Geita. Mgodi wa dhahabu wa Mwamba uliopo katika Kijiji cha Buziba, Kata ya Nyarugusu, Wilaya ya Geita umetumia zaidi ya Sh200 milioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kijamii ikiwemo ya elimu na afya.
Utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya mpango wake wa kurejesha kwa jamii, faida ya rasilimali zinazochimbwa kwenye maeneo yao.
Mgodi huo pia umetoa ajira kwa vijana 150 wanaotoka kwenye kata ya Nyarugusu waliopata ajira za muda mrefu na mfupi, lengo likiwa ni kuhakikisha rasilimali ya madini inayopatikana kwenye eneo hilo inawanufaisha, pia, wazawa.
Akizungumza leo Mei 24, 2025 katika tamasha la michezo lililoandaliwa na kampuni hiyo, Meneja wa Mgodi huo, Calvin Nabil amesema mashindano hayo yamelenga si tu burudani, bali kuwa njia ya kuibua vipaji vya vijana na kuhamasisha maendeleo ya kijamii.
“Tumeamua kuhakikisha faida tunayopata inarudi kwa wananchi. Tumewekeza kwenye elimu, afya na sasa tunashirikiana na jamii kuwawezesha vijana kwa kuwapatia ujuzi na ajira badala ya kuishia kuzurura mitaani au kujihusisha na uchimbaji usio rasmi unaotumia kemikali hatarishi kama zebaki,” amesema Nabil.
Nabil ametaja miradi waliyoitekeleza kuwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na kutoa vifaa vya huduma ya afya kwa zahanati iliyopo kwenye kijiji hicho pamoja na ujenzi wa visima vya maji kwa ajili ya wakazi wa eneo hilo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano na Ushirikiano na Wadau wa kampuni hiyo, Evance Rubara amesema lengo ni kuhakikisha kuwa uchimbaji unawanufaisha wananchi wa maeneo husika moja kwa moja.
“Tumekuwa tukisikia malalamiko ya vijana kukosa ajira na wengine kuingia katika uchimbaji wa kienyeji ambao sio rafiki kwa afya, sasa tunataka kila kazi iwe fursa kwa vijana wa hapa,” amesema Rubara.
Amesema katika kuibua vipaji kampuni hiyo inashirikiana na wataalamu mbalimbali kutoa mafunzo kwa vijana, lengo likiwa kuwaunganisha na taasisi au timu za kitaalamu ili kukuza vipaji vyao.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nyarugusu, Lusekelo Mwaikenda amesema hatua ya mgodi huo kuwekeza kwenye vipaji vya michezo ni njia mpya ya kuwasaidia vijana kupata ajira nje ya sekta ya uchimbaji.
“Mara nyingi tumekuwa tukiona watoto wakimaliza shule wanazurura mitaani, wengine wanaingia kwenye kamari au migodini, lakini programu hii inawashirikisha, inawaibua na kuwajengea mwelekeo mpya wa maisha,” amesema Mwaikenda.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Buziba, Ntobi James amesema uwepo wa mgodi huo umewapunguzia wananchi michango inayotozwa kwa kwenye sekta ya elimu kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na madawati.
“Tunajivunia kupata wawekezaji, mgodi huu umetusaidia hali ilikua mbaya hasa kwenye elimu lakini sada wametujengea shule, wamesaidia watoto wa mazingira magumu kurudi shule lakini pia wametuchimbia visima vya maji, sasa hivi tuna uhakika wa maji safi na salama na vijana wetu wameajiriwa wameacha kuwa wazururaji,” amesema James.
Kata ya Nyarugusu ina shule 14 ambapo shule za msingi na sekondari zina jumla ya wanafunzi 17,000.