Chunya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Chunya kutoa Sh20 milioni zikamilishe Ujenzi wa shule ya mpya ya Sekondari Masache iliyopo Kitongoji cha Itumbi Kata ya Matundasi.
Hatua hiyo imekuja kutokana na kilio cha diwani wa kata hiyo, Kimo Choga alichokitoa leo Jumapili Mei 25,2025 baada ya kumueleza Dk Homera changamoto ya wanafunzi wanao chaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kutembea umbali wa kilomita 13 kufuata elimu katika Shule ya Sekondari ya Makala
“Mkuu wa Mkoa, kwanza nikushukuru kwa ujio wako tuna matumaini utasema neno, kitongoji hiki tangu nchi ipate uhuru hakina shule ya sekondari, wanafunzi wakimaliza elimu ya msingi hulazimika kusafiri au kutembea kilomita 13 kusaka elimu,” amesema diwani huyo.
Amesema hali hiyo imekuwa changamoto hususan kwa wanafunzi wa kike kushindwa kutimiza ndoto zao kwa kukutana na adha mbalimbali vikiwamo vishawishi.
Kimo amesema mradi umefikia hatua ya kupaua, lakini kesho Jumatatu Mei 26,2025, tunatarajia mafundi wanaingia kuendelea na kazi.
Amesema endapo ujenzi huo ukikamilika utakuwa mwarobaini kwa wanafunzi kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata elimu.
“Mradi huu unapaswa kumamilika kwa wakati kabla ya kuanza msimu wa mvua Desemba, lengo ni kuepuka kukimbizana na mafundi,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera akimsikiliza mmoja wa wakazi wa Itumbi akiwalisha kero yake kwenye mkutano wa hadhara Picha na Hawa Mathias
Mkazi wa Itumbi, Sakina Mwakyusa amesema ukosefu wa sekondari kuna wakati wazazi wanapata hofu watoto wanapochelewa kurejea majumbani nyakati za usiku.
Kufuatia kero hizo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Homera ameagiza halmashauri ya Wilaya ya Chunya kuharakisha kutenga Sh20 milioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi ili wanafunzi watakao chaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwakani waanze masomo.
“Halmashauri kamilisheni haraka Shule ya Sekondari Masache, Pia shirikisheni wadau ili ifikapo Januari 2026, ianze kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza jambo ambalo litawaondoa na adha ya kusafiri au kutembea umbali mrefu kufuata elimu,” amesema.
Amesema taarifa ya awali imeeleza kuwa mfuko wa jimbo umechangia Sh15 milioni kwenye ujenzi, lakini pia halmashauri mkiongeza Sh20 milioni mradi huo utapiga hatua.
“Lakini pia tupieni jicho ujenzi wa shule shikizi na kuajiri walimu ili kusaidia kundi la watoto kupata elimu na kunufaika na uwekezaji wa Serikali,” amesema.
Hata hivyo, Homera ameshtushwa katika Kitongoji hicho kuwa na idadi kubwa ya watoto wadogo na kuwashauri wanaume kutumia muda mwingi kwenye shughuli za kiuchumi, badala ya kukaa na wenza wao ili kuweka mipango mizuri ya makuzi ya familia.
Kauli hiyo ya mkuu wa mkoa, iliungwa mkono na Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbaraka Batenga aliyesema ongezeko la watu katika kitongoji hicho ni ya kasi kubwa hali inayochochea Shule ya Msingi Itumbi kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi.
“Mkuu hili eneo watu wanazaliana mpaka Shule ya Msingi Itumbi imezidiwa na idadi kubwa ya wanafunzi, mpaka sasa wako wanafunzi 2,000, Serikali tunasaka eneo lingine la kujenga shule ili kupunguza msongamano,” amesema.
Awali, akizungumza na wananchi Mbunge wa Lupa, Masache Kasaka amesema hayo ni matunda ya Serikali ya awamu ya sita katika kuleta maendeleo.
“Ndugu zangu hayo ndio mliyonituma kuwawakilisha kulikuwa na changamoto ya barabara kutoka Matundasi kuja Itumbi tayari Serikali ilitoa Sh400 milioni, lakini pia tunaona vipo vituo vya afya zahanati, miradi ya maji sambamba na kupanda kwa soko la bei ya tumbaku na dhahabu,” amesema.