Aliyembaka mwanafunzi wa darasa la kwanza mikononi mwa Polisi

Njombe. Jeshi la Polisi mkoani Njombe linamshikilia Daniel Kafyulilo (39) mkazi wa Chaugingi halmashauri ya mji wa Njombe kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa darasa la kwanza (6) wa Shule ya Msingi Selestini iliyopo mkoani humo.

Hayo yamebainishwa leo Mei 27,2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya jeshi hilo.

Amesema kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo wa ubakaji kumetokana na taarifa za raia wema walizozitoa kwa jeshi hilo kwa kushirikiana na wazazi wa mtoto huyo.

“Kwa hiyo uchunguzi wa jalada hili unaendelea na utakapokamilika mtuhumiwa huyu atafikishwa mahakamani” amesema Banga.

Ametoa wito kwa wakazi wa Njombe kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo katika kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu, na kusisitiza wazazi kuwaelekeza watoto wao kutembea makundi wanapoenda na kurudi shuleni.

Mkazi wa Njombe, Joseph Roja amesema uongozi wa shule uzungumze na wazazi juu ya kuwapeleka na kuwafuata watoto baada ya masomo.

“Tumesikia watoto wengi wamebakwa na hii imerudia kama awamu ya pili katika shule hiyohiyo changamoto ni msitu uliopo karibu na shule,” amesema Roja.

“Tunaiomba Serikali haya matukio yakomeshwe au huyu mtu anaweza kuwa mmoja anafanya matukio haya kwa nini yajirudie kwa nyakati tofauti” amesema Batwel Kadege mkazi wa Njombe.