Osaka. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ushirikiano wa Tanzania na Japan umezidi kuimarika siku ha siku katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kidiplomasia ambapo mauzo ya biashara kati ya nchi hizo yameongezeka kutoka dola za Marekani bilioni saba mwaka 2023 hadi bilioni 37 kwa mwaka 2024.
Majaliwa ameyasema hayo leo Jumapili, Mei 25, 2025 alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho ya Siku ya Tanzania kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Osaka (World Expo Osaka 2025) yanayoendelea nchini Japan.
Amesema Wajapan wanapenda sana bidhaa kutoka Tanzania zikiwemo za kilimo kama chai, kahawa, ufuta, tumbaku, tingatinga, vinyago, katani, viungo ikiwamo karafuu na madini mbalimbali yanayopatikana nchini.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan na duniani kote waje kuwekeza katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo ya elimu, afya, miundombinu, nishati, kilimo, utalii kwani Tanzania imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji na pia ina amani na utulivu.

“…Tanzania licha ya kuwa na fursa nyingi za uwekezaji ikiwemo ardhi yenye rutuba, amani na mazingira tulivu, pia ni kitovu cha biashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki, Kusini na Kati kwa kuwa inapakana na nchi saba ambazo ni Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Zambia, Malawi na Msumbiji hivyo kuwawezesha wawekezaji kupata masoko ya uhakika katika mataifa hayo.”
Waziri Mkuu amesema Serikali ipo katika mchakato wa kuvifanyia maboresho viwanja vya Maonyesho vya Mwalimu Julius Nyerere, maarufu sabasaba ili viwe na hadhi ya kimataifa na kuwezesha kufanyika mikutano na maonyesho ya biashara ya kikanda na kimataifa.

Maonyesho hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Maonyesho hayo yalianza tangu Aprili 13, 2025 na yanatarajia kumalizika Oktoba 13, 2025, hii ni mara ya pili kwa Japan (Osaka) kuwa mwenyeji wa maonyesho hayo ya kimataifa, ambapo mara ya mwisho yalifanyika 1970 (EXPO 1970).
Kesho Jumatatu, Mei 26, 2026, Majaliwa anatarajiwa kushiriki katika kongamano la biashara, uwekezaji na utalii ambalo litahusisha wafanyabiashara kutoka Tanzania na Japan. Pia, Waziri Mkuu atashiriki katika mikutano ya uwili na viongozi wa Serikali ya Japan, mashirika ya maendeleo na watendaji wakuu wa kampuni mbalimbali kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Japan.