Machungu ya wanawake wanaozaa na wanaume tofauti

Dar es Salaam. Baadhi ya wanawake waliozaa na wanaume tofauti wanakumbana na changamoto za kijamii, kifamilia na kihisia. Wanahisi kutengwa na kulazimika kubeba mzigo wa malezi peke yao huku wakihukumiwa na jamii.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, baadhi ya wanawake wamefunguka kuhusu maisha yao ya kila siku, wakisema jamii imekuwa ikiwahukumu kwa mtazamo wa juu juu, bila kuelewa sababu zilizosababisha wao kuzaa na wanaume tofauti.

Wanawake hao wanaeleza jinsi wanavyopata changamoto ya msongo wa mawazo, kutengwa na kudharauliwa na baadhi ya watu.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, baadhi ya wanawake wamefunguka kuhusu maisha yao ya kila siku, wakisema jamii imekuwa ikiwahukumu kwa mtazamo wa juu juu, bila kuelewa sababu zilizosababisha wao kuzaa  na wanaume tofauti.

Mkazi wa Mbagala, Amina (jina lake halisi limehifadhiwa) alizaliwa na kulelewa Morogoro, lakini maisha yalimpeleka Dar es Salaam akiwa na matumaini ya kupata maisha bora.

 Alijikuta akiwa mama wa watoto wawili kutoka kwa wanaume wawili tofauti na tangu hapo, kila hatua ya maisha yake imekuwa vita mpya.

“Nilimpenda wa kwanza, tukawa pamoja miaka mitatu. Nilipopata ujauzito alinitosa. Nilihangaika kulea mtoto mwenyewe,” anasimulia Amina kwa sauti ya majonzi.

Miaka miwili baadaye, alikutana na mwanaume mwingine aliyemuahidi ndoa…“Nilidhani nimepata mtu wa kweli. Lakini baada ya mtoto kuzaliwa, alibadilika ghafla,” anasema Amina anayedai kwa yaliyomkuta hawezi tena kuingia kwenye uhusiano.

“Wanaume wakijua nina watoto wawili wa wanaume tofauti, wananikimbia. Wanadhani mimi ni tatizo. Hata ndugu hawanielewi,’’ anaeleza.

Rehema Ally (29) mkazi wa Gongo la Mboto, ana watoto wawili wa baba tofauti. Anasema hakuwahi kufikiria kuwa maisha yake yangekuwa ya aina hiyo, lakini alijikuta akifanya uamuzi kutokana na shinikizo la maisha na matumaini ya kupata hifadhi ya ndoa.

“Baada ya kuachwa na baba wa kwanza wa mwanangu, niliendelea na maisha. Nilipokutana na wa pili, nilitamani tu mtoto wangu awe na kaka wa damu, mwenye baba wa kumtambua. Sikujua naye atanitenda,” anasema Rehema.

Amesema kwa sasa analazimika kufanya kazi mbili tofauti kuuza maandazi asubuhi na kuuza mitumba jioni ili kuwahudumia watoto wake.

Kwa upande wake Zuena Kauzeni, mkazi wa Mabibo anasema amesusiwa watoto wawili wa   wa kiume wa baba tofauti,  huku akizidiwa na majukumu ya kuwalea watoto hao na kuamua kuwapelekea kwa babu yao mkoani wa Tabora.

“Nilizalishwa nyumbani Tabora na wanaume wawili lakini baadaye wakanisusia kwenye upande wa malezi ndipo nikaamua kuja Dar es Salaam, kutafuta maisha ili niweze kuwalea watoto wangu, lakini kwa sasa wapo kwa wazazi wangu mkoani Tabora,” anasema Zuena.

Anasema chanzo cha kususiwa watoto ni baba wa watoto kuwataka watoto wakiwa  bado wadogo sana naye akakataa. Zuena kwa sasa anafanya kazi kwenye kiwanda kimoja  jijini Dar es Salaam.

Mtaalamu wa saikolojia ya famlia kutoka Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Dk Joyce Nyoni, anasema hali ya mwanamke kulea watoto wa wanaume tofauti,  mara nyingi huambatana na msongo wa mawazo unaotokana na lawama, kukataliwa na mzigo wa kiuchumi.

“Jamii ina tabia ya kumhukumu mwanamke bila kujua mazingira yaliyosababisha hali hiyo. Hii huathiri uwezo wake wa kujenga uhusiano mpya au hata kulea watoto kwa utulivu wa kiakili,” anasema Dk Joyce.

Kwa upande wake, Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Njombe, Subilaga Mwaigwisya, anasema changamoto nyingi zinazowakumba wanawake hawa zinatokana na ukosefu wa msaada kutoka kwa baba wa watoto na uelewa mdogo wa haki zao.

“Wanawake wengi hawaelewi kuwa wanaweza kufungua kesi mahakamani kudai matunzo ya watoto. Lakini pia kuna hofu ya kufedheheshwa au kushindwa kuwasiliana na baba wa mtoto,” anasema Subilaga.

Mwanasheria aliyebobea katika masuala ya haki za familia, Felix Luhanga, anashauri wanawake kutafuta msaada wa kisheria ili kuwalazimisha wazazi wenza kushiriki katika malezi ya watoto.

“Kulingana na Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, mtoto ana haki ya kutunzwa na mzazi yeyote bila kujali hali ya uhusiano. Mwanamke hana sababu ya kubeba mzigo huu peke yake,” anasema Luhanga.

Related Posts