Polisi watoa kauli sakata la mchungaji kutekwa Arusha, Padri Kitima

Dar/Arusha. Ikiwa ni takribani wiki moja tangu watu wasiojulikana kumteka Mchungaji Steven Jacob (35) wa Kanisa la Huduma ya Kristo mkoani Arusha na baadaye kuokotwa akiwa na majeraha, Jeshi la Polisi mkoani humo limesema upelelezi unaendelea.

Mchungaji huyo baada ya kutekwa mkoani Arusha, siku moja baadaye alipatikana porini West Kilimanjaro akiwa na majeraha mwilini.

Hata hivyo tukio la kushambuliwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima, limeendelea kuwa kitendawili baada ya Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alipotafutwa kwa njia ya simu na ujumbe wa maandishi kueleza wapi wamefikia, hakutoa mrejesho wowote.

Akizungumzia uchunguzi wa tukio la mchungaji huyo leo Mei 26, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Justine Masejo amesema sakata hilo bado liko polisi likifanyiwa kazi.

“Swala hilo bado linafuatiliwa, kikubwa familia iwe na subira wakati upelelezi unaendelea na soon (haraka iwezekanavyo) tutatoa taarifa juu ya tukio hilo,” amesema Kamanda Masejo.

Polisi mkoani Arusha imetoa tamko hilo, siku moja tangu familia ya mchungaji huyo kusema imeamua kumwachia Mungu kwa kile kilichomtokea ndugu yao.

Mchungaji Jacob alitekwa na watu wasiojulikana Mei 16, 2025 kabla ya kesho yake kuokolewa na walinzi wa mashamba ya ngano mkoani Kilimanjaro akiwa na majeraha mbalimbali ya kipigo mwilini mwake.

Aidha jana Jumapili Mei 25, 2025 akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, baba mzazi wa mchungaji huyo ambaye pia ni mchungaji na balozi wa nyumba 10 wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jacob Gumbo amesema kwa sasa wamemuachia Mungu suala hilo na wanaendelea kumuuguza ndugu yao.

“Polisi walishakuja tangu ile Mei 17 alivyopatikana wakachukua maelezo ila baada ya pale hatujapata mrejesho wowote, wala hakuna hatua yoyote na sisi hatujachukua hatua nyingine zaidi tumemuachia Mungu.”

Baba huyo amesema mwanae kwa sasa wanaendelea kumuuguza nyumbani na anaendelea vizuri.

Awali Mei 17, 2025 akisimulia tukio hilo, Mchungaji Jacob alidai watu hao waliomteka walijitambulisha kwake kuwa maofisa wa polisi, lakini hawakumuonyesha vitambulisho wakimtaka kufika naye kituo kikuu cha polisi.

Amesema kutokana na namna walivyomchukua, alielewa ametekwa kwani hawakuwa na vitambulisho na hawakutaka aage mtu, badala yake walimchukua na kumfunga vitambaa viwili usoni na pingu mkononi, ndipo alipopiga kelele kuwa anatekwa, kisha watu hao wakamrusha kwenye gari na kuondoka naye kwa kasi.

Mchungaji huyo alidai waliomteka walimpeleka hadi eneo hilo la West Kilimanjaro ambako walichukua simu zake za mkononi na kumtaka afute picha mjongeo (video) alizokuwa amepandisha kwenye mtandao wa YouTube.

“Naomba nisiongee mengi kwa sababu ni ishu za mtandao nilipost YouTube. Baada ya kunipiga na kuchukua baadhi ya maelezo ambayo nafikiri nisingependa kuyaongea, baada ya pale nikasikia kama wananipeleka mahabusu ila haikuwa hivyo, wakanipeleka porini West Kilimanjaro.

“Walivyotaka nifute, kwa bahati mbaya bando lilikuwa limeisha, ikabidi wafanye mpango wapate bando, wakasema wawili au mmoja abaki na mimi halafu wengine wakatafute bando ili nifute video,” amesema mchungaji.

Mchungaji huyo amesema watu hao walimwambia alale chini wakamkanyaga shingoni, mmoja akawaambia wenzake wanamuachaje hapo.

Amesema mambo mengine hawezi kuzungumza zaidi ila walimuacha wakaondoka na simu yake.

“Walivyoondoka nikaanza kubiringita na kutembea kwa magoti hadi barabarani, nikafika barabarani pakatokea bodaboda, alivyoona ile hali akapita, lori la mafuta nalo likaogopa.

“Wakaja watu wanaolinda tembo wasiingie kwenye mashamba, nikajitambulisha mimi ni mtumishi wa mtandaoni nimetekwa nimetupwa huku nisaidieni, mmoja wao alikuwa mwoga kesi isije kuhamia kwao ila wakanisaidia nikaomba simu ili niwajulishe watu niko hai,” amesema.

Mchungaji huyo amesimulia, “Walinipeleka kwenye kambi yao na baadaye wakaniambia watu wale wamerudi kule kama wananitafuta, wakafanya mpango nikatolewa nikaenda sehemu nyingine, naomba mengine nisongee.”

Ili kufahamu zaidi kama uchunguzi bado unaendelea kuhusu tukio la Padri Kitima, Mwananchi ilimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, kwa njia ya simu bila mafanikio.

Tayari TEC kupitia kwa rais wake Askofu Wolfgang Pisa katika ibada maalumu ya kuwekwa wakfu kwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, Mhashamu Josephat Jackson Bududu alisema,

“katika utawala bora na wa sheria wahalifu wale walipaswa wawe wameshafikishwa mahakamani mpaka sasa, matumaini yetu uchunguzi hautachukua muda mrefu zaidi kabla ya wahusika kufikishwa mbele ya sheria,” alidokeza.

Ikukumbwe mwanzoni mwa Mei, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kupitia kwa kamanda wake Muliro lilieleza kuendelea kuchunguza tukio la kushambuliwa kwa Padri Kitima.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda Muliro, tukio hilo lilitokea saa nne na robo usiku, usiku wa kuamkia Mei Mosi, 2025.

Padri Kitima alikuwa ametoka kuhudhuria kikao cha viongozi wa dini kilichodumu kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa moja jioni.

Baada ya kikao hicho, aliendelea kubaki kantini ya baraza kwa ajili ya kupata kinywaji, ambapo baadaye alielekea maliwatoni na ndipo alipovamiwa na kushambuliwa na watu wawili waliotumia kitu butu.

Padri Kitima alipelekwa katika Hospitali ya Aga Khan kwa ajili ya matibabu na hali yake inaelezwa kuwa inaendelea vizuri.

Kabla ya kuhamishiwa Aga Khan, Jeshi la Polisi lilieleza kumshikilia mtu mmoja, Rauli Mahabi (maarufu kama Haraja), mkazi wa Kurasini, kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na tukio hilo huku uchunguzi wa kina ukiendelea ili kuwabaini wote waliohusika na kuhakikisha hatua kali zinachukuliwa mara moja.

Pia Mei 5, 2025, Kamanda Muliro alitangaza jeshi hilo linamshikilia na kumuhoji Dk Frey Edward Cosseny aliyemuonya Padri Kitima kupitia mitandao ya kijamii.

Dk Cosseny aliandika ujumbe wa kumuonya Padri Kitima na siku mbili baadaye akashambuliwa. Ujumbe huo aliutoa Aprili 28, 2025 usiku ukisomeka:

“Mwambieni Kitima iko siku ataingia kwenye 18 hatokaa asahau Tanzania muacheni ajifanye mwanasiasa. Mfikishieni message siku si nyingi atapata anachokitafuta dawa yake iko jikoni atakuja kuozea jela.”

Kukamatwa kwake ni baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa, kuliagiza jeshi hilo kumtafuta na kumuhoji mtuhumiwa huyo aliyeandika kwenye mitandao ya kijamii “siku za Kitima zinahesabika.”

“Naliagiza Jeshi la Polisi kumtafuta kwa haraka, yule mtu aliye-tweet kwenye mitandao ya kijamii kwamba, ‘siku za Kitima zinahesabika’ mtu huyu atafutwe haraka ahojiwe ametumwa na nani, na hatua kali za kisheria zichukuliwe haraka iwezekanavyo kwa watu wote watakaobainika kuhusika katika tukio hili,” aliagiza Bashungwa, Mei 2, 2025.

Related Posts