Njia kusafirisha umeme Ipole-Inyonga yawashwa, walima mpunga kicheko

Katavi. Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO), imekamilisha ujenzi wa laini mpya ya umeme ya kilovolti 132 kutoka Ipole, Wilayani Sikonge, Mkoa wa Tabora hadi Inyonga Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi.

Laini hiyo yenye urefu wa kilomita 133 iliyowashwa, ni hatua muhimu ya kuunganisha Mkoa wa Katavi katika Gridi ya Taifa kwa mara ya kwanza.

Akizungumza wakati wa kuwasha laini hiyo katika kituo cha kupoza umeme cha Inyonga Mkoani Katavi leo Jumapili Mei 25, 2025, Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, Sadock Mugendi amesema ujenzi umekamilika kwa asilimia 100, huku  akiishukuru Serikali na Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa kuiamini kampuni hiyo kutekeleza mradi huo wa kimkakati.

Mhandisi wa Mradi kutoka Tanesco, Dalali Lunyamila amesema kituo cha Inyonga kina uwezo wa kupokea megawati 12, na mahitaji ya sasa ya Wilaya ya Mlele ni megawati nne, hivyo kufanya uwepo wa umeme wa ziada wa megawati nane ya matumizi ya sasa na baadaye.

Mhandisi Lunyamila amesema

wananchi wa Wilaya ya Mlele na  Majimoto wanatarajiwa kupata huduma ya umeme wa uhakika kupitia gridi ya Taifa kwa mara ya kwanza na kusaidia kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wakazi wa maeneo hayo.

“Wakazi wa maeneo haya sasa watakuwa na uhakika wa kupata umeme tofauti na awali, niwahimize tu kuendelea kufanya shughuli zao za maendeleo kwa kasi zaidi,” amesema Linyamila.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa ETDCO, Mhandisi Dismas Massawe akizungumza baada ya kuwashwa kwa njia hiyo amesema laini hiyo itakuwa kwenye kipindi cha matazamio kwa saa 48 kabla ya kuanza kutumika rasmi.

Akizungumzia mkoa wa Katavi kuunganishwa na gridi ya Taifa, mkulima wa mpunga kutoka eneo maarufu kwa kilimo hicho la Majimoto, Paul Mwasha amesema sasa wakulima na wafanyabiashara wa mchele watapata ahueni kubwa.

“Ilikuwa ukipeleka magunia ya mpunga mashine kukoboa, unaanza kuwaza umeme, lakini sasa tutapeta,” amesema.

Mwasha amesema kuna nyakati walikuwa wakiingia hasara kwa kulipa gharama ya kusubiri hasa kwa magari wanayoyakodi kusafirisha zao hilo kwenda sokoni kutokea mashine za kukoboa mpunga.

“Kama dereva alipanga kuja kupakia na kuondoka, anakuta sijamaliza kukoboa kwa sababu ya shida ya umeme, na kule sokoni nako mtu akiagiza mzigo ukimcheleweshea inakula kwako, sasa safi na tunaomba iendelee kuwa safi hivi hivi,” amesema Sophia Mwazembe mkulima wa mpunga.

Related Posts