Mtifuano mabasi ya Ngorika, wanafamilia wazidi kuvutana

Moshi. Ngorika hakujapoa, ni kauli unayoweza kuitumia kuelezea kinachoendelea kwenye umiliki wa mabasi ya Ngorika, baada ya mmoja wa wanafamilia ambaye ni Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya Ally Mberesero Foundation, Charles Mberesero kudai mabasi mawili yamekatwakatwa na kuuzwa kama chuma chakavu.

Hata hivyo, leo Jumapili Mei 25, 2025, Mwananchi ilipomtafuta aliyekuwa meneja wa kampuni hiyo, Kapesa Mberesero kuhusu kuhamishwa na kukatwakatwa kwa mabasi hayo, alidai taarifa hizo sio za kweli na kwamba, mabasi hayo yapo eneo la Kisangara Wilaya ya Mwanga.

“Hakuna basi la Ngorika limehamishwa wala ‘kuchinjwa’  (kukatwakatwa)  yapo kwenye eneo la maegesho Kisangara,” amesema Kapesa ambaye alikuwa mjibu maombi katika kesi ya madai namba mbili ya mwaka 2022 kati ya kampuni ya Ngorika dhidi yake.

Baadhi ya mabasi ya Ngorika yakiwa yameegeshwa nyumbani kwa mmoja wa wanafamilia katika eneo la Soweto Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro.

Katika madai yake, kampuni hiyo iliomba mahakama imwamuru Kapesa kukabidhi mabasi 10 ya kampuni hiyo, eneo la maegesho iliyopo Moshi, gari aina ya Toyota Landcruiser, pikipiki na mali mengine yakiwa katika hali nzuri.

Kama hilo lisingewezekana, basi kampuni iliomba mahakama imlazimishe Kapesa, kulipa Sh1.27 bilioni ambayo ni sawa na thamani ya mali hizo na kuwasilisha faida halisi iliyotokana na biashara ya mabasi kati ya Desemba 2015 hadi Januari 2022.

Mbali na amri hizo, lakini kampuni hiyo ilikuwa inaiomba mahakama imuamuru pia mdaiwa huyo kulipa Sh750 milioni kama faida iliyotokana na biashara ya mabasi hayo ambayo haikuwasilishwa kwenye kampuni na fidia ya Sh500 milioni.

Katika hukumu yake aliyoitoa Machi 24, 2025, Jaji Safina Simfukwe wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, aliitupilia mbali kesi hiyo ya madai dhidi ya Kapesa.

Kuhusu hoja kuwa kama mdai alikuwa anashikilia mali zote za kampuni hiyo, Jaji alisema Mahakama haiwezi kuamua hoja hiyo kwa kuwa tayari ilishaamuliwa na Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara katika hukumu yake ya mwaka 2019.

“Hata malalamiko kuwa mdaiwa alikusanya mtaji ili kuanzia kampuni ya mabasi ya Kaprikon ni kama imepotea njia, kwa sababu mdai mwenyewe alishindwa kuthibitisha kama mdaiwa anashikilia mali za mdai wa shauri hili,”alisema Jaji huyo.

Hata hivyo, baada ya hukumu hiyo na wamiliki wa kampuni hiyo wakiwa katika mchakato wa kukata rufaa, mwanafamilia Mberesero anadai mabasi mawili yamekatwakatwa na kuuzwa kama chuma chakavu.

Mberesero anadai mabasi hayo yalitakiwa kuwepo eneo la maegesho Kisangara, wilayani Mwanga lakini hayakupelekwa huko na badala yake, yamehifadhiwa nyumbani kwa mmoja wa wanafamilia hiyo eneo la Soweto Manispaa ya Moshi.

Akizungumza leo, Mberesero amedai kuwa mabasi mawili kati ya 10 ya kampuni hiyo hayajulikani yalipo na taarifa walizonazo kama wana familia ni kwamba mabasi hayo mawili yaliyokuwa yameegeshwa pembeni ya barabara ua Boma yamekatwa na kuuzwa kama chuma chakavu.

“Sasa hivi tuko katika mchakato wa kukata rufaa. Kwa hiyo kama mabasi yanakatwa ni sawa na kupoteza ushahidi, hivyo tunaomba vyombo vya dola viangalie hilo, kwa sababu mabasi haya yapo hadharani na yanaonekana na huyo anayesema hayajasogezwa sio kweli,”amesema mwanafamilia huyo.

“Hayo mabasi yalipaswa kukaa Kisangara wilaya ya Mwanga lakini huyo ndugu yetu mmoja aliondoka nayo hakurudisha Kisangara kama Mahakama ya biashara ilivyoamuru. Zipo taarifa mabasi mawili yamechinjwa na kuuzwa scraper.”

“Kama siku tatu, nne baada ya hukumu yale mabasi mawili yaliyokuwa pale nje ya maegesho ya Capricorn ambapo zamani ilikuwa Ngorika nilipata taarifa kwamba yameanza kukatwa, hatujui ni nani anayeyakata ndio maana tunaomba vyombo vya dola viangalie hilo kwa sababu sisi hatujui,” amesema Mberesero.

Related Posts