Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche amesema Kikao cha kamati kuu kilichokutana Jumamosi ya Juni 23, 2025 kimeridhia kwa kauli moja kutokuijibu barua ya msajili wa vyama vya siasa.
Barua hiyo ya msajili aliituma kwa Chadema akielezea uamuzi wake wa kukitaka chama hicho kuitisha upya Baraza Kuu ili kuwaidhinisha viongozi wanane waliokuwa wameteuliwa na mwenyekiti wake, Tundu Lissu Januari 22, 2025. Msajili amesema Akidi haikuwa imetimia ya kuwaidhinisha.
Leo Jumapili, Machi 25, 2025, Heche akitoa maazimio ya kamati kuu katika kongamano la wasomi wa Vyuo na Vyuo Vikuu Mkoa wa Dar es Salaam (Chaso) makao makuu ya Chadema, Mikocheni amesema kamati kuu imejadili suala hilo kwa kina.
“Kamati kuu imejiridhisha msajili wa vyama vya siasa amekwenda kinyume na sheria ya vyama vya siasa kwa sababu hana mamlaka ya kupokea, kusikiliza na kufanyia uamuzi malalamiko ya mwanachama wa chama cha siasa na kamati kuu imesema, ni batili na haitafanyia kazi na huu ndio msimamo wa chama,” amesema Heche.
Katika hilo amedai: “Msajili amejigeuza kamati ya rufaa ya chama chetu, sheria anayoitumia haimpi hayo mamlaka, Katiba ya nchi haimpi mamlaka na kama kuna mwanachama analalamika vipo vyombo ndani ya chama vinavyoweza kushughulikia.”
Viongozi wanaolalamikiwa na msajili kuamua kuwaweka kando hadi Baraza kuu jingine liitishwe ni Katibu Mkuu, John Mnyika, Amani Golugwa (Naibu Katibu Mkuu – Bara) na Ally Ibrahim Juma (Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar).
Wengine ni wajumbe wa kamati huu Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh pamoja na Dk Rugemeleza Nshala, ambaye aliteuliwa kuwa mwanasheria mkuu wa chama hicho.
Mzizi wa yote hayo ni barua ya malalamiko iliyowasilishwa na aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Lembrus Mchome akisema chama hicho kimekiuka katiba yake katika mchakato wa uthibitishwaji wa wajumbe hao.
Hadi Mchome anafikisha barua hiyo kwa Msajili alikiandikia chama chake na kabla ya kujibiwa aliwasilisha malalamiko hayo katika Ofisi ya Msajili.
Mchome alikuwa akilalamikia kwamba akidi ya Baraza Kuu haikutimia wakati wa kuwathibitisha viongozi hao.