Iringa. Wananchi, viongozi wameshiriki mazishi ya aliyekuwa diwani wa Kata ya Kiwere, Felix Waya aliyefariki dunia baada ya kumaliza kuhutubia kwenye mkutano katika mkutano wa hadhara uliofanyika ukumbi wa Masai.
Miongoni mwa walioshiriki mazishi hayo ni viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Iringa, ambapo wameeleza kupata pigo kufuatia kifo cha Felix.
Wameeleza kuwa ni pigo kwao kutokana na tabia njema ya diwani huyo ya kupenda kutafuta maendeleo kwa manufaa ya jamii nzima inayomzunguka.

Ikumbukwe kuwa Diwani Waya alifariki ghafla jioni ya Mei 23, 2025 baada ya kujisikia vibaya baada ya kumaliza kuhutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika ukumbi wa Masai katani hapo.
Diwani Waya, alihudumu kwenye nafasi hiyo kwa vipindi viwili 2015-2020 alikuwa kiongozi kutokea cha cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) huku 2020-2025 alihamia CCM akihudumu kwenye nafasi hiyo hiyo.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Mei 26, 2025 msibani hapo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yassin amesema kuwa chama kimepoteza mzalendo wa kweli ambaye hakuwa na makuu.

Baadhi ya waombolezaji waliofika msibani kwa aliyekuwa Diwani wa kata ya Kiwere Wilayani Iringa, Felix Waya.
“Diwani Waya alikuwa ni kiongozi wa mfano na hata juzi kwenye mkutano wetu hapa katika kata yake ameeleza vizuri sana ilani yetu ya CCM kwa kweli tutamkumbuka kwa mengi,”amesema Yassin.
“Diwani Waya alikuwa kiongozi wa mfano, hakuwa mtu wa maneno mengi bali matendo na katika kata yetu amefanya maendeleo kwenye sekta mbalimbali kwa juhudi zake,” amesema Agatha Mwaya, mkazi wa kijiji cha Mgela.

Mke wa marehemu Felix Waya akiwa ameshikiliwa na ndugu zake wakati kutoa heshima za mwisho kwa kumwaga mchanga kaburini.
Roliy Lyangi, amesema kuwa kifo cha diwani huyo ni pigo kwa wanawake wafugaji wa kata hiyo.
Kwa mujibu wa wananchi, Waya alikuwa chachu ya mafanikio ya miradi ya afya, elimu na miundombinu ikiwemo madarasa na mazingira.
Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Anold Mvamba amesema, “ingekuwa inawezekana tungemuomba Mungu na kumwambia kaka yetu Waya anyanyuke na atazame umati huu unaomlilia.
“Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe,” amesema Mvamba.
Marehemu Waya ameacha mjane na watoto wanne.