Chunya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera ameagiza Serikali Wilaya ya Chunya kufunga king’amuzi na runinga kwenye wodi za wajawazito walio kwenye uangalizi na baada ya kujifungua katika Hosptali ya Wilaya.
Agizo hilo limekuja baada ya Mkuu wa Wilaya ya Chunya na Kamishna Mwandamizi wa Uhamiaji, Mbaraka Batenga kumueleza kuwepo kwa maboresho hususani kufunga Mifumo ya Kamera za Usalama (CCTV), kwa lengo la kufuatilia mienendo ya utoaji huduma.
Agizo hilo amelitoa leo Jumamosi Mei 24, 2025, katika ziara yake ya siku ya pili ya kukagua uboreshaji wa miundombinu ya majengo katika Hosptali ya Wilaya ya Chunya.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera, akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua ukarabati wa jengo la kinamama wajawazito. Picha na Hawa Mathias
Uboreshwaji huo umefadhiriwa na Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhudumia Watoto Duniani (Unicef), kwa gharama ya Sh946.3 milioni.
Dk Homera amesema Serikali inatambua mchango wa wadau katika sekta ya afya na uboreshwaji huo uhusishe kufungwa mifumo itakayo wasaidia kujua uwekezaji wa Serikali iliyopo madarakani.
“Awali nilitaka kutoa maelekezo ya kuboresha huduma kwa kununua king’amuzi na Tv na kuweke ulinzi wa kamera maeneo yote ili kufuatilia utendaji usio mzuri kwa watumishi,”amesema.
Dk Homera amesema Serikali itaendelea kuboresha huduma za afya sambamba na kuomba wajawazito kutunza miundombinu iliyoboreshwa na wadau.
Mbunge wa Lupa Masache amelishukuru Shirika la Unicef kwa kuunga mkono jitihada za serikali kuboresha huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya.
“Tunaomba Shirika hilo kuendelea kuunga mkono uboreshwaji wa miundombinu ya afya kwa kina mama wajawazito kabla na baada ya kujifungua,”amesema.

Mkuu wa Wilaya, Batenga amesema miundombinu hiyo itasaidia kupunguza changamoto kwa wajawazito kutembea umbali kufuata huduma.
“Kuna wajawazito wanaishi maeneo ya Kambikatoto, Lupa wanasafiri umbali mrefu kufuata huduma ya uzazi hali ambayo ni hatari kwao,”amesema.
Katika hatua nyingine ameomba Shirika la Unicef kuendelea kuboresha huduma za matibabu kwa njia za mawasiliano ya teknolojia za kisasa baina ya kituo na kituo.
Aidha katika hatua nyingine, ameomba Serikali kuwezesha ujenzi wa chuo cha wauguzi ili kupunguza tatizo la watumishi katika vituo vya afya.
“Tumetenga eneo lenye ukubwa wa hekari 35, ambalo tumeweka mikakati kujenga chuo cha wauguzi, lakini changamoto ni fedha,” amesema.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Charles Jockel amesema wamefanya ziara kukagua utekeleza wa miradi ya maendeleo na kuridhishwa.
“Tumeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, tunaelekea kipindi cha uchaguzi Mkuu Oktoba 2025,”amesema.
Mariam Maganga amesema wanaishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa wa huduma za afya za mama na mtoto tofauti na miaka ya nyumba tangu nchi ipate uhuru.
“Kimsingi huduma za afya za mama na mtoto zimeboreshwa hali ambayo utapunguza vifo vitokanavyo na uzazi, lakini awali tulikuwa tunalala kitanda kimoja watu wawili,” amesema.