Kweleakwelea waliovamia mashamba ya mpunga Kilombero,   wadhibitiwa

Kilombero. Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viatilifu (TPHPA) kwa kushirikiana na Shirika la kudhibiti nzige wa jangwani, wamefanikiwa kuwadhibiti ndege aina ya Kweleakwelea waliovamia mashamba ya mpunga yaliyopo kwenye bonde la Mto Kilombero mkoani Morogoro.

Kudhibitiwa kwa ndege hao kumesaidia kuokoa zaidi ya hekari 700 za mpunga zilizokuwa hatarini kuteketezwa.

Akizungumza wakati wa kufanya tathimini ya kazi ya kuwadhibiti ndege hao kwa kutumia ndege ndogo iliyopuliza dawa kwenye mashamba hayo, Kaimu Mkurugenzi wa TPHPA kanda ya mashariki, Dk Mahmoud Sasamalo amesema baada ya kupata taarifa kutoka kwa wakulima na viongozi wa wilaya Mei 22, walifika kwenye bonde hilo na kuanza kazi ya kuwadhibiti.

Dk Sasamalo amesema hali waliyoikuta kwenye mashamba hayo ilikuwa mbaya kwa kuwa makundi makubwa ya Kweleakwelea yalikuwa yametanda angani na tayari walikuwa wameshajenga viota kwenye mashamba ya miwa yaliyopo kwenye bonde hilo.

Amesema mbali na kuwadhibiti ndege hao, mamlaka hiyo pia imechukua hatua za kutafuta na kuharibu mazalia na makazi ya ndege hao.

“Tumefanikiwa kuteketeza karibu viota vyote, na kwa sasa hali ni shwari, wakulima wanaendelea na shughuli zao nyingine tofauti na awali, ambapo walilazimika kutumia muda mwingi shambani kulinda mpunga,” amesema Dk Sasamalo.

Aidha, amebainisha kuwa Serikali kupitia TPHPA inaendelea kuweka mikakati ya kusaidia wakulima kukabiliana na changamoto kama hizo, ili kuhakikisha Taifa linakuwa na utoshelevu wa chakula na ziada ya kuuza nje ya nchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Yuda Mgeni amesema ni mara ya kwanza kwa ndege hao kuvamia kwenye bonde hilo, jambo linalochangiwa na mabadiliko ya tabianchi yaliyowafanya ndege hao kuanza kuhama.

“Kwa kuwa ndege hawa wameonyesha tabia ya kuhamahama, ninatoa tahadhari kwa wakulima wa bonde hili kuhakikisha wanatoa taarifa kwa maofisa ugani pindi wanapowaona kwenye maeneo yao,” amesisitiza Mgeni.

Wakulima wa kata za Sanje na Kidatu waliopo katika bonde hilo wameeleza namna ndege hao walivyoingia na kuhatarisha mashamba yao, pamoja na juhudi walizokuwa wakichukua kunusuru mazao yao, kabla ya timu ya TPHPA kufika na kupuliza dawa ya kudhibiti hali hiyo.

Moja ya mashamba ya mpunga katika kata ya Sanje na Kidatu kwenye bonde la Kilombero yaliyovamiwa na ndege aina ya Kweleakwelea mapema mwezi Mei mwaka huu, hata hivyo mamlaka ya afya ya mimea na viuatilifu TPHPA iliweza kuwadhibiti haraka ndege hao kwa kuwapulizia dawa kwa kutumia ndege ndogo (Helkopta). Picha Hamida Shariff.

Shomari Ngonji, mkulima kutoka Kijiji cha Miwangani, kata ya Sanje, amesema tangu ndege hao waingie mapema Mei, amekuwa akiamka alfajiri na kwenda shambani kulinda mashamba, huku muda mwingi akiwa shambani akiwafukuza ndege hao hadi anakosa hata muda wa kula.

“Nafika shambani alfajiri, nakuta tayari wameshatua, nawafukuza mpaka saa mbili usiku, nakosa hata muda wa kula wala kwenda kujisaidia; nikifukuza kundi moja, linakuja jingine. Ni kazi hadi usiku narudi nyumbani,” amesema Ngonji.

Amesema kuna siku alikuwa anapelekewa chakula shambani, kundi kubwa la ndege lilishuka ghafla.

“Nilichanganyikiwa nikarusha tonge la ugali kwa ndege, huku nikitia jiwe mdomoni. Ndege walikuwa wamejaa angani kiasi kwamba jua halikuonekana.”

Amina Mbecha, mkulima kutoka kijiji hicho, amesema kuwa kutokana na shinikizo la kulinda mashamba, yeye na wanawake wenzake walilazimika kuwa mashambani kuanzia asubuhi hadi usiku, huku wakiwaacha watoto nyumbani bila uangalizi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Miwangani, Kata ya Sanje, Ibrahim Moyo amesema zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wa kijiji hicho ni wakulima wa mpunga na miwa.

Amebainisha kuwa kama ndege hao wangeteketeza mashamba, wakulima wengi wangeingia kwenye hasara kubwa.

Ameishukuru Serikali kwa hatua ya haraka waliyochukua, ambayo ilisaidia kuokoa mashamba ya mpunga yaliyokuwa hatarini kuangamia kutokana na uvamizi wa ndege hao.

Related Posts