Arusha. Familia ya Mchungaji wa Kanisa la Huduma ya Kristo lililopo Mtaa wa FFU, Kata ya Muriet mkoani Arusha, Steven Jacob, aliyekuwa ametekwa na watu wasiojulikana na baadaye kuokolewa na walinzi wa mashamba ya ngano mkoani Kilimanjaro, imesema inamuachia Mungu kwa kile kilichotokea kwa ndugu yao.
Mchungaji Steven alitekwa na watu wasiojulikana alipotoka nyumbani kwake asubuhi ya Mei 16, 2025 kisha kupatikana Mei 17, 2025 katika eneo la West Kilimanjaro wilayani Siha, Mkoa wa Kilimanjaro.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Mei 25,2025 baba mzazi wa mchungaji huyo ambaye pia ni mchungaji na balozi wa nyumba 10 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jacob Gumbo amesema wamemuachia Mungu suala hilo na wanaendelea kumuuguza ndugu yao.
“Polisi walishakuja tangu ile siku alipopatikana wakachukua maelezo ila baada ya pale hatujapata mrejesho wowote. Hakuna hatua nyingine yoyote tuliyochukua sisi tumemuachia Mungu na tunaendelea kumuuguza ndugu yetu hapa nyumbani,”amesema.
Alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia suala hilo Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, simu yake iliita bila kupokelewa.
Awali Mei 17,2025 Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude amesema tukio hilo linafanyiwa upelelezi wa kina kujua undani wake na chanzo chake.
“Tumeshaanza uchunguzi wa tukio la kijana kuchukuliwa na hao watu na tayari tuko hatua nzuri tutawajulisha kinachoendelea,”alisema Mkude
Awali akisimulia tukio hilo Mchungaji Steven alidai watu hao waliomteka walijitambulisha kwake kuwa maofisa wa polisi, lakini hawakumuonyesha vitambulisho wakidai wanampeleka kituo kikuu cha polisi.
Alisema kutokana na namna walivyomchukua alielewa ametekwa, kwani hawakuwa na vitambulisho na hawakutaka aage mtu, badala yake walimchukua na kumfunga vitambaa viwili usoni na pingu mkononi, ndipo alipopiga kelele kuwa anatekwa, kisha watu hao wakamrusha kwenye gari na kuondoka naye kwa kasi.
Mchungaji huyo alidai waliomteka walimpeleka hadi eneo hilo la West Kilimanjaro ambako walichukua simu zake za mkononi na kumtaka afute picha mjongeo (video) alizokuwa amepandisha kwenye mtandao wa Youtube.
“Naomba nisiongee mengi kwa sababu ni ishu za mtandao niliposti Youtube. Baada ya kunipiga na kuchukua baadhi ya maelezo ambayo nafikiri nisingependa kuyaongea, baada ya pale nikasikia kama wananipeleka mahabusu ila haikuwa hivyo, wakanipeleka porini West Kilimanjaro.
“Walivyotaka nifute kwa bahati mbaya bando lilikuwa limeisha, ikabidi wafanye mpango wapate bando, wakasema wawili au mmoja abaki na mimi halafu wengine wakatafute bando ili vifute video,”amesema mchungaji.
Mchungaji huyo amesema watu hao walimwambia alale chini wakamkanyaga shingoni, mmoja akawaambia wenzake wanamuachaje hapo. Alisema mambo mengine hawezi kuzungumza zaidi ila walimuacha wakaondoka na simu yake.
“Walivyoondoka nikaanza kubiringita na kutembea kwa magoti hadi barabarani, nilipofika akatokea mwendesha bodaboda, alivyoona ile hali akapita, lori la mafuta nalo likaogopa.
“Wakaja watu wanaolinda tembo wasiingie kwenye mashamba, nikajitambulisha mimi ni mtumishi wa mtandaoni nimetekwa nimetupwa huku nisaidieni, mmoja wao alikuwa mwoga kesi isije kuhamia kwao, ila wakanisaidia. Nikaomba simu ili niwajulishe watu niko hai,”amesema.
Mchungaji huyo alisimulia: “Walinipeleka kwenye kambi yao na baadaye wakaniambia watu wale wamerudi kule kama wananitafuta, wakafanya mpango nikatolewa nikaenda sehemu nyingine, naomba mengine nisongee.”
Jumapili iliyopita Mei 18,2025 ibada kanisani hapo iliongozwa na Mchungaji Vulfrida George akisaidiana na Mchungaji Gumbo ambapo waumini wa kanisa hilo kutoka matawi mbalimbali nchini walieleza namna walivyokimbilia kanisani kuomba kwa saa kadhaa ili kiongozi wao arejee salama.
Waumini hao walisema hawakuwa na namna yoyote wala hawakujua nini kingine wanaweza kufanya zaidi ya kukimbilia kanisani kumuomba Mungu.
Kumekuwa na kilio kuhusu utekaji nchini, tukio la hivi karibuni likiwa la kutekwa mwanaharakati na kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mdude Nyagali tangu Mei 2,2025 alipovamiwa na kushambuliwa nyumbani kwake ambapo hadi sasa hajulikani alipo.