Babu aliyebaka kulawiti wajukuu na  mtoto wa shemeji yake jela maisha

Arusha. Mahakama ya Rufaa imetupilia mbali rufaa iliyokatwa na mkazi wa Ilemela, Mwanza  Hamis Kihalule na kubariki adhabu ya kifungo cha maisha jela aliyohukumiwa baada ya kukutwa na hatia ya makosa matatu ya ubakaji na moja la ulawiti.

Hamis alishtakiwa na kukutwa na hatia katika makosa yote manne aliyoyatenda kwa watoto watatu ambao ni wajukuu zake wawili na mmoja akiwa mtoto wa shemeji yake, aliokuwa akiishi nao nyumba moja.

Hii ni rufaa yake ya pili kukwaa kisiki ambapo ya kwanza aliikata Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza baada ya Hakimu aliyekuwa akiisikiliza kuongezewa mamlaka, ambapo Mahakama iliyotupilia mbali rufaa hiyo.

Awali Mahakama ya Wilaya ya Ilemela ilimkuta na hatia na kumuhukumu adhabu ya kifungo cha maisha jela baada ya kukutwa na hatia katika makosa matatu ya ubakaji kinyume na kifungu cha 130(1)(2)(e) na 131(1) cha kanuni ya adhabu, na kosa moja la ulawiti  kinyume na kifungu cha 154(1)(a) na (2) cha kanuni ya adhabu.

Hukumu hiyo imetolewa Mei 23,2025 na jopo la majaji watatu wa Mahakama hiyo ya juu ambao ni Lugano Mwandambo, Abraham Mwampashi na Dk  Ubena Agatho, katika rufaa hiyo ya jinai na nakala yake kuwekwa katika mtandao wa Mahakama.

Baada ya kupitia sababu za rufaa na mwenendo wa shauri hilo, majaji hao walikubaliana makosa yote yalithibitishwa pasipo shaka yoyote hivyo kutupilia mbali rufaa hiyo kwani haina mashiko.

Katika shitaka la kwanza alidaiwa Januari 3, 2021 eneo la Kirumba, wilayani Ilemela Mkoa wa Mwanza alimbaka mtoto wa kike (AA) aliyekuwa na umri wa miaka saba.

Kosa la pili alidaiwa tarehe hiyohiyo alimbaka mtoto wa kike (BB), aliyekuwa na umri wa miaka mitatu.

Kosa la tatu, katika tarehe isiyojulikana kati ya Desemba 2020 na Januari 3,2021 katika eneo la Kirumba mkoani humo alimbaka mtoto wa kike  (CC), aliyekuwa na umri wa miaka saba.

Katika kosa la nne, Hamis alishtakiwa kwa kosa la ulawiti alilodaiwa kutenda kwa tarehe isiyojulikana kati  ya Desemba 2020 hadi Januari 3,2021 kwa mtoto wa kike (CC), aliyekuwa na umri wa miaka saba.

Katika kesi hiyo upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi wanane, ambapo mwathirika wa pili (BB) alishindwa kutoa ushahidi kutokana na umri wake kuwa mdogo.

Kwa mujibu wa kumbukumbu, shahidi wa kwanza (baba wa AA), alishuhudia kuwa mrufani ni shemeji yake na walikuwa wakiishi nyumba moja.

Alieleza Januari 3, 2021, akiwa kazini mtoto wake mwingine alimfuata na kumjulisha kuwa mrufani huyo amembaka AA, ambapo alilazimika kurudi nyumbani na kumpeleka mtoto kituo cha polisi, na baadaye hospitali kwa uchunguzi wa kiafya.

Shahidi wa pili ambaye ni mama wa BB, aliieleza Mahakama kuwa alipokuwa akitoka kwenye mazishi, alijulishwa na shahidi wa saba kuwa BB amebakwa na mrufani.

Akitoa ushahidi shahidi wa tatu ambaye ni bibi wa CC, aliiambia Mahakama kuwa mrufani ni mumewe na siku ya tukio Januari 3, 2021, alipotoka kwenye maziko alikuta umati wa watu nyumbani waliomjulisha kuwa AA na CC wamebakwa na mrufani.

Alieleza kuwa watoto hao walipelekwa kituo cha polisi na baadaye hospitalini ambapo ilibainika kuwa walibakwa na CC alilawitiwa.

Shahidi wa nne (AA), aliileza Mahakama siku ya tukio Hamis alipeleka kochi nyumbani kwao ambapo alimbaka ambapo wakati tukio hilo linatokea BB na mtoto mwingine walikuwepo hapo.

Shahidi wa tano (CC), aliiambia Mahakama kuwa Hamis ni babu yake na alikuwa akimbaka na kumlawiti mara kwa mara huku akimpa pesa kwa ajili ya kununua pipi shuleni, na kuwa alipata tatizo la kushindwa kuzuia haja kubwa.

Shahidi wa sita ambaye ni bibi wa mwathirika wa pili na tatu na shemeji wa Hamis, aliiambia Mahakama kuwa siku ya tukio alipigiwa simu na kujulishwa shemeji yake amewabaka watoto na aliporudi nyumbani aliwakagua watoto hao na kubaini wamefanyiwa vitendo hivyo, huku CC akiwa ameharibika njia ya haja kubwa.

Shahidi wa saba ambaye ni msaidizi wa kazi za nyumbani, aliiambia Mahakama kuwa Januari 2, 2021 aliona Hamis akimbaka AA huku CC akiwa ameketi kwenye kochi katika chumba hicho.

Shahidi wa nane ambaye ni daktari bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Sekou-Toure jijini Mwanza, alishuhudia kuwa Januari 3, 2021 akiwa kazini alipokea watoto watatu (AA,BB na CC) waliokuwa na wazazi na walezi wao, aliwachunguza na kubaini wote wamebakwa na CC amelawitiwa.

Katika utetezi wake Hamis alijitenga na mashitaka hayo na kueleza Mahakama siku ya tukio alikuwa kwenye mazishi na kudai kuwa kesi hiyo ni ya kutengenezwa kwa sababu alikataa kuwapa samaki baadhi ya mashahidi wa mashitaka.

Katika rufaa hii ya pili, Hamis alikuwa na sababu nne za rufaa ambazo ni shitaka halikuonyesha muda kamili ambao kosa lilitendeka, taratibu za utambuzi zilikiukwa kwa vile waathiriwa hawakumtambua mrufani kizimbani, utetezi wake haukuzingatiwa na kesi haikuthibitishwa bila kuacha shaka yoyote.

Katika rufaa hiyo Hamis alijiwakilisha mahakamani mwenyewe huku mjibu rufaa akiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Safi Amani, aliyepinga rufaa hiyo.

Baada ya kusikiliza mawasilisho ya pande zote, majaji hao walieleza kuwa kuhusu sababu ya muda wa kosa kutendeka, rekodi ya rufaa katika ukurasa wa tatu inaonyesha makosa hayo yalitendeka kati ya Desemba 2020 hadi Januari 3, 2021.

Kuhusu hoja ya utambuzi, amesema wa  shahidi wa nne katika ukurasa wa 25 wa rekodi ya rufaa ni wazi kwamba alimtambua Hamis kizimbani huku ukurasa wa 26 shahidi wa tano akimtambua kama babu yake na kumtaja kwa jina lake.

“Tunashikilia kwa kuwa waathiriwa walimtambua mrufani, utambulisho wa kizimbani hautakuwa wa ziada. Kwa hivyo, msingi wa pili wa rufaa umekataliwa,”alisema Jaji Agatho

Kuhusu hoja ya utetezi wake kutozingatiwa na Mahakama ya kwanza ya rufaa, rekodi inaonyesha katika ukurasa wa 67, 70,74 na 76 inaonyesha Mahakama ilizingatia ushahidi wa pande zote mbili ikiwemo utetezi.

Jaji Agatho alisema kuhusu makosa hayo kutothibitishwa, rekodi ya rufaa inaonyesha ushahidi wa shahidi wa tano hadi wa nane walithibitisha makosa ya ubakaji na ulawiti na ushahidi wa shahidi wa tano, sita na saba ulithibitisha kuwa ni mrufani ametenda makosa hayo.

“Kwa sababu zilizotajwa hapo juu, tunaona rufaa hii haina mashiko na hivyo basi, tunaitupilia mbali,”alihitimisha Jaji Agatho.

Related Posts