Arusha. Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limeitaka familia ya Mchungaji wa Kanisa la Huduma ya Kristo, lililopo Mtaa wa FFU, kata ya Muriet mkoani Arusha, Steven Jacob (35), aliyekuwa ametekwa na watu wasiojulikana, kuwa na subira wakati wakikamilisha upelelezi wa tukio hilo.
Polisi imetoa tamko hilo ikiwa imepita siku moja tangu familia ya mchungaji huyo kusema kuwa imeamua kumwachia Mungu kwa kile kilichomtokea ndugu yao.
Mchungaji huyo alitekwa na watu wasiojulikana Mei 16, 2025 kabla ya kesho yake kuokolewa na walinzi wa mashamba ya ngano mkoani Kilimanjaro, akiwa na majeraha mbalimbali ya kipigo mwilini mwake.
Akizungumza leo Mei 26, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema sakata hilo bado lipo polisi likifanyiwa kazi.
“Suala hilo bado linafuatiliwa, kikubwa familia iwe na subira wakati upelelezi unaendelea na soon (haraka iwezekanavyo) tutatoa taarifa juu ya tukio hilo,” amesema Kamanda Masejo.
Jana, Mei 25, 2025, akizungumza na Mwananchi, baba mzazi wa mchungaji huyo ambaye pia ni mchungaji na balozi wa nyumba 10 wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jacob Gumbo alisema kwa sasa wamemuachia Mungu suala hilo na wanaendelea kumuuguza ndugu yao.
“Polisi walikuja tangu ile siku (Mei 17) alivyopatikana wakachukua maelezo ila baada ya pale hatujapata mrejesho wowote wala hakuna hatua yoyote na sisi hatujachukua hatua nyingine zaidi tumemuachia Mungu”
Gumbo amesema kwa sasa wanaendelea kumuuguza ndugu yao nyumbani na anaendelea vizuri.
Awali, Mei 17, 2025 akisimulia tukio hilo Mchungaji Steven alidai watu hao waliomteka walijitambulisha kwake kuwa maofisa wa polisi, lakini hawakumuonyesha vitambulisho wakidai wanampeleka kituo kikuu cha Polisi.
Alisema kutokana na namna walivyomchukua alijua ametekwa, kwani hawakuwa na vitambulisho na hawakutaka aage mtu. Alisema walimchukua na kumfunga vitambaa viwili usoni na pingu mkononi, ndipo alipopiga kelele kuwa anatekwa, watu hao wakamrusha kwenye gari na kuondoka naye kwa kasi.
Mchungaji huyo alidai waliomteka walimpeleka hadi eneo hilo la West Kilimanjaro ambako walichukua simu zake za mkononi na kumtaka afute picha mjongeo (video) alizokuwa amepandisha kwenye mtandao wa Youtube.
Mei 18, 2025, ibada ya Jumapili kanisani hapo iliongozwa na Mchungaji Vulfrida George akisaidiana na Mchungaji Gumbo ambapo waumini wa kanisa hilo kutoka matawi mbalimbali nchini walieleza namna walivyokimbilia kanisani kuomba kwa saa kadhaa, ili kiongozi wao arejee salama.
Waumini hao wamesema hawakuwa na namna yoyote wala hawakujua nini kingine wanaweza kufanya zaidi ya kukimbilia kanisani kumuomba Mungu.