Arusha. Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Thadei Nnko (67) mfanyabiashara wa vyuma chakavu na mkazi wa kata ya Sinon jijini Arusha amejinyonga kwa kile kinachodaiwa kusababishwa na deni la Sh300,000 analomdai mkewe.
Kwa mujibu wa mashuhuda, marehemu alimpa mkewe fedha hizo kwa ajili ya kununua mzigo wa vyuma chakavu, lakini baadaye akaja tena kuitaka kwa ajili ya kwenda kunywa pombe na alipokataliwa ndio ugomvi kuzuka hadi kwenda kuchukua hatua hiyo.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya rufaa Mount Meru.
“Upelelezi unaendelea kujua chanzo halisi cha tukio hilo na ikibainika kuna aliyehusika atachukuliwa hatua za kisheria” amesema.
Balozi wa shina namba 22, Maria Athumani amesema kuwa Mei 25,2025 saa mbili usiku alipigiwa simu kufahamishwa kuwapo kwa ugomvi wa mtu na mke wake.
“Nilitoka mbio kufika eneo la tukio nikakuta Thadei (marehemu) akiwa amelewa sana anampiga mkewe huku akimtukana matusi makubwa akitaka apewe hela yake akanywee pombe.”
“Niliomba msaada wa watu wengine kuwaachanisha ndio akasema ameomba mkopo kwa bosi wake wa Sh300,000 na amempa mkewe amshikie kwa ajili ya kununua chuma chakavu mitaani, akauze arudishe hela lakini mkewe amekataa kumpa,”amesema.
Balozi huyo amesema kuwa alichukua hatua za kumshauri Thadei akalale kesho atapewa lakini aligoma na kuendelea na ugomvi hadi wakafanikiwa kumtuliza na kumuingiza ndani.
“Baada ya kuingia ndani niliondoka sikujua kilichoendelea ndio nashangaa asubuhi hii naambiwa amekutwa amejinyonga kwenye chumba alicholala usiku huo”.
Mke wa marehemu, Magreth Thadei amesema kuwa saa mbili usiku Mei 25,2025 mumewe akiwa amelewa aliingia jikoni alikokuwa anapika akaanza kumdai hela huku akimtukana matusi makubwa.
“Mume wangu anafanya kazi ya kununua vyuma chakavu mitaani na kwenda kuuza na akiwa hana hela anaenda kuomba kama mtaji kwa bosi wake (mnunuzi ) anapewa na ananunua na kwenda kumuuzia.”
“Juzi aliniambia amepewa hela nimshikie kwa ajili ya kununua mzigo sasa nashangaa anakuja tena kudai akiwa amelewa na anataka kuondoka nayo nikaona ataenda kuinywa au kuporwa mzigo uwe kwangu, hivyo nilijificha lakini akanipata na kuanza kunipiga,”amesema na kuongeza.
“Nilikimbia asiendelee kunipiga huku akisema hakuna mtu kulala ndani kwake, lakini baadaye aliingizwa ndani akajifungia hivyo nilinyata kuingia chumba cha pili nikalala kuepusha ugomvi zaidi,”amesema.
Amesema asubuhi ya siku inayofuata hadi saa tatu asubuhi alishangaa mumewe hajaamka hali ambayo si kawaida yake, hivyo aliamua kugonga mlango bila kuitikiwa ndipo aliamua kuuvunja na kukuta amefunga kamba kwenye dari na kujinyonga.
“Nilishtuka sana na kuanza kupiga kelele na kuita watu na walivyokuja majirani ndio watashughulikia hadi mwili wake kufikishwa mochwari” amesema.
Diwani wa viti maalumu kata ya Sinoni, Sophia Mwidan amesema kuwa alipata taarifa akiwa mgonjwa lakini alifika eneo la tukio na kukuta mwananchi wake amejinyonga.
“Sijawahi kusikia ugomvi wowote uliowashinda wanandoa hawa na kufikisha kwetu, zaidi nasikia huyu mwanaume huwa analewa na kuanguka hadi kwenye mitaro na mkewe huwa anafuatwa na kwenda kumchukua.”
“Nitoe ushauri kwa wananchi wetu, kama kuna jambo unahisi liko nje ya uwezo wako basi fikisha kwenye ngazi ya Serikali tunaweza kusaidia, kuliko hadi unafikia hatua hiyo ya kugharimu maisha yako, nawaomba sana tusifikie hatua hiyo,”amesema Mwidan.