Wabunge wawachachamalia wanaharakati kutoka nje

Dodoma. Baadhi ya wabunge leo wamegeuka mbogo wakiwataja wanaharakati kutoka Kenya kwamba “wanachezea amani na usalama wa Tanzania”.

Wengine wamekwenda mbali wakisema Tanzania ni Taifa imara na lenye nguvu na watu wake wana akili na wanajitambua.

Wametoa kauli hizo kwa nyakati tofauti wakati wakichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2025/26, iliyowasilishwa na Waziri wa wizara hiyo, Innocent Bashungwa.

Bashungwa ameomba Bunge lipitishe Sh2.06 trilioni ambazo zitakwenda kutekeleza jumla ya vipaumbele vitano kwa mwaka 2025/26, ikiwa ni ongezeko la takriban Sh300 bilioni kutoka Sh1.71 trilioni za mwaka 2024/25.

Mei 18, 2025, Karua akiwa na Jaji Mkuu mstaafu Mutunga walizuiwa kuingia nchini wakiwa tayari wamefika Uwanja wa JNIA jijini Dar eSalaama na kutakiwa warudi kwao, wakiwa wanataka kwenda Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusikiliza kesi zinazomkabili Tundu Lissu, mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mbali na wawili hao, wanaharakati wengine wawili, Agather Atuhaire wa Uganda na Boniface Mwangi wa Kenya nao walidaiwa kukamatwa katika sakata hilo na kupatikana wakiwa wametupwa kwenye mipaka ya nchi zao, wakiwa wameshambuliwa na kujeruhiwa.

Hata hivyo, David Maraga, jaji mkuu mwingine mstaafu wa Kenya alifanikiwa kufika Kisutu kusikiliza kesi hiyo.

Kitendo cha kuzuiwa kwa wanaharakati hao kilizua maswali mengi miongoni mwa wadau wa siasa, watetezi wa haki za binadamu wa ndani nan je ya Tanzania wakipinga na kukosoa kitendo hicho.

Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan alijibu kauli za wanaopinga kuzuiwa kwa wanaharakati hao na akaonya tabia ya wanaharakati kutoka nje ya Tanzania na kutaka kuingilia mambo ya ndani ya nchi yake.

“Tumeanza kuona mtiririko wa wanaharakati ndani ya kanda yetu hii kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu, sasa kama kwao wamedhibitiwa, wasije wakatuharibia huku. “Tusitoe nafasi, walishavuruga kwao. Nchi iliyobaki haijaharibiwa, watu wanaishi kwa amani na usalama ni hapa kwetu,” alisema Rais Samia Mei 19, 2025 alipokuwa anazindua Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania.

Alitumia fursa hiyo kuvitaka vyombo vya Ulinzi na Usalama na Wizara ya Mambo ya Nje, kutotoa nafasi kwa aliowaita ni watovu wa nidhamu kuja na kutaka kuingilia mambo ya ndani ya Tanzania.

Alisema binafsi akiwa Rais wa nchi, hana upande, lakini anachofanya ni kulinda nchi yake.

Kauli ya Rais Samia iliungwa mkono na Waziri Kiongozi wa Baraza la Mawaziri la Kenya, Musalia Mudavadi ambaye alisema kuna baadhi ya wanaharakati wa nchi hiyo wanatumia vibaya uhuru uliopo nchini humo.

Hali hiyo ndiyo imewaibua wabunge wakitumia fursa hiyo kukemea vitendo vya kumdhalilisha Rais, ambapo Joseph Kasheku (Musukuma), mbunge wa Geita Vijijini, amesema hakuna disco la Kimasai nchini Tanzania, hivyo haiwezekani Rais akadhalilishwa.

Amesema msimamo wa Tanzania ni kumlinda Rais wake muda wote.

Mbunge huyo pia amesema Watanzania hawana ugomvi na Wakenya bali sakata lililopo ni la mapambano baina yao na wanaharakati, ambao wanalenga kuwachonganisha na kuwaondolea maelewano.

“Na hili tunalisema si kwa wanaharakati kutoka nje tu, lakini hata hapa nchini kama kuna mtu anaonekana kutaka kuvuruga amani ya nchi, akamatwe mara moja na kuwekwa ndani, ili watu wasiwe na dharau na vyombo vya ulinzi na usalama,” amesema Musukuma.

Amesema Watanzania wanapaswa kuwa na wivu wa kumlinda Rais wa nchi akitolea mfano kilichowapata walipotembelea China na kuzungumzia masuala ya Rais wa Taifa hilo kwenye gari.

Amesema kwa sababu ya wivu wa kuwalinda viongozi wa nchi hiyo, dereva teksi aliwashusha kwenye gari kake huku akihoji wameingia katika nchi hiyo kwa lengo la biashara au kumsema kiongozi wao.

 Msukuma amesema kwa namna yoyote wanaharakati hao walipaswa kukamatwa na kushikiriwa siyo kuachiwa watambe kisha wanarudi kwao.

Akizungumzia suala hilo, Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu amesema kuna tatizo mahali na bila ya kuangalia, huenda kutakuwa na matatizo makubwa ya kutokuelewana wakati nchi hizi mbili (Tanzania na Kenya) ni ndugu wa damu.

Pamoja na changamoto ndogondogo zilizopo, bado hazijafikia kuwa sababu ya kutoheshimiana au kuhatarisha utulivu wa Taifa.

Amesema Watanzania hawatakubali kuona nchi yao ikivurugwa na majirani au watu kutoka nje wanaotaka kuhatarisha amani.

“Tanzania bado ni kisiwa cha amani. Hao wanaotutukana majukwaani na mitandaoni, wakipata matatizo wao ndio wa kwanza kutegemea wakimbilie Tanzania,” amesema.

Amesisitiza kuwa vijana wa Kitanzania hawatajiingiza katika mambo ya ‘kipumbavu’, yanayoweza kuvuruga nchi na akawataka wananchi waendelee kuiheshimu na kuilinda amani iliyopo.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Viti Maalum, Ferister Njau amewataka askari polisi kuacha ‘msalia mtume’, bali yeyote anayemgusa Rais kwa hila, anapaswa akamatwe na kuwekwa ndania ili hatua za kisheria zichukuliwe.

“Mtu yeyote anayekwenda kumgusa na kumchezea Rais Samia Suluhu Hassan, lazima akamatwe na kutiwa ndani, kitendo hicho hakipaswi kukubalika mbele ya jamii,” amesema Njau.

Mchango mwingine ulikuwa wa Tauhida Cassian Galoss, mbunge wa Viti Maalumu, ambaye amesema uvumilivu umekuwa mkubwa lakini kwa sasa umefika mwisho, nchi imechoka kuona watu wachache wanamchokonoa Rais bila sababu za msingi.

Amesema kile kinachoendelea mitandaoni hivi sasa ni tishio ndani ya nchi na hivyo anawataka wahusika kusimamia na kuona namna ya kulidhibiti jambo hilo.

Kwa upande wake Mwita Getere (Bunda Vijijini) amesema lazima Rais alinde masilahi ya nchi kwa namna yoyote na kwamba cheo hicho ni taasisi, hivyo anapoguswa si anaguswa Samia bali linaguswa Taifa kwa ujumla.

Hivyo, amewaomba wabunge kusimama pamoja na kulaani vitendo vyote vilivyofanywa na wanaharakati wa Kenya pamoja na kauli zingine za kudhalilisha, akisisitiza ni wakati wa Serikali kuweka mkakati wa kuwachunguza watu kabla ya kuwateua kuwa viongozi.

Hoja hiyo imegusiwa pia na Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu ambaye ameonya kuwa Tanzania isifananishwe na choo ambacho mtu anaweza kuingia kujisaidia na kuondoka zake.

“Tanzania haina ugomvi na marais wanaokuja kwenye Taifa hili ikiwamo Kenya, Uganda, Burundi, Ruanda, Sudani wala DR Congo bali shida yetu tunataka kulinda umoja na mshikamano, uliopo ili watu wengine wasijekuvuruga amani yetu,” amesema mbunge huyo.

Katika hatua nyingine Musukuma amemvaa mbunge mwenzake, Askofu Josephat Gwajima wa Jimbo la Kawe ambaye hivi karibuni alikemea matukio ya utekaji nchini.

Musukuma amewakumbusha wanasiasa wanapoelekea kwenye uchaguzi mkuu, wasipende kutoa ahadi ya vitu ambavyo hawawezi kuvitekeleza huku Askofu Gwajima, kwamba aliahidi kuwapeleka wapigakura wake Japan na China ili wakajifunze, lakini muda umekwisha hajafanya hivyo.

Related Posts