Katika dunia ya sasa inayobadilika kwa kasi kubwa kutokana na maendeleo ya kiteknolojia, kijamii na kiuchumi, familia nyingi zimejikuta katika changamoto ya kutafuta usawa kati ya kazi na majukumu ya kifamilia.
Mojawapo ya changamoto kubwa zinazowakumba wazazi wa kizazi hiki ni malezi ya watoto, hasa katika kipindi cha awali cha maisha yao ambacho ni nyeti na cha msingi kwa ukuaji wao.
Katika kukabiliana na hali hii, vituo vya kulelea watoto ndiyo imekuwa suluhisho muhimu na vinaonekana kuwa na msaada mkubwa kuhakikisha ulinzi na usalama wa mtoto wenye umri kati ya miaka miwili na minne.
Miongoni mwa mambo yanayopewa mkazo kwenye Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM), ni uwepo wa vituo vya kulelea watoto mchana, hata hivyo si maeneo mengi ambayo yana vituo hivi.

Katika halmashauri ya Kilwa kuna vituo 21 vya kulelea watoto mchana ambavo kwa mujibu wa Ofisa ustawi wa jamii wa wilaya hiyo Charity Ngezi, vituo hivi vina mchango mkubwa si tu kwa familia bali pia kwa jamii na Taifa kwa jumla.
Anasema katika kipindi hiki ambacho wazazi wanahangaika na shughuli za kuwaingizia vipato kukiwa na wimbi kubwa la matukio ya ukatili dhidi ya watoto, vituo hivyo ni msaada mkubwa katika kuhakikisha ulinzi na usalama wa watoto na kuwajengea msingi mzuri wa hatua za awali za ukuaji.
“Vituo ya kulelea watoto vinatoa msaada mkubwa kwa wazazi wanaofanya shughuli mbalimbali za kuwaingizia kipato, huku kwetu pia kuna uvuvi, kilimo, biashara na hata wengine watumishi wa umma hivyo muda mrefu wanakuwa kwenye shughuli zao na watoto wanakUwa chini ya uangalizi wa watu wengine.
“Kutokana na hali hiyo, kuwa na sehemu salama na ya kuaminika ya kuwaacha watoto wakati wazazi wakienda kazini ni jambo la msingi. Vituo hivi huwapa wazazi utulivu wa akili na nafasi ya kufanya kazi zao bila wasiwasi mkubwa kuhusu usalama na ustawi wa watoto wao,”anasema Charity
Mtaalamu huyo wa ustawi wa jamii anasema mbali na vituo hivyo kuwa na msaada wa kimalezi kwa wazazi, vina mchango mkubwa katika kukuza maendeleo ya awali ya watoto kwa kuwajengea malezi ya kitaaluma.
Anaongeza: “Watoto wadogo wanapopelekwa katika mazingira haya yenye programu maalum za kielimu na michezo ya kujifunza, hukuza uwezo wao wa kiakili, kihisia, na kijamii. Watoto hujifunza mambo ya msingi kama vile kuzungumza, kusikiliza, kushirikiana na wenzao na kufuata maelekezo.’’
Hata hivyo Charity anasema ni muhimu wazazi wakatambua kuwa vituo hivyo sio kwa ajili ya kuwafanya watoto wabobee katika masomo au matumizi ya Kiingereza kwa kile alichoeleza kuna walimu ambao wanalazimika kuwafundisha vitu vikubwa watoto kwa ajili ya kuwafurahisha wazazi.
Anasema” “Miongoni mwa vitu tunavyovifanyia ufuatiliaji ofisi ya ustawi wa jamii ni hivi vituo vya kulelea watoto mchana, lengo ni kuhakikisha hawatoki kwenye lengo la kuanzishwa kwake. Watoto wanatakiwa kufundishwa kulingana na umri wao, lakini utakuta mtoto mdogo analazimishwa kujua kusoma na kuandika na kuzungumza Kiingereza haya yote tunayasimamia kuhakikisha hayafanyiki na badala yake wanalelewa na kujengewa uwezo kwa misingi ya michezo.”

Charity anaeleza pia kuwa vituo hivi huimarisha uhusiano wa kijamii miongoni mwa watoto, kupitia mwingiliano wao wa kila siku hujifunza stadi muhimu za maisha kama vile kuvumiliana, kushirikiana, kusaidiana na kutatua migogoro kwa amani.
Anasema hali hiyo huwasaidia watoto kukuza ujasiri, maadili na tabia njema ambazo ni muhimu katika maisha yao yote kama ambavyo matarajio ya jamii yoyote yenye maadili mema huanza kujengwa tangu utotoni.
Kwenye ulinzi na usalama, anasema vituo vya kulelea watoto vinachangia kwa kiasi kikubwa katika kuhakikisha usalama wa mtoto na vina mchango mkubwa katika kupunguza matukio ya unyanyasaji wa watoto au utegemezi wa malezi yasiyo salama
“Tofauti na hali ambapo mtoto huachwa nyumbani bila uangalizi au chini ya uangalizi wa mtu asiye na mafunzo, vituo hivi hutoa huduma bora ya malezi kwa kuzingatia usalama, afya na lishe ya watoto.
Katika familia nyingine, watoto huachwa mikononi mwa watu wasiostahili au huachwa peke yao nyumbani, jambo ambalo linaweza kuwaweka katika hatari ya kudhurika kimwili, kihisia au hata kiakili. Walezi katika vituo hivi wana jukumu la kuhakikisha mtoto anapata uangalizi wa hali ya juu. Hili ni jambo la msingi hasa kwa watoto wa umri mdogo ambao wanahitaji uangalizi wa karibu,” anasema.
Mbali na hayo, ofisa huyo wa ustawi wa jamii anasema uwepo wa vituo vya kulelea watoto umekuwa chachu ya ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi.
“Katika jamii nyingi, jukumu la malezi limekuwa likiwaangukia wanawake zaidi. Hali hii imewazuia wanawake wengi kushiriki kikamilifu katika kazi au biashara. Vituo vya kulelea watoto vinaposaidia kuondoa mzigo huu wa malezi kwa kutoa huduma ya malezi bora, wanawake hupata fursa ya kujishughulisha na shughuli za maendeleo, hivyo kusaidia kuongeza pato la familia na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Yanayopaswa kuzingatiwa na walimu.
Mratibu wa kituo cha Kilwa Masoko FDC Daycare Sara Said anasema yapo mambo kadhaa ambayo mwalimu anayelea watoto anapaswa kuzingatia ili kuhakikisha anakuwa msaada kwa watoto hao.
“Mwalimu anapaswa kuwa na uelewa wa kina wa hatua za ukuaji za mtoto kulingana na umri wao. Watoto katika vituo hivi huwa katika umri wa miaka sifuri hadi sita, kipindi ambacho kinahesabika kuwa cha msingi katika maisha ya binadamu.
Katika kipindi hiki, mtoto anaanza kujifunza kuzungumza, kuwasiliana, kuingiliana na watu wengine, na kutambua mazingira yanayomzunguka. Ukielewa jinsi watoto wanavyokua kimwili, kiakili, kihisia, na kijamii utaweza kuwasaidia ipasavyo”anasema Sara na kuongeza:
“Kwa mfano, mtoto wa miaka miwili hawezi kutarajiwa kuwa na uwezo wa kujieleza kama mtoto wa miaka mitano, hivyo walimu wanapaswa kutumia mbinu mbalimbali zinazolingana na hatua ya ukuaji ya kila mtoto.
Jambo lingine la kuzingatia ni stadi za mawasiliano, Sara ambaye kitaaluma ni mwalimu anasema eneo hilo ni msingi mkubwa katika kazi ya walimu wa watoto wadogo.
“Mawasiliano kati ya mwalimu na mtoto yanapaswa kuwa ya kirafiki, yenye upendo na kueleweka kwa urahisi. Watoto wadogo hawana uwezo mkubwa wa kueleza hisia zao au matatizo yao, hivyo walimu wanapaswa kuwa na uwezo wa kusoma ishara, mienendo na mabadiliko ya kihisia kwa watoto ili waweze kuwasaidia”.
Mkazi wa Kilwa Masoko Seleman Kindamba anasema kuna umuhimu mkubwa wa Serikali, mashirika binafsi na jamii kwa ujumla kuwekeza katika kuanzisha na kuimarisha vituo vya kulelea watoto kama sehemu ya mkakati wa kukuza maendeleo endelevu na ustawi wa jamii.
“Kulingana na mfumo wa maisha yetu ya sasa, hivi vituo vya kulelea watoto vina umuhimu mkubwa katika mazingira ya sasa yanayohitaji usawa kati ya kazi na familia. Mtu utafanya kazi zako kwa ufanisi ukiwa na uhakika mtoto yuko sehemu salama, lakini changamoto ni kwamba si wote tunaweza kumudu hizo gharama kwa sababu vituo hivi vingi ni vya watu binafsi,”anaeleza.