Ujenzi wa minara 758 wafikia asilimia 90

Dar es Salaam. Mradi wa ujenzi wa minara 758 ulioanza mwaka 2023 umefikia asilimia 90.3 huku ukitajwa kuwa chachu ya ongezeko la watu wanaotumia huduma za mawasiliano Tanzania.

Hadi Mei 23 mwaka huu, minara 682 ilikuwa tayari imekamilika huku mingine ikiwa katika hatua mbalimbali za kumaliziwa ujenzi.

Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu Mfuko Wa Mawasiliano Kwa Wote (UCSAF), Peter Mwasalyanda leo Jumatatu ya Mei 26, 2025 wakati akizungumza na waandishi na wahariri wa vyombo vya habari alipokuwa akielezea mafanikio ya mfuko huo ndani ya miaka minne ya awamu ya sita.

Amesema mkataba wa utekelezaji wa mradi huo uliingiwa Mei 2023 ambapo Serikali kupitia UCSAF ilisaini makubaliano na watoa huduma kufikisha mawasiliano maeneo ya vijijini.

Kupitia mradi huu wananchi milioni 8.5 kutoka mikoa 26 wanatarajiwa kufikiwa na huduma za uhakika za mawasiliano kupitia wilaya 127 zitakazofikiwa.

“Pia mradi huu utafika katika kata 713 na tayari minara 533 imewaka na imeanza kutoa huduma katika maeneo mbalimbali nchini, mradi huu ulitumia ruzuku ya Sh126 bilioni. Hii itawasaidia watu kunufaika na huduma za uhakika za mawasiliano hasa katika maeneo yaliyokuwa na huduma hafifu au hakuna kabisa” amesema.

Amesema mbali na kujenga minara mipya pia mingine 304 imeongezwa nguvu kutoka 2G kwenda 3G au 4G ili watu wapate intaneti huku ruzuku ya Sh5.51 ikitumika.

Amesema mwaka 2021 taarifa zinaonyesha kuwa idadi ya laini za simu ilikuwa milioni 54 ambazo ziliongezeka hadi kufikia milioni 90.4 Machi mwaka huu kwa mujibu wa ripoti ya Machi, 2025 iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Pia idadi ya watumiaji wa intaneti waliongezeka hadi kufikia milioni 49.3 Machi mwaka huu ikilinganishwa na watumiaji milioni 29.8 waliokuwapo 2021.

Mwasalyanda amesema uwekezaji huu haushii katika kujenga miundombinu pekee bali pia wamekuwa wakitoa mafunzo kwa walimu wa sekondari ili waweze kusaidia wanafunzi wao kujifunza na kuendana na kasi ya mabadiliko ya Tehama.

Hadi sasa walimu 3,798 kutoka shule za umma 1,791 wamepata mafunzo hayo ambapo kati ya 326 ni kutoka Zanzibar na Tanzania Bara wakiwa walimu 3,180.

“Mafunzo haya hutolewa katika vyuo vya DIT, UDOM na MUST kwa miaka minne walimu 1,585 wamepata mafunzo haya,” amesema Mwasalyanda.

Mbali na mafunzo hayo pia wamekuwa wakifanya uwezeshaji wa vifaa vya kujifunzia katika shule na tayari 1,121 zimefikishiwa vifaa ambapo kwa wastani shule hupata kompyuta tano, printa moja na projecta moja huku gharama za mradi zikiwa ni Sh5.94 bilioni.

“Mradi huu wa vifaa vya Tehama pia hufanyika kwa shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu ambapo hadi sasa shule 22 kulifikishiwa vifaa ambavyo ni runinga, Braille Machine (Nukta Nundu) Orbit reader (Machine za Kisasa), kompyuta mpaka, Embosser (Printa ya nukta nundu), Digital voice recorders (kidaka sauti cha kisasa), Magnifiers,” amesema.

Ili kufanikisha hilo, ruzuku ya Sh1.8 bilioni ilitumika huku shule zilizonufaika ni kutokana Tanzania Bara na Visiwani. Katika utoaji wa vifaa hiyoi pia vyuo 10 viko mbioni kunufaika na vifaa mbalimbali watakavyopewa vikiwa na thamani ya Sh700 milioni.

Uboreshaji wa miundombinu ya mawasiliano haukufanyika Tanzania bara pekee bali hata Zanzibar ambapo mkataba wa ujenzi wa minara 42 ulisainiwa Januari 2022 utekelezaji ukifanyika kwa ushirikiano na Zantel/Honora. Mradi huo ulinufaisha shehia 38 huku ukitumia ruzuku ya Sh6.9 bilioni.

Akizungumza kwa niaba ya Jukwaa la Wahariri Tanzania, Bakari Kimwanga ametaka jitihada zaidi kufanyika kuhakikisha maeneo ambayo hayana mawasiliano yanafikiwa kikamilifu.

Related Posts