Majaliwa ataja njia mbadala kuwawezesha wafanyabiashara

Osaka. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea na mikakati ya kuwaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na wenzao wa mataifa mbalimbali duniani, ikiwemo Japan, ili kuwawezesha kunufaika na fursa zilizopo katika mataifa hayo.

Majaliwa amesema Serikali imekuwa ikifanya hivyo kwa kushiriki katika makongamano mbalimbali ya kimataifa, ambayo yamekuwa yakiwakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji ili kuongeza tija kwenye masuala ya biashara na uwekezaji.

Amesema hayo leo (Jumatatu, Mei 26, 2025) alipofungua kongamano la Biashara, Uwekezaji na Utalii lililowakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania pamoja na wafanyabiashara na wawekezaji wa Japan, katika Hoteli ya Westin, Osaka, Japan, ikiwa ni sehemu ya  ushiriki wa Tanzania katika maonersho ya World Expo Osaka 2025.

“Tumewaeleza wafanyabaishara na wawekezaji hawa wa Japan fursa ambazo zipo nchini, hii ni mara ya tatu tunakutana na wafanyabara na wawekezaji kutoka Japan, tayari tumeanza kuona manufaa ya makongamano haya kutokana na kuongezeka kwa biashara kati ya mataifa haya mawili.”

Amesema hadi Machi 2025, jumla ya kampuni 24 kutoka Japan zimewekeza nchini katika miradi mbalimbali yenye thamani ya Dola 42.70 milioni za Marekani (sawa na Sh115 bilioni) nchini na kutoa ajira 1,182 kwa Watanzania.

Majaliwa amesema licha ya uwekezaji wa makampuni hayo, Serikali ya Tanzania imeendelea kunufaika na ushirikiano wake na Japan kwa kupata misaada katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo na miundombinu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameshuhudia utiaji saini wa hati sita za makubalino, ikiwemo ya ushirikiano katika kuendeleza sekta ya mafuta baina ya Serikali ya Tanzania na Shirika la JGC la Japan, hati nyingine ni baina ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Axcel Afrika kwa ajili ya kukuza uwekezaji nchini.

Hati nyingine zilizosainiwa ni kati ya Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) na Axcel Afrika kwa ajili ya kukuza uwekezaji Zanzibar, Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC) na Shirika la Nishati la Toshiba, Shirika la Tiba la Tokoshukai na Chuo Kikuu cha Dodoma na Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Hati nyingine ni kati ya Chuo Kikuu cha Dodoma na Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa upande mmoja na Chama cha Maendeleo na Uchumi Afrika cha Japan (Afreco)

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Suleimani Jafo amesema dhamira ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania nchi ya uwekezaji inazindi kufunguka, hivyo amewaomba Watanzania kuhakikisha wanachangamkia fursa hizo kwa ajili ya maendeleo yao binafsi na Taifa.

Amesema lengo la Serikali la kutafuta fursa hizo za biashara, uwekezaji na utalii ni kukuza uchumi pamoja na kuwezesha upatikanaji wa ajira nchini.

Katika kufanikisha hilo, amesema kipaumbele kimewekwa katika sekta za biashara, miundombinu, utalii, uchumi wa buluu, uwekezaji kwa kuwa Japan imepiga hatua kubwa katika sekta hizo.

Dk Jafo amesema kipaumbele kingine ni kutafuta wawekezaji watakaoshirikiana nao katika kuendeleza sekta ya kilimo ili kuwa na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, kuendeleza kilimo cha umwagiliaji kwa kujenga miundombinu ya kisasa, katika sekta ya madini na kuyaongezea thamani madini ya kimkakati.

Kwa upande wake Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Omar Said Shaaban amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejipanga katika kutumia fursa za uwekezaji zinazotokana na ushirikiano kati ya Tanzania na Japan.

Waziri Shaaban amesema tayari Serikali imeshaanza utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya uwekezaji ikiwemo ujenzi wa mitaa ya viwanda ambapo mmoja umejengwa mtaa wa Duga Zuze, Zanzibar na Chamanangwe, Pemba.

Mbali na miradi ya ujenzi wa mitaa ya viwanda, pia Waziri Shaaban amesema SMZ kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyabiashara Zanzibar wameandaa jarida linaloeleza fursa za uwekezaji Zanzibar ambalo limezinduliwa na Waziri Mkuu na kugawiwa kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa Japan.

Amesema eneo jingine ambalo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejipanga kutafuta wawekezaji ni uchumi wa buluu kupitia mazao ya bahari, ikiwemo usindikaji wa samaki ili kuhakikisha unafanyika kisasa zaidi kwa faida ya wananchi na Serikali.

Awali, Kamishina Jenerali wa World Expo Osaka 2025 kwa Tanzania na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa Khamis amesema kongamano hilo ambalo ni sehemu ya ushiriki wa Tanzania katika maonesho hayo linalenga kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Japan.

Mkurugenzi huyo alisema maeneo ambayo yamepewa kipaumbele katika kongamano hilo ni kwenye sekta ya nishati, madini, kilimo, huduma za kibenki, utalii, uwekezaji na afya.

 Katika maonyesho hayo wafanyabiashara wa Tanzania wanakutana na wafanyabiashara wa Japan kujadiliana namna ya kushirikiana katika kukuza biashara na uwekezaji.

Related Posts