana,” amesema Banga.
Aidha, Kamanda Banga ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha kuwa wanawasindikiza watoto wao shuleni asubuhi na kuchukuliwa wanaporejea jioni au kutembea kwa makundi badala ya kwenda mmoja mmoja.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Ngalanga Julius Lulandala, amesema tukio hilo limetia hofu kubwa kwa wakazi wa eneo hilo na tayari wamechukua hatua za haraka kuimarisha ulinzi, ikiwemo kufyeka vichaka vilivyopo kandokando ya barabara ili kuondoa maficho ya wahalifu.
Amesema katika mtaa huo umeanzisha utaratibu wa kuwatambua wakazi wapya wanaofika eneo hilo kwa kuhakikisha kila mgeni anajitambulisha kwenye ofisi za serikali ya mtaa ili aweze kufahamika na shughuli anayoifanya.
“Japo hatuna ushahidi kamili ila tuna hofu kuwa baadhi ya wahalifu ni waliopata msamaha wa kifungo na sasa wanafanya matukio haya ili warudi gerezani,” amesema Lulandala.
Mkazi wa Ngalanga, Renifrida Batwel amesema matukio ya ubakaji wa watoto wadogo inawaathiri hata kisaikolojia na wakati mwingine kupelekea kufanya vibaya katika masomo.
“Adhabu kali ziendelee kutolewa kwa watu hawa kwani wanaweza kuwasababishia magonjwa na kuwaharibu kisaikolojia na hata kushindwa kusoma na kufaulu mitihani yao,” amesema Batwel.
Katika tukio jingine, Kamanda Banga amesema jeshi hilo limemkamata Soseth Mligo (32), dereva na mkazi wa Mgendela kwa kumgonga Wema Nziku (12), mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi Magufuli na kusababisha kifo chake, eneo la kivuko cha watembea kwa miguu.