Serikali ilivyopangua ‘dili’ utoroshaji almasi ya Sh1.7 bilioni usiku

Mwanza. ‘’Serikali ina mkono mrefu’’ Huo ndio usemi unaofaa kutumika kueleza jinsi Serikali inavyong’ámua na kudhibiti mbinu kutorosha madini nje ya nchi.

Usemi huo umetimia jijini Mwanza Mei 18, 2025 baada vyombo na taasisi za Serikali kumnasa raia wa kigeni ambaye jina lake halijajulikana akitorosha nje ya nchi madini ya almasi yenye thamani ya zaidi ya Sh1.7 bilioni kupitia Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Mwanza usiku wa Mei 23, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema mtu mmoja ambaye ni raia wa kigeni (hakumtaja jina) anashikiliwa kwa mahojiano na uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo.

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti ya wizara yake bungeni hivi karibuni, Waziri Mavunde alisema kati ya Julai 2024 hadi Machi 2025, Serikali imefanikiwa kukamata na kutaifisha madini ya aina mbalimbali yenye thamani ya Sh17.75 bilioni katika mikoa ya kimadini 12 baada ya wahusika kubainika kufanya shughuli zao kinyume cha sheria.

Miongoni mwa mikoa ambako madini  hayo yalikamatwa kwa mujibu wa Waziri Mavunde ni pamoja na Geita, Ruvuma, Kahama, Mwanza, Shinyanga, Kagera, Dar es Salaam, Manyara, Simiyu, Singida, Chunya, Arusha, na Lindi ambako watuhumiwa 75 walikamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Akizungumzia tukio la Mwanza, Waziri Mavunde amesema; “Uchunguzi wa kina unaendelea kubaini mtandao wa wote wanaohusika kuwezesha utoroshaji wa madini ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao ikiwemo kufikishwa mahakamani, kutaifisha madini yao na kuwafutia leseni,” amesema Mavunde

Waziri huyo amesema vitendo vya kutorosha madini siyo tu ni kosa la jinai, bali pia vinaikosesha Serikali mapato kupitia kodi na ushuru mbalimbali huku akiwaomba Watanzania kila mtu alipo kusaidiana na Serikali kwa kutoa taarifa za wanaojihusisha na vitendo hivyo vinavyohujumu uchumi wa nchi.

‘’Serikali imeboresha sekta ya biashara ya madini kwa kufungua masoko 43 na vituo 49 vya kuuza na kununua madini kote nchini; tumepunguza kodi na ushuru mbalimbali, hivyo hakuna sababu ya watu kutumia njia za panya kuuza na kununua madini,’’ amesema Mavunde

Kwa nia ya udhibiti, Wizara ya Madini imeunda kikosi kazi maalum kukabiliana na utoroshaji wa madini na tayari imefanyakazi eneo la Tunduru na sasa kiko eneo la Nyamongo kwa kazi ya usimamizi wa biashara ya madini.

‘’Udhibiti wa biashara ya madini umesaidia ongezeko la makusanyo ya mapato kupitia sekta hiyo kutoka zaidi ya Sh162 mwaka wa fedha wa 2015/16 hadi kufikia zaidi ya Sh753 bilioni kwa mwaka wa fedha wa 2023/24. Malengo yetu kwa mwaka 2024/25 ni kukusanya Sh1 triolini na hadi kufikia sasa tayari tumekusanya zaidi ya Sh925 bilioni,” amesema Mavunde

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Justine Nyari, mchimbaji na mfanyabiashara wa madini ya viyo ya Tanzanite ameishauri Serikali kuongeza usimamizi na udhibiti katika maeneo ya migodi, masoko na vituo vya kuuza na kununua madini na kutumia teknolojia katika ukaguzi maeneo ya mipakani, vituo vya usafiri wa umma vikiwemo viwanja vya ndege.

‘’Uaminifu, kufanya kazi kwa weledi na uzalendo ni miongoni mwa watumishi wa umma katika sekta ya madini na vyombo vya ulinzi na usalama ni eneo muhimu katika udhibiti wa vitendo vya kurosha madini nje ya nchi,’’ amesema Nyari.

Kiongozi huyo wa zamani wa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Mkoa wa Maranya (Marema), ameshauri zitungwe sheria zitakazotoa adhabu kali ikiwemo vifungo vya muda mrefu magereza kwa wote wanaobainika na kuthibitika kujihusisha na utoroshaji wa madini nje ya nchi.

‘’Serikali idhibiti wa uingiaji hole wa watu wasiohusika katika maeneo ya migodi, masoko na vituo vya kuuza na kununua madini ili kuondoa ushawishi usiofaa kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini,’’ amesema Nyari.

Katika ngazi ya Kimataifa, Nyari ameshauri Serikali kupitia vyombo na taasisi zake kujenga mfumo na utaratibu wa kushirikiana na mamlaka za Serikali za mataifa mengine kudhibiti biashara ya madini kuanzia ngazi ya kanda na Kimataifa.

‘’Pawepo utaratibu wa madini yote yanayouzwa nje ya nchi kuwa na vibali au vyeti maalum vinavyoonyesha imetoka nchi gani. Hii itazuia utoroshaji iwapo watumishi wa Serikali wanaohusika na utoaji wa vyeti na vibali hivyo watafanya kazi zao kwa weledi, uaminifu na uzalendo kwa Taifa,’’ ameshauri Nyari.

‘’Umma wa Tanzania, kuanzia wachimbaji na wafanyabiashara wa madini uelimishwe umuhimu wa kushirikiana na Serikali na vyombo vyake kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa madini vinahujumu uchumi wa Taifa,’’ amesema Saddiki Mneney, mchimbaji na mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite eneo la Mirerani wilayani Simanjiro.

Amesema wachimbaji na wafanyabiashara wa madini wanapaswa kujua athari za utoroshaji wa madini ikiwemo kushtakiwa na kufilisika kwa madini yao kutaifishwa pindi wanapothibitika kujihusisha na vitendo vya kutorosha madini.

Mneney anasema kwa sababu ni vigumu kujenga ukuta katika maeneo ya madini mengine kama ilivyofanyika Mirerani, ni vema Serikali iongeze matumizi ya teknolojia katika ukaguzi na kubaini madini katika maeneo na vituo vyote vya usafiri wa umma vikiwemo viwanja vya ndege, vituo vya mabasi na mipakani.

Related Posts